MADHARA: Kucha za bandia zagharimu maisha ya bibi harusi

Mikono iliyobandikwa kucha za bandia.

Muktasari:

  • Aliibandika kwa ajili ya ndoa yake, lakini alipoibandua baada ya harusi tatizo likaanza.

“Sijui walitumia gundi ya aina gani kumbandikia kucha mwanangu, mpaka sasa sielewi, mtoto mwenyewe ndiyo huyo huyo mmoja wa kike niliyekuwa nikimtegemea na ndiyo kwanza ndoa yake bado change kabisa hata mwezi mmoja haina, huu ni mtihani mkubwa kwangu na kwa mumewe ambaye wamefunga naye ndoa wiki tatu zilizopita, inauma sana lakini tunamwachia Mungu.”

Ni maneno ya mama mzazi wa Sophia Komba aliyefariki dunia hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baada ya kupata kidonda kwenye kidole chake cha mkono wa kushoto alipokuwa akibandua kucha za bandia alizobandikwa siku ya harusi yake na kusababisha apatwe na tetenasi.

Sophia hadi kifo kinamkuta alikuwa na umri wa miaka 28, Oktoba 15 alifunga ndoa na Richard Mmary katika harusi ya aina yake iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Wakisimulia namna walivyomuuguza Sophia kwa takriban wiki moja na nusu, mume wa marehemu anasema wiki moja baada ya sherehe ya harusi yao, Sophia aliamua kwenda tena salon kwa ajili ya kutengeneza nywele na kutoa kucha alizobandikwa siku ya harusi yao.

“Ilikuwa siku ya Jumamosi jioni, Sophia aliniaga anaenda saluni, alirudi baada ya saa mbili kupita lakini alikuwa akilalamika kuwa kidole kinamuuma sana, nikamuuliza amefanya nini akanijibu kuwa alikuwa anabandua kucha, lakini bahati mbaya kucha moja inaonekana ilibandikwa vibaya walipokuwa wanaibandua ilibanduka na ngozi ya pembeni ya kidole na ikamuachia kidonda.

“Sikujali sana nikajua ni kidonda cha kawaida tu, nikaenda kwenye duka la dawa nikamnunulia spiriti nikamsafisha lile eneo, lakini kilichonishangaza alikuwa akilalamikia maumivu makali,” anasema.

Mama yake Sophia, Victoria Haule anasema kuwa anaamini kuwa kifo cha mwanaye kimetokana na kucha bandia ambayo ilimsababishia apatwe na tetenasi.

“Tulipoona maumivu yanamzidia, tulimpeleka Hospitali ya Sinza, daktari alipomfanyia vipimo alitutaka tumpeleke Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu zaidi, kwa kuwa alibaini kuwa Sophia ana tetenasi iliyosababishwa na kile kidonda. Binafsi niliamini kucha ile ndiyo tatizo, kwa kuwa ilifikia hatua mkono mzima ukawa umevimba na kubadirika rangi na kuwa mweusi sana kama damu imevilia,” anasimulia mama yake Sophia.

Kwa maelezo ya ndugu hao wa marehemu, Sophia alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu na kwa mujibu wa daktari kifo chake kilisababishwa na tetenasi.

Mabibi harusi wengi hivi sasa na hata wanawake kwa wasichana wanapendelea sana kubandika kucha bandia wakilenga kuboresha mwonekano wa vidole vyao. Wengi hupenda kuwa na kucha ndefu ambazo huzipaka rangi na hivyo kuvutia pindi mtu azionapo.

Licha ya wao kuona kuwa kwa kufanya hivyo hupendeza, daktari mmoja wa magonjwa ya ngozi, anasema urembo wa kubandika kucha una athari zake kutokana na kutumika kwa gundi ambayo hunata hata kwenye ngozi.

Dk Patrick Kashaija wa Hospitali ya St. Benedict ya jijini Dar es Salaam, anasema amewahi kukutana na kesi za aina kama ya marehemu Sophia nyingi ambazo husababishwa na kubandikwa kucha za bandia.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa hajajua ni kemikali ya aina gani inayotumika kubandika kucha hizo alizodai kuwa huenda zina madhara makubwa kiafya. Anasema wanawake wanaopenda kuwa na kucha ndefu, ni vyema wakazikuza za kwao za asili badala ya kujitafutia matatizo yanayoweza kusababishwa afya zao kuathirika na hata kifo.

 “Nasikia kuna wengine wanatumia mpaka gundi aina ya super glue, sasa hii ni hatari, lazima watu watathmini kwa makini madhara ya kitu anachotaka kukifanya kabla ya kutoa uamuzi wa kuanza kufanya,” anasema Dk Kashaija.

Wamiliki na wafanyakazi wa saluni

Wengi wao walipozungumzia suala hili walikiri kuongezeka kwa wateja wanaofika kwenye saluni zao kusafishwa kucha na kubandikwa za bandia. “Hii ni biashara nzuri hivi sasa, si unaona hata vijana wanavyozidi kuongezeka huko mitaani wakiifanya kila kukicha, kwa kweli inalipa,” anasema Asha Abdalah mmoja wa wamiliki wa saluni katika eneo la Sinza, Dar es Salaam.

Asha anasema miongoni mwa kazi inayoifanya saluni yake ifurike wateja siku za mwisho wa wiki ni pamoja na kupamba maharusi ambao wengi hubandika kucha za bandia na kope.

Hata hivyo anasema kutokana na biashara hiyo kuvamiwa na watu wasio na utaalamu, matokeo yake wamekuwa wakiwaathiri wateja wao.

“Kuna tatizo kubwa kwa sasa, watu wengi hawana utaalamu wa kuzibandika hizi kucha na matokeo yake wale wanaobandikwa hujikuta wakidhurika vibaya na mbaya zaidi wengine hutumia gundi feki na wapo ambao hutumia hata gundi hatari ya super glue. Kama unavyoijua gundi hiyo ambayo ukiweka kwenye kitu kubanduka kwake ni mpaka kile kitu kikatwe, sembuse kwenye ngozi, ni hatari sana,” anasema Asha.

Alipoulizwa ni kwa nini wanafanya hivyo, anasema kutokana na uchunguzi alioufanya, asilimia kubwa ya watoa huduma hiyo wanataka kupata faida kubwa, hivyo huamua kutumia njia za mkato ili kufikia malengo yao.

“Hizi kucha hubandikwa kwa kutumia gundi yake maalumu ambayo hununuliwa pia. Bei yake ni tofauti na bei ya gundi nyingine na ni ghali, hivyo mtu anaona ni bora achukue gundi yoyote ile ya bei ndogo anaitumia bila kujua madhara yanayoweza kumtokea yule anayebandikwa kucha hizo.

Neema Mwasa mhudumu katika salon moja kubwa iliyoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam, anasema alishanusurika kupelekwa polisi  baada ya kumbandika kucha mteja wake ambaye alikuwa na mzio wa ngozi.

“Siku hiyo ilikuwa pata shika, asingekuwa mama yake mdogo aliyekuwa anakaa naye kuingilia kati sijui ingekuwaje, maana yeye ndiye alituambia kuwa binti yake ana aleji (mzio) wa ngozi na hawajui unasababishwa na nini, huenda hata ile gundi ilipogusa ngozi yake ya kucha ilisababisha avimbe vidole,” alisimulia Neema.

Anasema umakini unahitajika katika kuifanya kazi hiyo huku akisisitiza kutumika kwa vifaa vinavyoruhusiwa, sambamba na wataalamu waliosomea kazi ya urembo.

Neema anasema ukubwa ama umaarufu wa salon siyo tiketi ya kuwa ndiyo inahudumia wateja kwa kiwango cha ubora.

Binti huyo anasema zipo saluni kubwa na maarufu lakini wahudumu wake hawako makini na wanafanya kazi chini ya kiwango. “Ninawaomba sana wanawake wanaopenda urembo, wasiangalie umaarufu bali waangalie ubora wa huduma itolewayo na salon husika. Unaweza kukuta saluni ni ndogo na haina umaarufu, lakini kumbe wahudumu wake ni makini na walioenda shule.

Wasichana wengi sasa hivi wanasoma Veta na wanafuata maadili ya kazi yao.

Wanamuhudumia mteja kwa kufuata kile alichofundishwa darasani na siyo kwa ajili ya kutoa huduma ili mradi tu apate fedha,” anasema Neema.

Wapaka rangi kucha wazungumza

Kijana Hussein Mhina anayefanya kazi ya kupaka rangi na kubandika kucha bandia kwa kupita mitaani, anasema kucha za kubandika zina madhara makubwa ambayo wanawake wengi bado hawajayagundua. Anasema masharti ya kucha hizo, yanataka ukae nazo kwa takribani wiki mbili tu tangu uzibandike kisha uzitoe. “Lakini wengi wao wakizibandika hukaa nazo hata mwezi mzima, ile gundi tunayotumia kuzibandikia inamadhara kwenye kucha ya asili na hata kwenye ngozi pia.

Ndiyo maana utaona wengi wakikaa nazo kwa muda mrefu akija kuzibandua anakuta kucha zake zimebadilika na kuwa nyeusi sana, hayo ni madhara,” anasema Mhina.

Anasema weusi ule huathiri kucha ya asili na kila inapoota akitaka kuifuga ili irefuke hukatika katika. Hata hivyo alishindwa kufafanua kwanini inatokea hivyo, kwa madai kuwa hata yeye hajui.