Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yasaini mkopo Sh1.04 trilioni, kujenga miundombinu Pemba


Muktasari:

  • Serikali ya Zanzibar na Uingereza zimesaini makubaliano ya mkopo wa bei nafuu wa Euro 400 milioni sawa na Sh1.04 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba na zaidi ya kilometa 103 Unguja na Pemba.

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Uingereza zimesaini makubaliano ya mkopo wa bei nafuu wa Euro 400 milioni sawa na Sh1.04 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba na zaidi ya kilometa 103 Unguja na Pemba.

Fedha hizo ambazo ni mkopo nafuu kutoka Uingereza, unapitia benki za Deutsche na Citibank kiasi ambacho kinatajwa kuwa kikubwa kuwahi kupokewa kwa Serikali hiyo tangu Mapinduzi.

Hafla ya kutia saini hiyo imefanyika leo Juni 20, 2023 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Zanzibar kati ya Balozi wa Uingereza nchini Tanzania David Concar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji wa saini hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said amesema ni tukio kubwa la kihistoria kwa Zanzibar kugharamia miundombinu muhimu ya kimkakati kwa kiasi kikubwa cha fedha za namna hiyo.

“Hii itanufaisha uchumi wetu watu kutoka maeneo mbalimbali watakuja na kukuza utalii wetu,” amesema

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Saada Mkuya amesema kwa mara ya kwanza Zanzibar kupata kiasi hicho kikubwa cha fedha za mkopo kwa mkupuo.

“Hii ni historia tunakwenda kuifungua Zanzibar katika miundombinu ya kuchumi kwa kujenga barabara za hapa Unguja na Uwanja wa ndege wa Pemba ambao utakuwa wa kimataifa,” alisema Dk Saada.

Pia, katika hafla hiyo alikuwepo Bw Jamal Kassim, ambaye alianza kutafuta mkopo huo akiwa waziri wa fedha, akisema mpango wa awali ungechukua zaidi ya miaka minne lakini kwa AKEF, ilichukua mikutano michache.

"Kulikuwa shida nyingi mwanzoni lakini hatukukata tamaa na hatimaye kwa makubaliano ya ufadhili huu sasa tunaweza kuangazia manufaa ambayo mradi huu unaweza kuletea kwa taifa letu," alisema Bw Kassim.

Aliongeza: Tangu nchi yetu hii iwepo, hatujawahi kupata fedha nyingi namn hii kutoka popote, maana kwa viwango vya leo inaweza kuwa zaidi ya Sh1 trilioni.

Kwa maoni yake, mradi huo unatazamiwa kuugeuza kiwanja cha ndege cha Pemba kuwa kiwanja cha kimataifa kwa kupanua njia yake ya kurukia ndege hadi kilomita 2.5 na kuongeza jengo jipya la abiria.

Muonekano wa Pemba Airport utakavyokuwa baada ya ujenzi kukamilika mwaka 2026

Huu ni mpango wa kwanza wa ufadhili wa fedha kiasi hicho kati ya UKEF na Tanzania.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasilianio na Uchukuzi, Dk Khalid Salum alisema safari hiyo imeanza muda mrefu tangu awamu zilizotangulia na mawaziri tofauti wa Awamu ya Nane hivyo kufikia hatua hiyo ni jambo la kupongeza.

“Zaidi ya kilomita 800 zinakwenda kujengwa hapa Unguja na Pemba hii haijawahi kutokea mara nyingi zinajengwa barabara zenye urefu wa kilometa 200, lakini mara hii tunajenga kilometa hizo tena kwa wakati mmoja,” alisema Dk Khalid.

Naye Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar alisema katika utekeleji wa mradi huo utafungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa taifa na wananchi wa Zanzibar.

Alisema Serikali ya Uingereza itaendelea kushirikiana na Serikali za Tanzania na Zanzibar kuendelea kuitekeleza miradi mingine mikubwa ya kimkakati.

Miradi hiyo ya barabara na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Pemba, inatekelezwa na Kampuni ya Propav Infrastructure (Propav) na wakandarasi wa Tanzania, Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Limited (Mecco), jambo ambalo limetajwa kuwa ni mapinduzi makubwa visiwani humo huku yakiendelea kuvutia wawekezaji kutoka nje.

"Miradi hii inazungumzia nini tunasimamia kama kampuni," mkurugenzi wa Propav Leandro Motta alisema.

“Tunajitahidi kujenga miundombinu ambayo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi barani Afrika, na tunaamini kuwa katika mikataba hii, tuna mambo mengi yatakayochangia ukuaji wa Tanzania, si kwa sasa tu bali hata katika siku zijazo”, aliongeza. .

Kauli yake hiyo iliungwa mkono na Nasser Sheikh, mkurugenzi wa maendeleo ya biashara wa Mecco ambaye alionyesha kujivunia kuchangia maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.

Ujenzi wa uwanja wa ndege utafanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ikihusisha usanifu upya wa jengo la abiria na kupanua njia ya kurukia ndege.

Kiwanja cha ndege cha Pemba kwa sasa kinahudumia abiria 45,000 tu kwa mwaka, ambapo idadi ya watalii wanaotembelea kisiwa hicho inazidi 110,000 kwa mwaka, na baada ya kukamilika kwake kitakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 750,000 kwa mwaka.

Kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho kilijengwa mwanzo mwaka 1962, kwa sasa kina urefu wa mita 500 na upana wa mita 15, ambacho kinaweza kubeba ndege nyepesi tu, lakini usanifu huo mpya utaruhusu ndege kubwa za kimataifa kuruka na kutua moja kwa moja ndani ya kisiwa hicho.