Zaidi ya nusu ya wanawake Kinondoni wanajichubua

Muktasari:

  • Utafiti huo na tafiti nyingine zitawasilishwa kwenye kongamano la kisayansi litakalofanyika Juni 27-28, mwaka huu.

Dar es Salaam. Imebainika kuwa zaidi ya nusu wa wanawake  waliopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam wanatumia vipodozi vya kujichubua.

Hali hiyo imebainika kupitia tafiti iliyofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) ambayo imeonyesha asilimia 54.5 ya wanawake hao wanatumia vipodozi hivyo, ili wawe weupe.

Utafiti huo umebaini wengi wao ni wale wanaofanya kazi mapokezi. Tafiti hiyo imefanyika ili kubaini iwapo vipodozi vinavyotumika ni salama katika afya ya ngozi na haliveti madhara kwa mtumiaji.

Akidokeza juu ya tafiti hiyo na nyingine nyingi zilizofanywa na chuo hicho ambazo zitawasilishwa katika kongamano la kisayansi litakalofanyika Juni 27 na 28, mwaka huu.

Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema pia wamebaini asilimia 15 ya watu wanaioshi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wana kiwango cha juu cha sukari.

"Unywaji wa pombe na shinikizo la juu la damu linachangia wagonjwa hawa kuwa na kiwango cha juu cha sukari mwilini," amesema Profesa Kamuhabwa, alipozungumza na waandishi wa habari leo Juni 24, 2024  kuhusu kongamano hilo.

Aidha, amesema katika kongamano hilo litakalo wakutanisha wadau zaidi ya 400 wa ndani na nje ya nchi, linatarajiwa kuwasilisha tafiti za kisayansi 80 kwa njia ya maongezi na 107 kwa njia ya mabango ambazo zitawasilishwa katika mada ndogo nane. 

Akizitaja tafiti hizo amesema ya kwanza ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza, afya ya akili, upasuaji na lishe.

"Pia tafiti nyingine zitahusu magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea dhidi ya dawa, afya ya mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana rika.

"Nyingine ni utunzaji na afya ya kinywa, jicho, sikio, pua na koo, viamuzi vya kijamii kwa afya (afya moja), utafiti wa mifumo ya afya tafiti zinafanyika jinsi ya kuboresha mfumo, tiba mbadala na asili, uvumbuzi wa dawa na maendeleo ya chanjo na masuala mtambuka, maadili na taaluma, akili mnemba, teknolojia na afya ya kazini,” amesema.

Profesa Kamuhabwa amesema kutokana na ongezeko la maradhi yasiyoambukiza na yale ya milipuko ni jukumu lao kama chuo kutafuta majibu juu ya magonjwa na matatizo ya kiafya yanayowakabili Watanzania.

Vilevile, wadau watabadilishana ujuzi  katika kongamano hilo  litakalofanyika katika Kituo cha Afrika Mashariki cha umahiri wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu (Muhas) kampasi ya Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Amesema wanafanya tafiti kulingana na mwenendo wa magonjwa duniani na hapa nchini na katika kongamano hilo ambalo ni la 12 kufanyika ni sehemu ya kutafuta majibu ya maradhi hayo.

Profesa Kamuhabwa amesema watashirikishana, kuelezana, kujifunza na kubadilishana ujuzi unaotokana na matokeo ya tafiti kati ya watafiti mbaalimbali, watoa huduma wa afya, watekelezaji wa mikakati na sera na wadau wengine wote ndani na nje ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kushirikisha jamii kwa ujumla.

Aidha, amesema kongamano la mwaka huu ni la kumuenzi mkuu wa chuo wa kwanza na Rais wa pili wa Tanzania, hayati Ali Hassan Mwinyi aliyefariki dunia, Februari, 29 2024.

Mkurugenzi wa tafiti, machapisho na ubunifu Muhas, Dk Nahya Masoud amesema pia kongamano hilo ni muhimu kwa kuwa linawagusa Watanzania, hivyo anawaomba washiriki.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Sayansi kama hadithi ya maisha: Nguvu ya tafiti, bunifu na ushirikiano kwenye kuimarisha mifumo thabiti ya afya”.