Prime
Wastaafu hatujasikilizwa kwenye hili

Mstaafu bado anaugulia maumivu yake aliyozawadiwa na mheshimiwa waziri mmoja wa Siri-kali Oktoba mwaka jana, aliyetangaza hadharani na mbele ya waandishi wa habari kuwa Siri-kali ilikuwa imeamua kuwaongeza wastaafu shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yao ya mwezi ya “laki si pesa” kuanzia Januari mwaka huu.
Baada ya miaka 21 ya kuomba, kutaka na kuomboleza kuhusu kuhitaji nyongeza ya pensheni, wastaafu tulitegemea kuwa Siri-kali ingeelewa kwa kuwapa wastaafu wake japo nyongeza ya shilingi laki moja na si shilingi elfu hamsini tu, baada ya kilio chao cha miaka 21, tokea yule muungwana wa Msoga alipowapa wastaafu nyongeza ya shilingi elfu hamsini miaka 21 iliyopita, ikaishia kuwa “laki si pesa”! Hakuna aliyejali, wala anayejali.
Kilichotokea Januari ni mstaafu tu anayejua maumivu yake. Baada ya kilio na maumivu ya miaka 21 ya kutaka nyongeza ya pensheni, huku akitakiwa kuisubiri nyongeza hiyo kwa miezi mitatu kwanza, toka Oktoba mwaka jana hadi Januari mwaka huu, sijui kwa nini, huku mstaafu wetu akishitukia dili na kuwataka wastaafu wenzake waanze kukaa chonjo, saa itakuwa mbaya... na ndivyo ilivyokuwa!
Wastaafu wameishia kupata kati ya shilingi elfu saba hadi elfu kumi kama nyongeza ya pensheni yao, badala ya shilingi elfu hamsini waliyoahidiwa! Hayo yasingekuwa maumivu sana kwa wastaafu kama yule mheshimiwa waziri ambaye alisimama kwa bashasha kadamnasi Oktoba na kutueleza wastaafu kuwa hatimaye Siri-kali ilikuwa imesikia kilio chetu na kuamua kutupa nyongeza ya shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yetu ili “tuweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha” iliyokuwa inawakabili wastaafu, angetimiza ahadi hiyo.
“Ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayowakabili”, kwa nyongeza ya shilingi elfu hamsini? Wee haya wee! Kweli aliyeshiba hamjui mwenye njaa.
Wawakilishi wetu wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kwa mshahara wa shilingi milioni... mama wee!... 14 kwa mwezi, lakini wastaafu wa taifa wakabiliane na hali ngumu ya maisha kwa shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi? Wahusika, hebu acheni hii mizaha mibaya kwa maisha ya wastaafu!
Shilingi elfu hamsini, mpaka shilingi elfu kumi kama nyongeza ya pensheni ya mstaafu mnayosema kwa bashasha kuwa ni ya kumsaidia mstaafu huyu kukabiliana na hali yake ngumu ya maisha? Waheshimiwa, tusisitize, acheni utani mbaya kwa maisha ya wastaafu, ambao Kinondoni inawakonyeza kwa nguvu zote tuende kuwa wakazi wake.
Msitufikishe mahali pa kuona kwamba ni heri kuwa wakazi wa Kinondoni kuliko wa Burundi, tulikoshauriwa kwa kejeli twende!
Ndiyo, hajajitokeza waziri au mheshimiwa yeyote anayehusika kueleza ni kwa nini wastaafu wameishia kupata nyongeza ya shilingi kuanzia elfu saba hadi kumi, tofauti kabisa na shilingi elfu hamsini waliyoahidiwa na Siri-kali, na hakuna yeyote anayejitokeza kutoa maelezo yoyote.
Vyombo vya habari vilivyoiandika habari hii kurasa zao za mbele hakuna chombo cha habari hata kimoja ambacho kimefuatilia habari hii ili angalau kujua shilingi elfu hamsini iliyoahidiwa na Siri-kali imegeukaje kuwa shilingi elfu kumi! Na shilingi elfu arobaini zao ziko wapi?
Siri-kali ilituambia kwamba inatupa nyongeza ya shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yetu ya “laki si pesa” ili tuweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha. Walichokifanya Siri-kali kimekuwa: "Zilongwa mbali, zitendwa mbali" (Kijerumani nini ili kusisitiza!). Badala ya kuboresha maisha ya mstaafu ili aweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha, ilichofanya Siri-kali ni kuyanyong’onyeza zaidi maisha ya mstaafu na hakuna anayeonyesha kulijali hili. Ndivyo wastaafu tunavyofanyiwa kwenye nchi hii tuliyoijenga wenyewe!
Siyo mheshimiwa Rais, siyo waheshimiwa mawaziri, wala siyo wawakilishi wetu bungeni wanaopokea milioni... mama wee tena!... 14 kwa mwezi, anayeonekana kuumizwa na hili la Kijerumani “Zilongwa mbali, zitendwa mbali”.
Hakuna hata mmoja anayeuliza: “Hivi kwa nini wastaafu wetu wa taifa tuliowaahidi nyongeza ya shilingi elfu hamsini tumeishia kuwapa shilingi elfu kumi? Kwa nini? Shilingi elfu arobaini zao zimepelekwa wapi?” Hakuna anayeuliza, hakuna anayejibu, wala hakuna anayetoa maelezo!
Nyongeza ya mstaafu imeishia kuwa: “santakalawe amina, mwenye kupata apate, mwenye kukosa atajiju…”!
Ndipo wastaafu tuliojenga nchi yetu hii kwa jasho na damu yetu tulipofikishwa pa kuonekana hatustahili kupata hata shilingi elfu hamsini ya nyongeza ya wastaafu baada ya kuifukuzia kwa miaka 21! Kwamba eti stahili yetu ni shilingi elfu kumi tu ili kuboresha hali ngumu ya maisha inayotukabili.
Hakuna anayejali wala kufuatilia zilikoyeyukia! Yaani ni kama Siri-kali imetupa, kwa shingo upande, shilingi elfu hamsini kwa mkono wa kulia, na kuchukua shilingi elfu arobaini kwa mkono wa kushoto! Mwe.
Mwaka jana, kibubu chetu kimetangaza kuwa kitakuwa kinatoa shilingi milioni tano kwa wategemezi wa mstaafu pale mstaafu anapofariki. Ni jambo jema, lakini wataweza? Kama Siri-kali imeshindwa kumpa mstaafu ambaye yuko hai shilingi elfu hamsini tu za nyongeza ya pensheni alizoahidiwa, je, kibubu kitaweza kutoa milioni tano kwa wategemezi wa mstaafu aliyefariki?
Ikiwa pensheni ya shilingi elfu hamsini tu imeyeyushwa, si shilingi milioni tano za mstaafu aliyeenda Kinondoni zitaoteshwa mbawa?
Itakuwa jambo jema kibubu kikianza kufikiri kumpa mstaafu milioni tano yake wakati akiwa hai, apate faraja yake ya miaka michache iliyobaki ya kuwa duniani ajue mwenyewe vipi anawaachaje wategemezi wake. Si ni hela yake?
Mheshimiwa Rais, sema neno moja tu, roho za wastaafu zipone. Amina.
0754 340606 / 0784 340606