Kongani ya viwanda Kibaha kuajiri Watanzania 600,000

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akipewa maelezo alipotembelea kiwanda vipodozi kilichopo mtaa wa viwanda wa Sino-Tan Kibaha, mkoani Pwani.

Muktasari:

  • Mradi wa Mtaa wa Viwanda unaojengwa Kibaha mkoani Pwani unatajwa kuwa na faida kubwa nchini na mbali ya kutoa ajira, Tanzania itazalisha na kuuza bidhaa ndani na nje ya nchi.

Pwani. Wakati kongani ya viwanda inayojengwa Kibaha mkoani Pwani ikifikia hatua ya mwisho ya ujenzi wa awamu ya kwanza, inaelezwa  ikikamilika itatoa ajira 600,000 kwa Watanzania.

Kongani hiyo (mtaa wa viwanda) inayojengwa na kampuni ya Sino-Tan kutoka nchini China ambayo itakuwa na viwanda vikubwa, vya kati na vidogo itatoa ajira hizo huku ikiongeza thamani ya bidhaa za Tanzania katika ushindani wa kibiashara.

Akizungumza leo Februari 20, 2024 baada ya kutembelea eneo la mradi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala, Katiba na Sheria, Joseph Mhagama ametaja  faida nyingine za uwekezaji huo kuwa ni bidhaa mbalimbali zitaanza kuzalishwa na kuuzwa nje ya nchi.

Asema mradi huo unaojengwa karibu na bandari kavu ya Kwala, kati ya ajira hizo, 100,000 zitakuwa za moja kwa moja na nyingine 500,000 zitakuwa si za moja kwa moja.

“Kutakuwa na viwanda 200 vya kuanzia na mradi ukikamilika kutakuwa na jumla ya viwanda 500 ambavyo vitakuwa vinazalisha bidhaa mbalimbali, kiujumla uwekezaji huu ni fursa kwa Watanzania,” amesema Mhagama.

Pia, amesema changamoto zinazoukabili mradi huo ikiwemo barabara, kodi na vivutio vya uwekezaji watazifikisha serikalini, ili zipatiwe ufumbuzi na kuweka mazingira mazuri ya kukamilisha mradi huo kwa wakati.

“Bidhaa nyingi zitakazotumika na kuuzwa nje ya Tanzania zitatoka hapahapa nchini. Hii ni hatua kubwa, pia tunataka kuwa na soko pana kwa wakulima wetu kupitia viwanda hivi,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameipongeza kampuni iliyowekeza hapo kwa uaminifu, huku akisema hayo yote yanakuja baada ya kuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.

“Hadi sasa wameshatekeleza mradi huu kama tulivyokubaliana, nitumie fursa hii kuwapongeza kwa mradi wa mtaa wa viwanda,” amesema Profesa Mkumbo.

Awali likisomwa wasilisho la mradi huo,  msimamizi mkuu wa mradi, Chen Xiong amesema mradi huo utakamilika mwaka 2027 na itakuwa eneo maalumu la viwanda.

"Hadi sasa viwanda vya vipodozi na nguo vimeshaanza na hadi kufikia Machi hadi Aprili vitaanza viwanda vingine," amebainisha.