Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Faida maziwa ya mbuzi kwa watoto wadumavu

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wanasema maziwa ya mbuzi yanafanana kwa karibu na maziwa ya mama kwa uwezo wake wa kumeng’enywa kwa urahisi, hali inayoyafanya kuwa chaguo bora katika kuboresha afya za watoto walio hatarini.

Katika jitihada za kupambana na tatizo sugu la lishe duni na udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Dodoma, maziwa ya mbuzi yameonekana kuwa mkombozi mkubwa kwa familia masikini wilayani Bahi na Chamwino.

Watoto waliokuwa wakikabiliwa na utapiamlo wameanza kupata afueni ya kiafya,  kwa kutumia maziwa hayo yenye virutubisho muhimu.

Wataalamu wa afya wanasema maziwa ya mbuzi yanafanana kwa karibu na maziwa ya mama kwa uwezo wake wa kumeng’enywa kwa urahisi, hali inayoyafanya kuwa chaguo bora katika kuboresha afya za watoto walio hatarini.

Kwa mujibu wa daktari wa mifugo Halmashauri ya wilaya ya Chamwino Abednego Eloti maziwa ya mbuzi yana wingi wa virutubisho vinachochea afya hasa kwa watoto wenye changamoto ya lishe duni.

Anasema maziwa hayo yana protini nyingi ambayo inahitajika katika kujenga mwili na kuupa afya njema itakayosaidia kwenye ukuaji wa mtoto.

“Maziwa mbuzi pia yana mafuta ambayo ni muhimu katika kuupa mwili nishati, virutubisho hivi na vingine vingi vinafanya mtoto akue vizuri na afya yake iimarike,”anasema Dk Abednego.

Mbali na maelezo hayo ya Dk Abednego, tovuti ya medicover inaeleza kuwa maziwa ya mbuzi yana virutubisho muhimu ikiwemo vitamin A, B2, C  na D.

Tovuti hiyo inaeleza pia maziwa ya mbuzi yana madini ya kalsium, magnesiamu na potasimu pia yana sifa ya kipekee ya kumeng’enywa kwa haraka tofauti na ilivyo kwa maziwa ya ng’ombe.

Sababu hizo na nyingine nyingi zimelifanya Shirika la Save the Children mkoani Dodoma kuweka mkazo kwenye matumizi ya maziwa wa mbuzi kukabiliana na udumavu kwa watoto katika vijiji na kata zote za wilaya za Bahi na Chamwino.

Kupitia mradi wa Lishe Yangu, Maisha Yangu unaofadhiliwa na Save The Children Korea Kusini , watoto waliokumbwa na changamoto zinazotokana na lishe duni ikiwemo udumavu na utapiamlo wamepewa mbuzi wa maziwa ili wayatumie maziwa hayo na kupata manufaa ya kiafya.

Mradi huo ambao umekuwa msaada kwa watoto wanaotoka kwenye kaya maskini, hauishii tu kutoa mbuzi wa maziwa bali elimu ya lishe kwa watoa huduma za afya kwenye vijiji husika na wahudumu wa afya ngazi ya jamii na hatimaye elimu hiyo kufika kwa jamii.

Mtaalamu wa lishe na mratibu wa mradi wa Lishe Yangu, Afya Yangu Mariam Mwita anasema tathmini ya ripoti ya lishe ilionesha Dodoma ina changamoto ya udumavu kwa asilimia 37 hivyo wakatafuta namna ya kukabiliana na changamoto hiyo ndipo ukaanzishwa mradi huo.

Tuliangalia ni maeneo gani yana changamoto zaidi ndipo tukachagua Bahi na Chamwino kwa kuvifikia vijiji vyote. Tukaanza kutoa elimu ya lishe kwa watoa huduma za afya kwenye zahanati na watoa hudama wa afya ngazi ya jamii ambao hawa ndiyo wanawafikia wanajamii moja kwa moja. Elimu hiyo inahusisha mpangilio wa vyakula, zile jamii nyingi ni maskini hivyo tukawafundisha wanavyoweza kupata mlo wa lishe katika mazingira yao. Tulitoa mbegu ili walime mbogamboga na matunda na kwa zile kaya zenye watoto ambao tayari wameathirika tuliwapa mbuzi wa maziwa,” anasema na kuongeza:

“Katika ufuatiliaji wetu tulibaini maziwa ya mbuzi yana virutubisho muhimu kwa afya na pia uyeyushwaji wake upo karibu sawa na maziwa ya mama tofauti na ilivyo kwa maziwa ya ng’ombe.Hata hivyo tunasisitiza mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwa miezi sita baada ya hapo ndipo anapoweza kuongezewa maziwa ya mbuzi kwa sababu haya yanayeyushwa vizuri kama ilivyo maziwa ya mama,”.

Ndikirai Tupa mkazi wa kijiji cha Mlowa barabarani wilayani Chamwino ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo, anayekiri kwamba hapo kabla afya ya mtoto wake ilikuwa ikitetereka hadi kulazwa kwa sababu ya kukosa lishe bora.

“Huku kwetu mtoto anakula kile kinachopatikana hivyo ugali na mlenda ndiyo chakula chetu na watoto tunawalisha hivyo hivyo. Sikujua kwamba nafanya makosa yatakayohatarisha afya ya mtoto wangu.

Akawa anaumwa mara kwa mara, nikienda kliniki uzito wake haungozeki badala yake unashuka, ikafikia hatua akawa anawekewa dripu za lishe. Manesi wakawa wananiambia hiyo siyo nzuri nijitahidi katika kuhakikisha mtoto anapata lishe bora, maneno yao niliyaelewa lakini sikuwa na cha kufanya,” anasema na kuongeza:

Haikupita muda mrefu ndipo mradi huu ukaja ukiwalenga watoto kutoka kwenye familia duni, kupitia watoa huduma za afya ngazi ya jamii na mimi nikaingizwa nikaanza kupewa elimu ya lishe pamoja na kupewa mbuzi wa maziwa na mbegu za mboga mboga,”

Anasema kadiri alivyokuwa akipewa elimu taratibu alianza kuzingatia kumpatia mtoto makundi yote ya chakula kulingana na kipato chake hadi pale alipopata mbuzi.

“Elimu ilinisaidia sana, nikawa nahakikisha mtoto anapata makundi yote ya chakula, nilipopata mbuzi nilimhudumia vizuri hadi alipoanza kutoa maziwa ikawa kama suluhisho la tatizo la mwanangu.

Ikawa kila siku lazima nimpikie uji wenye maziwa ya mbuzi na wakati mwingine nilimchemshia maziwa akanywa. Taratibu afya yake ikaanza kubadilika, uzito ukaongezeka na kupitiliza hadi manesi sasa wakaniambia nipunguze lishe maana uzito ukiongezeka zaidi inaweza kuwa hatari kwa mtoto,” anasema Ndikirai.

Kwa upande wake,  Hamida Omari mkazi wa kata ya Dabalo wilayani Chamwino naye anasimulia namna maziwa ya mbuzi yalivyonusuru afya ya mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka miwili aliyebainika kuwa na utapiamlo mkali.

Hamida  alichukua jukumu la kumlea mtoto huyo baada ya kufiwa na mama yake mzazi akiwa na mwezi mmoja hivyo kwa kiasi kikubwa alikosa lishe.

“Mwezi mmoja baada ya kuzaliwa Hamza, mama yake alifariki, ikabidi nichukue jukumu la kumlea lakini hata mimi sikuwa na uwezo hivyo akawa anakula kile kinachopatikana na kwa kuwa mimi ni mama lishe alikula vyakula vya kwenye biashara yangu.

Hali iliendelea hivyo, hadi siku moja nilipompeleka kliniki na kuambiwa kwamba mtoto ana utapiamlo hivyo nifanye jitihada za kuhakikisha anapata lishe bora kinyume na hapo mambo yanaweza kuwa mabaya,” anasema Hamida.

Taarifa za utapiamlo wa Hamza, zinathibitishwa na mhudumu wa afya ngazi ya jamii kata ya Dabalo, Erica Kahuluse ambaye anasema walibaini hali ya hatari kwa mtoto huyo na kuanza kumfuatilia.

Erica anasema kupitia mahudhuria ya kliniki ilibainika kuwa uzito wa mtoto huyo,  unashuka badala ya kupanda na alikuwa katika hali ya hatari, hivyo akaanza kufuatiliwa kwa ukaribu.

“Huwa tunashirikiana na watoa huduma za afya kwenye zahanati za vijiji, nilipata taarifa kuhusu huyu mtoto ambaye mama yake alifariki, hivyo hakuwa akipata maziwa ya mama na ikaonekana hata lishe hapati ndiyo sababu afya yake inazidi kuzorota na amepata utapiamlo mkali.

Tukaanza kumfuatilia kuanzia anakoishi tukagundua kuna changamoto, akaanzishiwa chakula dawa, bahati nzuri huu mradi wa lishe ukaja kwenye kata yetu tukaona tumuingize huyu mama ili ajifunze kuhusu lishe na apate mbuzi wa maziwa,” anasema na kuongeza:

“Ukweli ni kwamba kuna mabadiliko makubwa kwa sasa kwa huyu mtoto, afya yake inaimarika siku hadi siku, ule utapiamlo umekwisha kabisa. Kila siku anakunywa maziwa na yamemsaidia kwa kiasi kikubwa kuwa hivi alivyo sasa,”

Mtoa huduma huyo anaeleza kuwa katika vijiji vingi wilayani Chamwino kuna tatizo la watu kutozingatia lishe, hali inayosababisha watoto kupata udumavu na utapiamlo.

Si kwamba hakuna vyakula, watu hawana muda wa kutafuta elimu ya lishe na kuzingatia yale wanayoambiwa na watalaamu, ndiyo sababu unakuta mtoto chini ya miezi sita anaanza kupewa chakula. Tunaendelea kutoa elimu hii kwa wanajamii ila naona bado elimu zaidi inahitajika hasa maeneo ya vijijini,”.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya ya Bahi, Boniface Wilson anakiri kuwepo kwa tatizo la udumavu hasa katika vijiji vya pembezoni kutokana na kukabiliwa na umaskini.

Wilson anasema jamii nyingi katika maeneo hayo hazina uelewa wa kutosha kuhusu lishe, hivyo zipo familia ambazo watoto huangukia kwenye udumavu.

“Huku wengi wanategemea kilimo na ufugaji, vyote hivi vinategema hali ya hewa sasa nyakati za ukame hali inakuwa mbaya zaidi na ndiyo tunashuhudia watoto wakiwa na udumavu na utapiamlo.

“Ni kweli bado kuna uelewa mdogo wa masuala ya lishe, elimu inahitajika ili wananchi wajue umuhimu wa lishe na namna ya kuzingatia lishe bora hasa kwa watoto ndiyo sababu tunashirikiana bega kwa bega na wadau wanaotuletea miradi yenye tija kama huu wa Lishe yangu, Maisha yangu,” anasema Wilson.

Mradi huo unalenga kuwafikia watu 9800 kati yao wamo wanawake wenye umri wa kuzaa, wanawake wenye watoto chini ya miaka mitano na watoto wao, watoa huduma za afya na watoa huduma za afya ngazi ya jamii katika halmashauri za Bahi na Chamwino.