Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Latra, NIT waja na mkakati kupunguza ajali

Muktasari:

 Mafunzo hayo ni ya siku saba kwa watoa huduma kwa mabasi ya masafa marefu na ya mjini

Mbeya. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema muda ukifika itaanza kutekeleza kanuni za kuwataka wamiliki wa mabasi kuajiri watoa huduma waliopata mafunzo ili kudhibiti ajali za mara kwa mara na changamoto kwa abiria.

Akizungumza leo Februari 26, 2024 wakati wa mafunzo kwa watoa huduma kwa mabasi ya masafa marefu Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyoandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),  Meneja Leseni wa mamlaka hiyo, Leo Ngowi amesema wanahitaji kuona wamiliki wote wanaajiri watoa huduma waliopitia mafunzo.

Amesema kwa sasa bado hawajaanza kutekeleza kanuni hizo, licha ya kuwa tayari zimeshaandaliwa, lakini baada ya mafunzo watakaa ndani ya miezi mitano kufanya tathimini kisha kuanza utekelezaji.

“Lengo kubwa ni kupunguza au kuondoa hizi ajali na changamoto za abiria, kwa sasa mafunzo ni bure ila baadaye kutakuwa na gharama, hatutakubali kuona mhudumu wa basi ambaye hana cheti za mafunzo wale watakaokiuka sheria hii hatutasita kusitisha leseni," amesema Ngowi.

Akifungua mafunzo hayo ambayo yatadumu kwa siku saba jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kubadilika kuanzia lugha na kuweka usalama wa mali na abiria.

Amesema kwa sasa mabasi ya masafa marefu yamebadilika hasa kwa madereva na wasaidizi wao.

Homera amesema wengi wao wamekuwa makini hali inayosaidia kupunguza ajali zilizokuwa zimekithiri mkoani humo.

"Niwapongeze NIT kwa kuandaa mafunzo haya, hii ni fursa kwenu katika ufanisi kwenye majukumu yenu, jifunzeni lugha kwa mteja, kagua chombo chako kabla ya safari na lindeni usalama wa abiria na mali zao,"amesema Homera.

"Hivi karibuni ilishuhudiwa basi limebeba watoto sita bila kufahamu walijipenyeza chini kwa chini ikaja kugundulika wamefika Morogoro, hivyo inahitaji umakini."

Kaimu Mkuu wa NIT Taaluma na Utafiti, Dk John Mahona amesema wanatoa mafunzo hayo ili kusaidia wahudumu wa mabasi hayo kuondoa changamoto zinazowakabili.

"Niwaombe washiriki kutulia na kujifunza, mafunzo haya yatasaidia katika majukumu yenu hasa kwa haya mabasi ya masafa marefu na mjini, yataondoa na kukujenga kukabiliana na changamoto,” amesema Dk Mahona.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Amina Hassan amesema wanatarajia mafunzo hayo kuwajenga namna ya kutoa huduma kwa abiria, usalama wao na mizigo.

"Lakini suala la lugha katika kuhudumia, ukaguzi wa chombo cha moto kabla ya safari na usalama wa mali na abiria ndio mambo tunatarajia kujifunza ili kufanya kazi kwa ufanisi," amesema Amina mhudumu wa basi Kampuni Achimwene.