Mwanafunzi chuo cha KICHAS adaiwa kujiua kisa madeni

Erick Sawe(21) mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo cha KICHAS enzi za uhai wake
Muktasari:
- Mwanafunzi huyo wa mwaka wa pili katika idara ya mazoezi kwa tiba, anadaiwa kujiua Mei 13, 2025 kwa kutumia waya aliofunga kwenye dirisha la choo alichokuwa akitumia.
Moshi. Mwanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kilimanjaro (KICHAS), Erick Sawe(21) anadaiwa kujiua kwa kujinyonga chooni katika nyumba aliyokuwa amepanga eneo la Kiriwa chini, Kata ya Rau Manispaa ya Moshi, huku chanzo cha kifo hicho kikidaiwa ni wingi wa madeni.
Mwanafunzi huyo wa mwaka wa pili katika idara ya fiziotherapia (mazoezi kwa tiba) na mwenyeji wa Machame, Wilaya ya Hai anadaiwa kujiua Mei 13, 2025 kwa kutumia waya aliofunga kwenye dirisha la choo alichokuwa akitumia.
Inadaiwa kuwa, siku ya tukio, baadhi ya wanafunzi waliokuwa wanamdai walienda nyumbani kwake anakoishi kufuata fedha zao na walipofika waligonga mlango bila mafanikio na walipochungulia dirishani waliona mwili ukiwa unaning'inia chooni.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amezungumzia tukio hilo akidai kuwa chanzo ni msongo wa mawazo.
"Tukio limetokea Mei 13, 2025 saa nane mchana, kijana huyu ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo cha KICHAS, alijinyongea kwenye choo ambacho kipo chumbani kwake kwa kufunga waya dirishani eneo la Kiriwa chini, kata ya Rau," amesema DC Mnzava
DC Mnzava amedai chanzo cha tukio hilo ni kwamba mwanafunzi huyo anadaiwa kuwa na madeni mengi yaliyomfanya kuwa na msongo wa mawazo.
"Chanzo cha kufanya hivyo ni kwamba alikuwa na madeni lakini ulevi na mambo haya mawili yamesababisha kuwa na msongo wa mawazo," amedai DC Mnzava
Aidha, amesema mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya KCMC kwa uchunguzi wa kidaktari.
Pamoja na mambo mengine, mkuu huyo wa wilaya ametoa rai kwa wanafunzi kuhakikisha wawapo chuoni wanafuata mambo ya msingi yaliyowapeleka chuoni na sio vinginevyo.
Pia amewataka wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya wanafunzi wawapo chuoni ili kujua maendeleo yao kitaaluma.
Katibu wa Afya wa chuo cha KICHAS, Anna Mmbando amesema ni kweli mwanafunzi huyo amefariki kwa kujinyonga.