Zelothe afariki dunia, CCM yamlilia

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen enzi za uhai wake
Muktasari:
- Chama cha Mapinduzi CCM, kimesikitishwa na taarifa ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha Zelote Stephen.
- Zelote amewahi kukitumikia chama na serikali katika nafasi mbalimbali akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni.
Dar es Salaam/Arusha: Chama cha Mapinduzi CCM, kimesikitishwa na taarifa ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha Zelothe Stephen.
Zelothe aliyewahi kukitumikia chama na serikali katika nafasi mbalimbali akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, amefariki leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyolewa kwa niaba ya familia kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa,imesema taarifa za kifo cha kiongozi huyo wa chama mkoa, zimewapa simanzi.
"Kwa masikitiko makubwa, kwa niaba ya familia, naomba kuleta taarifa za kifo cha Mzee Zelothe Steven kilichotokea leo Dar es Salaam alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu,” imeeleza taarifa hiyo ya Waziri Silaa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mipango ya maziko inafanywa nyumbani kwa marehemu Sea view Upanga, jijini Dar es Salaam, na kwamba maziko yanatarajiwa kufanyika nyumbani kwake Olasiti Arusha kwa tarehe itayotangazwa.
“Kwa kuwa ni ngumu kumtaarifu kila mmoja, naomba mpokee taarifa hii kwa wote. Tumwombee marehemu na tuiombee familia katika kipindi hiki cha msiba,” imeeleza sehemu ya andiko hilo la Waziri Silaa.
Kwa upande mwingine Katika Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ambaye katika akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, ameweka picha ya marehemu Stephen huku akiandika maneno yanayoonyesha kuumizwa na msiba huo.
“Taarifa za kuondokewa na Zelothe Stephen, Mwenyekiti wetu wa CCM mkoa wa Arusha ni taarifa za kusikitisha sana. Kwani kwa hakika kifo chake kimetunyika fursa muhimu ya kuendelea kujifunza mengi na kuuishi uongozi wake,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen enzi za uhai wake
“Mungu ameendelea kutufunza. Mipango yetu imekwama. Nenda Laigwanan. Nenda mzee wangu. Nilipokutembelea siku chache zilizopita hospitali ulinipa matumaini. Kumbe mipango ya Mungu ikabaki. Wewe ni shujaa, Nenda Kamanda.”
Akizungumza na Mwananchi Digital usiku huu, Katibu wa CCM mkoa Arusha, Mussa Matoroka amesema wamepata taarifa za kifo cha mwenyekiti wao jioni.
"Ni kweli Mwenyekiti amefariki jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa amekwenda kupatiwa matibabu...huu ni msiba mkubwa kwetu CCM, familia ndugu na Jamii," amesema.
Matoroka amesema watamkumbuka Zelothe kwa kuweza kuwa kiungo kizuri baina ya CCM na Serikali lakini pamoja na vyombo vingine vya usalama.
"Alikuwa kiongozi makini mchapakazi na mzalendo, taratibu za kurejeshwa mkoani Arusha na maziko zitatangazwa," amesema Matoroka
Kwa upande wake Katibu wa Mwenezi Mstaafu wa chama hicho mkoa huo, Gerald Munisi ambaye amewahi kufanya kazi na marehemu, amesema wamepokea kwa masikitiko msiba.
"Ni kweli ametutoka Mzee Zelothe alikuwa ni mgonjwa tumepokea kwa masikitiko msiba huu," amesema.
Kwa mara ya kwanza marehemu Zelothe, alichakuguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Desemba 2019, akichukua nafasi ya Loota Sanare ambaye aliteuliwa na Rais wa wakati huko, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, akichukua nafasi ya Dk Stephen Kebwe ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Hata hivyo, Novemba 2022 Kamanda Zelothe alifanikiwa kuitetea nafasi yake na hivyo kuendelea kuongoza chama hicho mkoani Arusha mpaka mauti ilipomkuta.