Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wauguzi  walia mishahara, kupandishwa madaraja

Wakunga wakiwa kwenye matembezi ya hisani.

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha asilimia 60 ya watumishi wa idara ya afya ni wauguzi, ambao asilimia 80 ya kazi za hospitali hufanywa na kundi hilo.

Unguja/Tanga. Pamoja na kazi kubwa wanayofanya wauguzi, asilimia 60 hawajitambui wapo madaraja gani na wengine hawajawahi kupanda kwa takribani miaka 15, huku kukiwa hakuna muundo wa kiutumishi kwa kada hiyo.

Wauguzi hao wametaja vilio vyao ikiwemo mishahara midogo na kupanda madaraja licha ya changamoto lukuki wanazopitia kazini, wakidai zinarudisha nyuma ufanisi wa kazi katika kutoa huduma kwa za afya.

Hayo yamebainika leo Jumapili, Mei 12, 2024 wakati wa maadhimisho ya siku ya uuguzi duniani iliyofanyika kitaifa mkoani Tanga, huku  mgeni rasmi alikuwa  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na visiwani Zanzibar ikifanyika Unguja na mgeni rasmi akiwa Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said.

Akitoa taarifa ya ripoti ya utafiti uliofanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, hospitali za wilaya na vituo vya afya, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar, Dk Rukia Rajab amesema kati ya wauguzi 134 waliofanyiwa utafiti, asilimia 60 hawajawahi kupanda madaraja na wengine hawajui wapo katika madaraja gani.

Katika utafiti huo walihusisha wauguzi katika wodi za kawaida, majeraha, watoto, kliniki za mama na mtoto, upasuaji, magonjwa ya nje na dharura.

“Hakuna mfumo maalumu wa kupandisha madaraja, wengi hawajui wapo madaraja gani, unakuta mtu ana mwaka mmoja kazini kimasIlahi analingana na aliyefanya kazi miaka 15,” amesema na kutaja changamoto nyingine ni kukosekana uwiano wa wagonjwa na wauguzi katika hospitali hizo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wodi ya watoto, muuguzi mmoja anahudumia wastani wa wagonjwa 12, wodi ya dharura anahudumia saba, wodi ya wagonjwa mahututi anahudumia wagonjwa sita na wodi ya wagonjwa kawaida anahudumia 15.

“Serikali iajiri watu katika maeneo yenye upungufu mkubwa na kurejesha mfumo wa madaraja,” amesema

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said amesema kuna watumishi zaidi ya 500 wapo nje ya nchi kimasomo na ipo haja kuweka utaratibu wa kusubiriana kwani inaweza kutajwa kuwepo  upungufu, ilhali wapo masomoni.

“Hili Katibu Mkuu liangalie, wakati mwingine upungufu unasababishwa na ruhusa za kiholela watu kwenda kusoma,” amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Habiba Hassan Omar, amesema wanahakikisha kada ya uuguzi inaimarika kutoa nafasi ya masomo ndani na nje ya nchi kwa kupanga vipaumbele vya wizara.

“Mpango wetu tutakwenda kuangalia kada za uuguzi tuziboreshe ziweze kutumika ipasavyo katika muundo wa kutoa huduma kuanzia kwenye jamii, vituo vya afya, hospitali za wilaya hadi za rufaa,” amesema.

Naibu Waziri wa Afya, Hassan Hafidh amesema wapo baadhi ya wauguzi hawana sifa za kuwa wauguzi kwani wana kauli mbaya kwa wagonjwa.

Amesema kazi ya uuguzi ni ngumu lakini ni muhimu kuipenda na kuifanya kwa weledi ingawaje wengi  hawapendi kazi na kuiheshimu, akisisitiza kazi ni ibada hivyo ipo haja kubadilika katika utendaji kazi wao.

Dk Biteko atoa maagizo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Biteko ameiagiza Wizara ya Afya, kuja na majibu kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha,  kuhusu kubadilishwa muundo wa kiutumishi ili kutambua kada ya uuguzi na kupewa nafasi za kiutawala kama kada zingine.

Amesema muundo wa wauguzi kutopewa nafasi za kiutawala hata wanapojiendeleza kielimu, limekuwa likilalamikiwa kila wanapokutana.

"Wizara ya Afya mkaangalie upya suala la muundo huu unaoongelewa na wauguzi, kabla mwaka huu wa fedha haujaisha mtoe majibu inawezakana au hapana, ila katika mkutano ujao wa wauguzi hatuhitaji tena kusikia suala hili.

“Hivyo wauguzi wapewe majibu sahihi kwamba mabadiliko hayo yanawezekana au hapana ili kuhitimisha mjadala huu,” amesisitiza Dk Biteko.

Akitoa salamu kwa mgeni rasmi,  Rais wa Chama Cha wauguzi Tanzania (TANNA) Alexander Jumanne,  ameiomba Serikali kuziagiza mamlaka husika, kuangalia uwezekano wa wauguzi wanaojiendeleza mishahara yao kuongezeka, kwani wakati watumishi wanasoma lengo ni kupanda cheo na mishahara.

Pia amesema wauguzi wanataka usalama kazini, wapo wauguzi wameshambuliwa wakiwa kazini, hivyo elimu itolewe kwa jamii kuhusu kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazotokea.

Ameongeza kuwa ni kweli kuna changamoto zinaweza kutokea sehemu za kazi, kati ya wauguzi na jamii lakini zinapotokea ni vizuri zitatuliwe kwa njia zinazostahili na siyo wauguzi kuathirika zaidi.

Katibu Mkuu wa TANNA, Samwel Mwangoka akisoma risala, amesema bado kuna changamoto zinawakwaza kwenye utendaji kazi wao, ikiwemo kutopandishwa madaraja kazini.

Pia changamoto nyingine ni ajira za wauguzi hasa maofisa wauguzi wamekuwa wakiajiriwa wachache, hivyo kuiomba Serikali kutoa vibali kwaajili ya kuajiri kada hiyo.

Naibu Waziri Wizara ya afya, Dk Godwin Mollel amesema katika watumishi wa idara ya afya asilimia 60 ni wauguzi.

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian kwa upande wake,  amewapongeza wauguzi kwa utendaji kazi wao, hasa kwa kupambana kwenye masuala ya chanjo kwenye maeneo mbalimbali nchini.