NIT kuwa kituo cha mitihani ya leseni za kimataifa

Muktasari:
- Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) yapata ithibati kutoka wakala wa Usalama wa Anga Ulaya kuwa kituo cha mitihani ya leseni za kimataifa uhandisi matangenezo ya ndege
Dodoma. Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana na Athens Aviation Training Organization ya nchini Ugiriki imepata ithibati kutoka Wakala wa Usalama wa Anga wa Ulaya (European Aviation Safety Agency - EASA) ya kuwa Kituo cha Mitihani ya Leseni za Kimataifa kwa wahandisi matengenezo ya ndege.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Mei 15, 2025 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Profesa Mbarawa amesema NIT kitakuwa Kituo cha Mafunzo ya Uhandisi Matengenezo ya Ndege (EASA Part -147 Maintenance Training Organization).
“Mafanikio haya ni ya kipekee na ya aina yake kwa nchi yetu na yatawezesha wataalamu wetu kuwa na ubora na vigezo stahiki vya ushindani wa soko la ajira kikanda na kimataifa kwani Serikali kupitia Chuo cha NIT imepata ithibati ya kuanza mafunzo ya Urubani kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA). Mafunzo haya yanatarajia kuanza rasmi mwezi Juni 2025,” amesema Mbarawa.
Amesema kwa sasa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimeendelea kutoa Mafunzo ya kozi ndefu 48 za kimkakati ili kuzalisha wataalamu mahiri wa kuendeleza miradi mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa na Serikali.
“Chuo kina wanafunzi wa kozi ndefu 17,701 ikilinganishwa na wanafunzi 16,131 kwa mwaka 2023/24, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.7,” amesema.
Hilo linafanyika wakati ambao NIT kimeendelea kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu na vifaa vya kufundishia ikiwemo uundwaji wa ndege moja yenye injini mbili kwa ajili ya kufundishia marubani unaendelea nchini Marekani huku ndege hiyo ikitarajiwa kuwasili Chuoni Oktoba 2025.
“Serikali kupitia Chuo cha NIT imeendelea na utekelezaji wa mradi wa uanzishwaji wa kampasi ya NIT mkoa wa Lindi kwa ajili ya kuzalisha Nguvukazi Mahiri na kujenga uwezo wa kiteknolojia katika sekta ya usafiri majini, mafuta na gesi,” amesema.
Pia NIT kinaendelea na utekelezaji wa shughuli za uanzishwaji wa Kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga na operesheni za usafirishaji kitakachoanzishwa chini ya Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP) ambapo kimeshatekeleza kazi mbali mbali.
“Chuo kimeshatekeleza ujenzi wa majengo matano yanayojengwa katika kampasi ya Mabibo Dar es Salaam ambapo Mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,504 umekamilika na ujenzi wa majengo matatu yenye madarasa 10, maabara 15, karakana tano na ofisi za watumishi 25 umefikia asilimia 96,” amesema.
Mambo mengine yaliyotekelezwa kwa mujibu wa Mbarawa chuoni hapo ni pamoja na ujenzi wa jengo la Karakana ya Matengenezo ya Ndege (Aviation Hangar) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) itakayotumika kuhifadhia ndege za mafunzo ya urubani na matengenezo ya ndege hizo pamoja na mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege upo kwenye hatua ya kumpata mkandarasi.
“Wameshafanya ununuzi wa vifaa vya mafunzo ya urubani na uhandisi wa matengenezo ya ndege ikiwemo Flight Simulators mbili (2) na programu za Kompyuta (softwares) kwa ajili ya maabara, madarasa na ofisi katika Kampasi ya NIT Mabibo - Dar es Salaam na KIA umefikia asilimia 70,” amemalizia Waziri Profesa Mbarawa.