Kila tukio la kitaifa hupanda mti

Bella akionyesha mojawapo ya miti aliyoipanda shambani mwake. Picha na Shakila Nyerere.
Muktasari:
Kila anapopanda mti huandika kibao cha tarehe aliyopanda na tukio lililomsababisha akaupanda; Baadhi ya matukio hayo ni vifo vya viongozi.
Unaposikia kitu cha maajabu lazima ushtuke kidogo, kisha ndio ufuatilie kwa ukaribu kujua nini hasa kilichoko kwenye maajabu hayo; hivyo ndivyo utakavyoona kwa mzee mbunifu wa kijiji cha Choka wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma.
Rajabu Bella ni mkulima mbunifu kutoka katika kijiji hicho cha Choka, anajishuhulisha na ubunifu wa kuhifadhi udongo kutoka katika kichanga na kuwa udongo mkavu pamoja na kupanda miti kutokana na matukio yanayojitokeza katika Dunia hii kwa ujumla.
Kazi kubwa anayoifanya ni kutunza mazingira na kuhifadhi udongo kwa kuua makorongo na upandaji wa miti kwa kadri matukio mbalimbali ya kihistoria ya kitaifa na kimataifa yanavyotokea .
Ukizingatia katika Mkoa wa Dodoma hupata msimu wa mvua mara moja kwa wastani wa milimita 500 hadi 800 kwa mwaka hali ya hewa ni kame yenye kipindi kirefu cha jua na mara nyingi hupata mvua chini ya kiwango cha wastani.
Hali hii inasababisha shuhuli za kilimo katika mkoa huu kuwa ngumu, uzalishaji umekuwa mdogo na matukio ya njaa yamekuwa yakitokea kila mwaka; baadhi ya kaya zimekuwa zikishindwa kujiitosheleza kwa chakula.
Kumekuwa na mvua zisizotabirika pamoja na mazingira yasiyo rafiki kwa shughuli za kilimo.
Ni kutokana na hali hii, Bella amekuwa akifanya shughuli za kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo, kuongeza rutuba katika udongo na kudhibiti uharibifu wa mazingira na udongo kwa kutumia makingamaji, kuua makorongo na kupanda miti mbalimbali.
Bella aliyezaliwa mwaka 1934 katika kijiji cha Choka wilaya ya Kondoa, ana mke, watoto wawili na wajukuu sita.
Alianza ubunifu wa kupanda miti na kutunza mazingira kuanzia miaka ya 1960. Anasema mwaka 1975, palipotokea oparesheni ya vijiji aliumizwa sana na namna oparesheni hiyo, ndipo alianza kupanda mti wa kwanza na kuweka maandishi yanayoeleza kwamba aliupanda siku ambayo oparesheni hiyo ilifanyika.
Anaeleza kuwa kulipotokea oparesheni ya vijiji, aliamua kupanda mti wa kwanza na kuweka kumbukumbu, kwani baadhi ya wananchi walilazimika kulala nje kutokana na oparesheni hiyo.
“Siku hiyo vijiji vingi vilipitiwa na oparesheni hiyo pamoja na hiki chetu, watu wengi tulipoteza mwelekeo, ikiwemo makazi yetu ya kudumu, niliamua kupanda mti aina ya mfurufadi na kuweka kibao cha kumbukumbu za oparesheni vijijini mwaka 1975. Niliendelea kufanya hivyo hadi sasa.Kabla ya hapo nilikuwa nikihifadhi mazingira tuu bila kupanda mti na kuweka maandiko rasmi,”anaeleza Bella.
Katika shamba hilo amepanda miti mbalimbali huku akiwa ameandika kumbukumbu za matukio mengi yanayojitokeza katika Taifa na Mataifa. Shamba hilo lina ukubwa wa ekari tano.
Bella anaeleza namna anavyokabiliana na changamoto za eneo hilo, akisema limekuwa halina rutuba na lina makorongo na mchanga, hivyo hujikuta muda mwingine kuutumia kwa ajili ya kusawazisha udongo.
Anasema kuna wakati hutumia makingamaji kupunguza kasi ya maji yanayopita katika shamba lake. Anasema maji hayo hasa yale yanayotoka mlimani huwa yana kasi kubwa hivyo wakati fulani hata huathiri miti yake.
Katika shamba hilo lenye ukumbwa huo wa ekari tano, Bella amepanda miti mingi ikiwamo ya matunda.
Mingine ni ya mbao aina ya migrevalia lakini kikubwa zaidi na ambacho kinawavutia wengi ni kuona vibao vilivyorembwa kwa rangi nyingi tofauti kwa kutunza kumbukumbu za matukio ya kitaifa na kimataifa.
Ukiingia katika shamba hilo utakutana na matukio ya kitaifa kwa mfano vifo vya wazalendo wa kisiasa, viongozi wa dini zote na viongozi wengine maarufu.
Aidha utaona matukio ya chaguzi za kisiasa, na mengineyo. Pia kuna vitu anavyovilinganisha na tukio lenyewe kwa mfano waandishi walivyowahi kupanda mlima Kilimanjaro na kufika katika kilele ameweka kilima na kuweka kibao kinachoonesha kupanda mlima kwa waandishi hao na kufika katika kilele.
Sababu ya kupanda miti
Anaeleza sababu ya kujikita katika upandaji wa miti, kuwa ni kwa sababu ya changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa wilaya hiyo ya ukame; kwamba anaamini kwa kupanda miti, angalau itapunguza hali mbaya ya ukame inayolisumbua eneo hilo.
Anasema anakerwa sana kuona baadhi ya watu wakichoma misitu moto, akisema kuwa kitendo hicho kinachangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Bella anasema pamoja na jitihada hizo, anakabiliwa na changamoto ya maji katika shamba hilo. Anasema maji anayotumia kuendeshea kilimo cha miti katika shamba lake ni ya mvua.
“Namshukuru Mungu kwa kunijalia nguvu na afya njema, hata hivyo huwa napata shida sana katika kipindi cha kiangazi, kwani maji huwa ni shida,” anasema na kuongeza:
“Huwa nalazimika kuyanunua maji kutoka kwa watu wanaoyauza, yanapatikana mbali, pia ni gharama kubwa ukilinganisha na uwezo nilionao wa kiuchumi,” anasema Bella.
Anaongeza kusema kuwa tangu abuni shughuli hiyo amekuwa anajitembelewa na watu wengi wakiwemo viongozi wa Serikali.
Hata hivyo analaumu kuwa hajui ni kwanini Serikali imekuwa haionyeshi kumjali kwa kumshirikisha kwenye sikukuu zinazohusiana na mazingira au kumsaidia kupata elimu zaidi ya utunzaji mazingira ili aweze kuifanya kazi yake hiyo vizuri zaidi.
“Sijawahi kuisomea wala sina elimu yoyote, naifanya kwa mazoea tu. Naifanya kwa sababu naipenda na kuielewa kwangu kidogo, kunatokana na mimi mwenyewe kuuliza kwa watu juu ya namna ya kutunza mazingira,” anasema.
Bella anasema ikiwa halmashauri au wataalamu mbalimbali wangeweza kushirikiana naye, angeweza kuwa na shamba lililo bora zaidi ya sasa, kwani anahisi kuna vitu anakosea kwa namna anavyolitunza shamba hilo.
“Naamini shamba hili ni muhimu sana kwa jamii ya Tanzania hasa watu walioko karibu zikiwamo shule kwa sababu kuna mambo mengi wanaweza kujifunza.Hata sasa nimekuwa nikipokea watu kutoka maeneo mbalimbali kuja kutembelea na kubaki wakifurahia,” anasema Bella ambaye ameonekana kama mfano wa kuigwa kutokana na harakati zake za kutunza mazingira.