RC Kunege: Wekezeni kwenye kongani za viwanda

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka wawekezaji watarajiwa wa viwanda mkoani humo, kuhakikisha wanatumia fursa ya maeneo yaliyotengwa rasmi kwa ajili hiyo (industrial park/industrial zone), kama njia ya kuepuka utapeli kwa kununua maeneo yenye migogoro.

Kibaha. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka wawekezaji watarajiwa wa viwanda mkoani humo, kuhakikisha wanatumia fursa ya maeneo yaliyotengwa rasmi kwa ajili hiyo (industrial park/industrial zone), kama njia ya kuepuka utapeli kwa kununua maeneo yenye migogoro.

 Tahadhari hiyo ameitoa leo Oktoba 7, 2023; alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma cha Kinglion Steel kilichopo Zegereni Kibaha, ambacho mpaka kukamilika, kitakagharimu Sh163 bilioni.

“Pia msinunue maeneo tofauti tofauti kwa sababu haitakua rahisi kwa Serikali kutoa huduma zote muhimu kwa mwekezaji mmoja moja...mfano barabara za lami, umeme na maji ya kutosha. Huduma kama hizi ni rahisi kuzipata kwenye kongani za viwanda kwa sababu zinaenda kuhudumia wengi,” amesa RC huyo na kuongeza;

"...natoa maelekezo kwa halmashauri, lazima sasa eneo tulilosema ni zone ya viwanda lipimwe ili hawa Tarura, Tanesco, Tpdc, Dawasa na Tanroad, waweke katika mipango yao, ni vigumu sana leo useme unahitaji barabara hapa, haikua katika mipango."

Awali Meneja wa Kiwanda hicho cha chuma, Arnold  Lyimo, amesema ujenzi umeanza Machi 2022 na kwamba watakamilisha kufunga mitambo April 2024, huku wakitegemea kuanza uzalishajimiezi miwili baadaye.

Kwa mujibu wa Lyimo, kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha tani 300,000 za chuma kwa mwaka na kwamba ajira za moja kwa moja zinatarajiwa kuwa 400, huku zile zisizo rasmi kufikia 5,000.

Kwa upande wake Meneja wa Tarura mkoani humo, Leopold Runji amesema wanatarajia kwa kuanza kujenga kwa kiwango cha changarawe kipande cha kilometa mbili ambacho kitagharimu takribani Sh220 milioni huku wakiwa na mpango wa kuisanifu na baadaye kuiombea bajeti katika mwaka ujao wa fedha.

Kwa sasa Mkoa wa Pwani umeainisha maeneo 23 ambayo ni maalumu kwa ajili ya kongani za viwanda vikubwa.

Aidha Mkoa huo kutokana na kasi ya uwekezaji kwa sasa una zaidi ya viwanda 1,470 ambapo kati yake 97  ni vikubwa na vingine ni vya kati na vidogo.