RC Mbeya aagiza maofisa lishe kutoa elimu wasiobadilisha mlo

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera akihutubia wananchi wa Kata ya Inyala Halmashauri ya Mbeya katika uzinduzi wa mradi wa lishe ya mwanao. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera wakati akizindua mradi wa lishe ya mwanao, unaotekelezwa na Shirika la CRS kwa ufadhiri wa Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mafaifa Linalohudumia Wanawake na Watoto (UNICEF).
Mbeya. Katika kukabiliana na changamoto ya Udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano, Mkoa wa Mbeya umefanikiwa kupunguza changamoto hiyo kutoka wastani wa asilimia 9.8 mpaka asilimia 1.4, huku wito ukitolewa elimu kwa wasiobadilisha mlo.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera leo Jumanne, Mei 27, 2025, wakati akizundua mradi wa lishe ya mwanao unaotekelezwa katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Inyala Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ukishirikisha wadau mbalimbali wakiweoo wananchi wa vijiji vya pembezoni sambamba na kutoa elimu ya uandaaji wa lishe bora kwa watoto.
Dk Homera amesema kupungua kwa takwimu ni kutokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na mkoa ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na masuala ya lishe.
Aidha katika hatua nyingine amewataka maofisa lishe kutoa elimu kwa watu wazima kuzingatia namna bora ya ulaji wa vyakula badala ya kutumia mlo mmoja kila siku.
"Mbali na kuliwekea mkazo kundi la watoto suala la lishe elimu itolewe hata kwa watu wazima ili kuwajengea uwezo wa uandaaji wa chakula kwa watoto ili kukabiliana na tatizo la ukondefu na udumavu kwa watoto," amesema.
"Kwanza niwapongeza maofisa lishe kwa hatua nzuri ya kupunguza tatizo la ukondefu kutoka wastani wa asilimia 2.7 mpaka 0.6, udumavu kutoka asilimia 9.8 mpaka 1.4 sambamba na uzito uliopitiliza kutoka asilimia 5.3 mpaka 5.2,"amesema.
Amesema hilo ni jambo la kujivunia, lakini nitoe wito endeleeni kutoa elimu kwa jamii kujua namna bora ya uandaaji wa chakula na aina ya vyakula ili Mbeya tufikie asilimia 0 ya udumavu.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mwakilishi wa Unicef, Ophilia Katumuna amesema una lengo la kupunguza udumavu kwa watoto na kuboresha matokeo ya lishe kwa vijana kupitia mifumo ya jamii iliyo himarishwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera akiangalia aina ya vyakula vya lishe vilivyo andaliwa wakati wa uzinduzi wa mradi wa lishe ya mwanao. Picha na Hawa Mathias
Ophilia amesema hali ya udumavu kwa Mkoa wa Mbeya ni asilimia 32 ambayo iko juu kidogo ya wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 30, licha ya kuzalisha mazao mchanganyiko ya chakula na biashara katika kila msimu.
"Bado tunaendelea na jitihada mbalimbali za kutoa elimu ya lishe, lengo ni kuona kwa asilimia kubwa tatizo la udamuvu linapungua au kuisha kabisa,"amesema.
Meneja mradi wa lishe ya mwanao kutoka Shirika la CRS, Dorice Munisi amesema walengwa wakubwa kupitia mradi huo ni watoto chini ya miaka mitano, mama wajawazito, vijana wa rika balehe, wanaume vinara pamoja na jamii.
Amesema lengo kuu la mradi ni kuhamasisha ulaji, ulishaji wa watoto wachanga na walio chini ya miaka mitano kwa kutoa elimu ya kuongeza matumizi bora ya virutubishi na ufutiliaji wa ukuaji wa watoto.
"Lakini pia kukuza na kuongeza matumizi ya kuhamasisha jamii kuboresha hali ya lishe mashuleni kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wa uelewa wa masomo na kuongeza kiwango cha ufauru,"amesema.
Kauli za wananchi
Mkazi wa Kata ya Isanga jijini hapa, Ester John amesema mbali ya mkoa kufanikiwa kupunguza tatizo la udumavu bado elimu inapaswa kutolewa kwa kundi la mabinti balehe waliopata mimba za utotoni.
"Kundi hilo ni changamoto halina muda wa kuhudumia watoto katika suala la matunzo na lishe bora hali ambayo inachangia kukwamisha serikali kufikia malengo yaliyokusudiwa," amesema.