Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Neema ya madaraja kwa watumishi, Spika atia neno

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu.

Muktasari:

  • Hata hivyo, Spika Dk Tulia Ackson ametahadharisha kwa Serikali kuwa na msimamo katika upandishwaji madaraja kwa watumishi wanaojiendeleza kupitia taaluma zingine.

Dodoma. Serikali imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanawasilisha haraka majina ya watumishi wenye sifa za kupandishwa madaraja kabla ya mwisho wa Mei 2025 ili kuwawezesha kupandishwa madaraja kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ametoa kauli hiyo bungeni leo Ijumaa Mei 16,2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Buyungu, Aloyce Kamamba aliyetaka Serikali inampango gani wa kuwapandisha madaraja kwa mserereko walimu wenye changamoto ya kupandishwa madaraja wakiwemo walimu wa Kakonko.

Pia, Mbunge wa Viti Maalumu Sophia Mwakagenda naye aliuliza swali la nyongeza akitaka kujua kuna mpango gani wa Serikali wa kuwapandisha madaraja watumishi waliosoma kada zingine kwa gharama zao wenyewe.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, ametahadharisha Serikali kuhusu upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wa umma wanaojiendeleza kielimu katika fani tofauti na zile walizoajiriwa nazo.

“Mheshimiwa Naibu Waziri, ni muhimu kuwa waangalifu katika utaratibu huu wa kuwapandisha madaraja watumishi. Ikiwa kila anayesoma na kubadilisha mwelekeo wa taaluma ataachana na kada aliyopangiwa awali, ipo hatari baadhi ya kada muhimu kukosa wataalamu,” amesema Dk Tulia.

Akijibu swali la kupandishwa madaraja, Naibu Waziri Sangu, alitoa agizo bungeni akizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wakurugenzi wao wanawasilisha majina ya watumishi wenye sifa za kupandishwa madaraja haraka kabla ya mwisho wa Mei 2025, ili mchakato wa upandishwaji madaraja utekelezwe kwa ufanisi na kwa wakati.

Naibu Waziri amesema, kwa mujibu wa Kifungu cha 6 (1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura, 298 jukumu la kuwapandisha vyeo watumishi ni la mwajiri husika.

"Jukumu hili hutekekelezwa baada ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoa mwongozo kuwataka waajiri kuandaa na kuwasilisha Ikama na Bajeti ya Mwaka husika wa fedha na Ofisi kuridhia utekekelezaji wa bajeti hiyo," amesema Sangu.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, katika kipindi cha mwaka 2024/25, Serikali imetoa Mwongozo unaohusu upandishaji vyeo na ubadilishaji kada ikiwemo kwa watumishi waliocheleweshwa kupandishwa vyeo.

Pia, ametoa wito kwa waajiri wote nchini kutekeleza kwa wakati mwongozo huo ili kuepusha malalamiko kwa watumishi wa umma wenye changamoto za kupandishwa vyeo wakiwemo watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.

Hata hivyo, Naibu Waziri amesema katika kipindi kifupi Serikali imefanikiwa kuwapandisha vyeo jumla ya watumishi 48,186 na utaratibu unaendelea kwa wenye sifa.