Utunzaji ovyo, mifugo vyateketeza miti zaidi ya 10,000

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma wakifanya usafi katika bustani ya miti iliyoanzishwa shuleni hapo kupitia kampeni maalum ya balozi wa mazingira nchini. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Kati ya miti zaidi ya 45,000 iliyopandwa, takriban miti 10,000 imekufa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uharibifu unaosababishwa na mifugo na ukosefu wa utunzaji unaotolewa na taasisi husika.
Musoma. Zaidi ya miti 10,000 iliyopandwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari mkoani Mara imekufa kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuliwa na mifugo pamoja na ukosefu wa matunzo kutoka kwa taasisi husika.
Miti hiyo ni sehemu ya jumla ya miti 45,000 iliyopandwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita kupitia kampeni maalumu ya mazingira, iliyoendeshwa na Balozi wa Mazingira nchini, Jairos Sinene.
Kati ya miti hiyo, zaidi ya miti 35,000 imekua, huku takriban miti 10,000 ikishindwa kustawi kutokana na changamoto hizo. Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne, Juni 3, 2025 mjini Musoma na Balozi Sinene alipofanya ziara kukagua maendeleo ya miti iliyopandwa kupitia kampeni hiyo katika shule zilizopo Manispaa ya Musoma.

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma wakifanya usafi katika bustani ya miti iliyoanzishwa shuleni hapo kupitia kampeni maalum ya balozi wa mazingira nchini. Picha na Beldina Nyakeke
"Hii miti 45,000 ni tofauti na ile iliyoelekezwa na Serikali ambapo kila halmashauri inatakiwa kupanda miti 1.5 milioni kila mwaka. Hii ni kampeni maalumu ya kuhamasisha taasisi za umma kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira ili kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia kutokana na uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji wa miti," amesema Sinene.
Amesema ufuatiliaji na usimamizi madhubuti vimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kampeni hiyo, ambapo zaidi ya asilimia 95 ya miti iliyopandwa imefanikiwa kukua.
Balozi Sinene amewasihi wadau wengine kuhakikisha hatua ya ufuatiliaji inaendelezwa mara baada ya upandaji miti ili kuhakikisha uendelevu wa juhudi hizo.
Kwa upande wake, Rhobi Samuel, ,jumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Taifa, amesema utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwanajamii.
Rhobi ametoa wito kwa kila mmoja, kwa nafasi yake, kuhakikisha anapanda na kutunza miti katika maeneo yake ili kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
"Tusisubiri kampeni za balozi wa mazingira ndipo tupande miti. Kila mtu, kwa nafasi yake na katika eneo lake anapaswa kupanda miti kwa wingi kadri awezavyo. Hakika hili likifanyika tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, ambayo athari zake tayari tumeanza kuziona," amesema.

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma wakifanya usafi katika bustani ya miti iliyoanzishwa shuleni hapo kupitia kampeni maalum ya balozi wa mazingira nchini. Picha na Beldina Nyakeke
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034, na kwamba dhamira hiyo inapaswa kwenda sambamba na suala zima la uboreshaji wa mazingira, ikiwemo upandaji wa miti.
"Wakati tunajipanga kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, lazima tuhakikishe mazingira yanakuwa salama. Tunapanda miti na kuitunza, kwani sote tunajua faida ya miti kwa ustawi wa mwanadamu. Hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kujua ana wajibu mkubwa kulifanikisha hili," amesema.
Ameongeza kuwa mbali na upandaji miti, Watanzania pia wanapaswa kuzingatia maelekezo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kilimo himilivu na matumizi sahihi ya vyanzo vya maji – mambo ambayo ni sehemu ya mpango mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwisenge, Theopista Mashauri, amesema kupitia kampeni hiyo shule yake ilipanda miti 1,000 na kati ya hiyo, miti 968 imeweza kukua.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ufuatiliaji unaofanywa na uongozi wa shule mara kwa mara, lengo likiwa ni kuifanya shule hiyo kuwa ya kijani.
"Tunalenga ‘kuikijanisha’ Mwisenge. Ili kufikia lengo hili, yapo mambo kadhaa tuliyokubaliana, ikiwa ni pamoja na kila mwanafunzi kukabidhiwa mti wake ambao anatakiwa kuutunza hadi atakapohitimu kidato cha nne," amesema Mashauri.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wamesema kuwa ufuatiliaji baada ya upandaji wa miti ni jambo la msingi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
"Kuna baadhi ya maeneo Serikali inatumia fedha nyingi kupanda miti, lakini baada ya kuipanda inatelekezwa bila kuhudumiwa. Mwisho wa siku hakuna hata mti mmoja unaokua. Inabidi upandaji wa miti uende sambamba na mikakati ya kuihudumia," amesema Annasatazia Chacha.
Naye Richard Mabuba amesema kuwa endapo kutakuwa na usimamizi thabiti baada ya kila kampeni ya upandaji miti, suala la mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi litapata mafanikio makubwa.