Ziwa Victoria laongoza idadi ya vyombo majini

Muktasari:

  • Serikali imetoa takwimu za vyombo vya majini nchini huku ikieleza hatua inazochukua kwa wanaozidisha abiria na mizigo.

Dodoma. Serikali imesema Tanzania ina jumla ya vyombo vya majini 52,189 huku ziwa Victoria likiongoza kwa kuwa na vyombo vingi kwa asilimia 53.6

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 30, 2023 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge Mwantumu Haji.

Mbunge huyo alitaka kujua idadi ya vyombo vya majini nchini na adhabu wanazopewa kwa vyombo vinavyozidisha mizigo na abiria.

Akijibu maswali hayo, Mwakibete amesema kuwa sensa iliyofanywa na Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ulibaini kuwa vyombo vya majini ni 52,189.

Amesema kati ya vyombo hivyo asilimia 53.6 vipo katika ziwa Victoria huku asilimia 13.4 viko kwenye Bahari ya Hindi.

Kuhusu faini amesema faini inayotozwa kwa kuzidisha mizigo na abiria ni Sh200,000 kwa chombo chenye urefu wa chini ya mita 24 wakati kilicho juu ya urefu huo kikitozwa Sh400,000.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo amehoji kuna mpango gani wa kudhibiti vyombo vya Baharini vinavyozidisha mizigo na abiria.

Akijibu swali hilo, Mwakibete amesema TASAC hufanya ukaguzi kuhakikisha Meli inapakia mzigo bila kupitiliza mstari wa ujazo uliothibitishwa na msajili.

Amesema endapo itabainika kuwa meli imezidisha ujazo wa abiria, mizigo au vyote kwa pamoja itakuwa imetenda kosa kisheria.

“Meli hiyo itapaswa kuzuiliwa bandarini na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) itajulishwa ili kusitisha kutoa kibali kwa meli hiyo kutoka bandarini hapo,”amesema.

Amesema kwa hatua zaidi, TASAC humtoza mmiliki au nahodha wa meli faini na kisha kusimamia upunguzwaji wa abiria, mizigo au vyote kwa pamoja kisha kuruhusu meli hiyo pindi mkaguzi atakapojiridhisha kuwa meli ipo salama kwa kuanza safari.