Wizi wa miti waathiri mapambano mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:
- Wadau wa mazingira wameelezea masikitiko yao kufuatia wizi wa miti inayopandwa kwa ajili ya kuhifadhi mazingira, wakisema vitendo hivyo vinavuruga juhudi za kupambana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kondoa. Ofisa Mradi wa Maendeleo ya Jamii, Rajabu Rajabu, amebainisha kuwa Serikali kupitia mamlaka husika imekuwa na mchango katika jitihada za kuhifadhi mazingira, licha ya changamoto za wizi wa miti iliyopandwa na uharibifu unaosababishwa na mifugo.
Kwa mujibu wa Rajabu, baadhi ya wanajamii huiba miti inayopandwa, hasa miti ya matunda, jambo ambalo husababisha maeneo hayo kubaki bila miti na kuendeleza uharibifu wa mazingira.
Rajabu amesema hayo leo Ijumaa, Juni 6, 2025, kwamba Serikali kupitia mamlaka husika imekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia utekelezaji wa majukumu ya utunzaji wa mazingira.
Amebainisha kuwa licha ya mafanikio ya upandaji miti yanayofanywa na Serikali, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazorudisha nyuma jitihada zao, ikiwemo uharibifu wa miti inayopandwa kutokana na mifugo kuharibu mimea hiyo.
“Tunafurahia kuona viongozi wa Serikali wanatupokea kwa moyo mkunjufu na kushirikiana nasi katika jitihada zetu za kuhifadhi mazingira, hasa katika upandaji wa miti,” amesema Rajabu.
Hata hivyo, Rajabu amebainisha kuwa licha ya mafanikio hayo, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazorudisha nyuma jitihada zao, ikiwemo uharibifu wa miti inayopandwa kutokana na mifugo kuharibu mimea hiyo.
Ofisa Misitu wa Wilaya ya Kondoa, Clement Kabeni ameahidi kushirikiana na wadau wote katika jitihada za kuhifadhi na kutunza mazingira.
Pia, amewahimiza walimu kuhakikisha wanawasimamia wanafunzi kwa karibu katika utunzaji wa miti, ili miti hiyo iweze kutoa matunda yaliyokusudiwa katika siku zijazo.
“Ninatoa wito kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kuenzi na kutunza miti hii, na pia walimu waendelee kuwasimamia wanafunzi ili kuhakikisha jitihada hizi zinafaida kwa mazingira yetu,” amesema Kabeni.
Imeandikwa na Elidaima Mangela