Marufuku ya kucha, kope bandia yawaibua wafanyabiashara, wahofia ajira zao

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Kufuatia kusambaa kwa kipande cha video mitandaoni kinachomuonyesha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Athuman Ngenya akizungumzia kupigwa marufuku kwa kucha bandia na kope, wafanyabiashara wa bidhaa hizo wapaza sauti

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa kubandika kucha na kope wamesema, endapo bidhaa hizo zitapigwa  marufuku kundi kubwa la vijana wasio na ajira rasmi litarudi  mitaani, jambo linaloweza kuzua tabia hatarishi.

Wametoa kauli hiyo baada ya kuwapo kwa kipande cha video inayozunguka mitandaoni ikimuonyesha Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk Athuman Ngenya kuwataka wafanyabiashara wa kope kucha na rangi kuondoa sokoni bidhaa hizo, kwani zimekatazwa.

“Kope kucha rangi vimekatazwa, si hivyo tu kuna vitu vingi vimekatazwa na nichukue nafasi hii kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara wa bidhaa hizi kuhakikisha wanaviondoa sokoni vinginevyo tukifika tutawachukulia hatua za kinidhamu ambazo zitasababisha  kuharibu biashara na utu wao kwa ujumla,” amesema Dk Ngenya.

Licha ya kutobainisha hatua zitaanza kuchukuliwa lini, lakini aliwataka wafanyabiashara wa bidhaa hizo kubadilisha kile wanachokifanya na wafanye biashara nyingine zisizokuwa na matatizo.

 Akilizungumzia suala hilo kwenye mahojiano na Mwananchi Digital kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wamiliki wa ofisi za kupaka rangi amesema maamuzi mengine hufanyika bila kujua yataathiri vipi watu.

Akiwa amewekeza zaidi ya Sh20 milioni katika biashara hiyo ametaka uchambuzi wa kina kufanyika kabla ya uamuzi kuchukuliwa.

“Biashara ya kucha iko dunia nzima, sisi tu ndiyo tumeona kuna tatizo, unajua ni kundi gani linaenda kuathirika, vijana wasiokuwa na elimu, hii ndiyo sehemu ambayo wamewekeza, ukipiga marufuku unawaweka mtaani wawe vibaka,” amesema na kuhoji.

Akiwa na ofisi mbili ndani ya jiji la Dar es Salaam, vijana nane wameajiriwa katika ofisi hizo wakiwa na familia zinazowategemea huku akieleza kuwa uamuzi huo utawaathiri wengi walio nyuma yao.

“Mimi tayari nina mtaji, naweza kusema naacha biashara hii nafanya mambo mengine, vipi kuhusu hawa walio nyuma yangu, tusitumie mihemko kufanya vitu,” amesema.

 Licha ya watu kuidharau biashara hiyo, ameeleza kuwa kiasi cha fedha anachokipata kwa mwezi kinazidi watu wengi walioajiriwa maofisini,  jambo linalomuwezesha  kugusa maisha ya watu wengi.

“Lakini biashara hii, ndiyo imenifanya mimi kufika China kufuata kucha na rangi zinakotengenezwa, badala ya kupiga marufuku waseme nini kiboreshwe kwa faida ya watu walio nyuma yake,” amesema.

Maneno yake yanaungwa mkono na Twaha Kitambaa aliyeanza kazi hiyo mwaka 2007 ambaye amesema  kuwa maisha yake yote yapo katika ubandikaji kucha na upakaji rangi, hivyo kupigwa marufuku ni sawa na kumpotezea uelekeo wa maisha.

“Miaka hiyo mtaji wa Sh20,000 sasa hivi naongelea ofisi yenye huduma mbalimbali za urembo uje upige marufuku? Huduma nyingine zinaweza kuendelea lakini kitu kinachonitambulisha mimi ni kucha, wanataka maisha yetu yawe vipi,” amehoji Twaha.

Amesema ubandikaji wa kucha ndiyo kitu kinachowaingizia fedha zaidi katika biashara yake na bei zake hutofautiana kulingana na aina ya kucha mtu anayohitaji.

‘Sasa ukifunga biashara hii iliyokuwa inaweza kukupa wateja hadi 10 kwa siku unataka nifanye nini,” amesema Twaha huku akiwahurumia aliowaajiri.

Mpaka rangi mwingine ambaye pia anabandika kope, Victor Aityeko amesema badala ya kupiga marufuku ni vyema wapewe  elimu ya vitu vya kuzingatia ili kuepukana na athari na biashara ziendelee.

“Kupiga marufuku haituathiri sisi tu bali na vijana walio nyuma yetu tuliowaajiri, mimi nimeajiri vijana wanne sehemu tofauti, ukipiga marufuku maana yake ofisi inafungwa wanarudi mitaani,” amesema Aityeko.

Amesema hiyo itaathiri pia upatikanaji wa mahitaji muhimu kwa watu waliokuwa wanawategemea, jambo ambalo litaongeza utegemezi.

Katika hatua nyingine, Dk Bernadetha Shilio, Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma ya Macho kutoka Wizara ya Afya amesema matumizi ya vipodozi katika eneo linalozunguka macho ni hatari.

“Hata wanja tunakataza hasa zile zinazopakwa karibu na macho, zote zinaingia machoni zinaleta uvimbe, kope zinazobandikwa na kimiminika sijui cha aina gani inapopata nafasi ya kuingia ndani ya jicho inaharibu,”amesema.

Amesema inaharibu pale inapobandikwa kunakuwa na uvimbe na miwasho kama ambavyo wanaovaa wigi kwa muda nywele zinavyopungua uzito kwa kukosa hewa.

“Kwenye ngozi kuna vitundu vya kupumulia, sasa inapozibwa inakuwa ni rahisi kuleta muwasho, kutengeneza uvimbe na kuchangia kuharibu kope ambazo kazi yake ni kuzuia takataka kuingia ndani ya jicho,” amesema Dk Shilio.