DC Kasulu awataka madiwani kudhibiti uhamiaji haramu

Madiwani Halimashauri ya Kasulu Mjini wakiwa katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka 2024/25
Kasulu. Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, ametoa wito kwa madiwani wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika kuwahifadhi raia wa kigeni wanaoingia nchini bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesema vitendo hivyo vimechangia kuongezeka kwa matukio ya kihalifu, hususan katika baadhi ya vijiji na kata za halmashauri hiyo, zikiwemo wizi wa mazao na uvamizi wa mali za wananchi.
Akizungumza jana, Mei 5, 2025, wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani unaojadili taarifa ya utekelezaji wa robo ya tatu (Januari–Machi) ya mwaka wa fedha 2024/2025, Kanali Mwakisu alieleza kuwa Kata ya Muhunga imekuwa miongoni mwa maeneo yanayohusishwa na vitendo vya kuwahifadhi wahamiaji haramu, jambo linalosababisha hali ya usalama kuwa ya wasiwasi.
“Kwa sasa hali ya usalama katika maeneo yetu imeanza kuwa ya wasiwasi. Kuna taarifa kwamba baadhi ya vijiji vimekuwa na matukio mengi ya kihalifu, na upenyo wa watu kuvuka mipaka bila kufuata utaratibu. Inaonekana tunapokea wakimbizi wapya bila kujua,” amesema Kanali Mwakisu.
Amesisitiza kuwa ili kukabiliana na hali hiyo, jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu hatari za kuwapokea wageni wasiojulikana, na akawataka madiwani kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya usalama na kuanzisha mifumo ya ulinzi shirikishi kwenye maeneo yao.
“Usalama wetu uko mikononi mwetu. Muhunga ni eneo la kutazamwa kwa karibu kuna dalili za watu kupitishwa bila utaratibu. Tukatae hali hii kabla haijawa janga. Nawapa tahadhari mapema,” ameongeza.
Kufuatia agizo hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Muhunga, Dorcas Swai, amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kudhibiti wizi wa mara kwa mara unaojitokeza katika eneo hilo, ambalo lipo mpakani mwa Tanzania na Burundi.
“Awali taarifa hizi hatukuwa nazo rasmi, lakini sasa tumeanza kuwaagiza wenyeviti wa mitaa kuhakikisha wanapata taarifa za wageni wote wanaoingia katika maeneo yao, pamoja na wale wanaopangisha nyumba kuhakikisha wanajua historia ya wapangaji wao,” amesema Swai.
Ameongeza kuwa Machi, Shule ya Msingi ya Nyandula ilivamiwa na kuibiwa, na kwamba matukio ya wizi wa mazao yamekuwa yakiongezeka, hali iliyosababisha kuundwa kwa kamati ya ulinzi shirikishi ngazi ya kata kwa kushirikiana na mgambo na viongozi wa vijiji.

Watendaji wa Kata za Halimashauri ya Kasulu wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani
Kwa upande wao, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo walikiri kuwa changamoto hiyo inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi, kupitia elimu ya usalama na ulinzi wa pamoja.
“Tunahitaji mshikamano wa kweli. Ulinzi shirikishi ni suluhisho muhimu dhidi ya wahamiaji haramu ambao wamekuwa chanzo cha ongezeko la wizi na uporaji wa mali za wakulima na wafanyabiashara wetu,” amesema mmoja wa madiwani.