Wingi wa madaktari wasio na ajira rasmi washtua

Muktasari:
- Licha ya Sh450 bilioni kutumika kusomesha madaktari nchini Tanzania, zaidi ya wahitimu 5,000 waliohitimu kada hiyo wanaelezwa hawana ajira rasmi.
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na changamoto za uhaba wa wataalamu wa afya katika vituo vya kutolea huduma nchini, takwimu zinazoonyesha idadi kubwa ya madaktari wako mtaani zimewashtua wadau.
Uhaba huo umekuwa ukisababisha adha kwa wagonjwa, kuwalazimu kusota kwa muda kwenye vituo vya kutolea huduma na wengine wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kadhia hiyo.
Hali ikiwa hivyo, si kwamba wataalamu hao hawapo nchini, la hasha, wapo wamejaa tele. Zaidi ya madaktari 5,000 waliohitimu na kuwa na sifa za kuajiriwa, wapo wanasota mtaani kwa kukosa ajira rasmi, kwa mujibu wa Dk Deus Ndilanha, rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).
Mwongozo uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) daktari mmoja anapaswa kuhudumia watu 10,000. Nchini Tanzania daktari mmoja, anahudumia wastani wa wagonjwa 20,000 katika maeneo ya mijini na 35,000 hadi 50,000 maeneo ya pembezoni.
Mjadala huo ulitokana na kilichotokea juzi kwenye kongamano la kitaifa la wadau wa afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo Profesa Abel Makubi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma (BMH) alipotoa maoni yake kuwa lazima kuwe na mikakati ili rasilimali fedha inayowekezwa kusomesha wataalamu hao haipotei.
"Ajira ni changamoto kubwa sekta ya afya, tunao zaidi ya madaktari 3,000 na manesi 25,000 hawana ajira, hili suala linaniogopesha sana. Lazima tuweke mikakati katika dira ijayo, hawa watu wasiendelee kuzagaa katika jamii yetu hii ionekane kwenye dira yetu," amesema Profesa Makubi.
Takwimu zilizopo
Kwa ujumla, takwimu zinaonyesha nchi inahitaji watumishi wa afya 348,923 lakini waliopo katika mfumo wa ajira mpaka sasa ni 126,925, hali inayoonyesha kuwepo kwa upungufu wa asilimia 64.
Ukiacha hali hiyo ya jumla, uhaba wa madaktari nao ni mkubwa ingawa wakati mwingine si rahisi kuonekana kwa macho kutokana na wale waliopo mafunzoni au wale wanaojitolea.
“Kila mwaka kuna kundi kubwa la madaktari wanahudumu hospitali mwaka mzima kimafunzo, hao ndio wanaofanya upungufu wao usionekane. Sababu ni jambo endelevu. Kuna kazi kubwa ya kufanya ili nguvu kazi hii isipotee bure,” ameandika Fredy Pastory, aliyetoa mawazo yake kupitia ukurasa wa Instagram wa Mwananchi.
Mtaalamu wa afya Mathew Mandikilo amesema: “Watu wamekopeshwa na Serikali, wengine wamepewa ufadhili, lakini wapo mtaani, maana yake pesa ya Serikali zinaendelea kutumika bila malengo.”
Mmoja wa vijana waliohitimu miaka ya karibuni (hakutaka kutaja jina lake), amesema amejitolea kwa kipindi kirefu Hospitali ya Rufaa Temeke bila ajira mpaka alikata tamaa na kuacha.
“Miaka mitatu sasa tangu niwe daktari ni mimi na mtaa tu. Niliamua kujitolea Temeke Hospitali ya Rufaa ili ujuzi usipotee baadaye nilichoka sababu sina mtaji wa kufanya kazi ya kujitolea. Darasani tulianza 436 tukamaliza 45 na bado wote hatuna ajira,” ameeleza daktari huyo.
Kutokana na hali hiyo, wadau wameitupia lawama Serikali kwa kutoipa kipaumbele sekta hiyo muhimu kwa kutenga fedha za kutosha kuwaajiri madaktari na wahudumu wengine wa afya, suala ambalo hata ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha.
Msemaji wa sekta ya afya wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga amesema kuna mambo mawili makubwa yakifanywa nchi itapata fedha za kuajiri madaktari, akitaja kupunguza matumizi na kutambua huduma zisizo na ubora wa afya kwa kuwa huko zinapotea fedha nyingi baada ya kutoa huduma hafifu awali.
Dk Sanga amesema chanzo cha fedha ni kwenye bajeti ya kuendesha Serikali ambayo ni kubwa kuliko misharaha ambayo ingelipwa kwa madaktari 5,000, akitaja kupunguza matumizi kwa wabunge pamoja na marupurupu yao.
“Kuna matumizi makubwa ya kuendesha Serikali hayana ulazima wowote kama kuongeza mashangingi (magari ya kifahari) kila mwaka huku mengine yakiachwa yanaoza, kila wizara ikikata fedha ikapeleka kwenye malipo muhimu, Wizara ya Fedha ingezichukua na kuajiri madaktari walio mtaani,” amesema.
Akifafanua, amesema magonjwa ngazi za msingi ambako kuna asilimia 80 ya Watanzania hayatambuliki mapema sababu hakuna madaktari, yakishakuwa sugu na kufika hatua za juu watu wanatibiwa ngazi za rufaa kwa gharama kubwa.
“(Serikali) Ingeajiri madaktari wakae huku chini, wangeyatambua magonjwa mapema na kuyatibu kwa gharama ndogo,” amesema Dk Sanga.
Athari kukaa mtaani
Mbali na upungufu wa wataalamu, zipo athari nyingine za kitaaluma pale daktari anapohitimu na akakaa bila kuufanyia kazi ujuzi wake, kama anavyoeleza Dk Ndilanha kuna athari, rais wa MAT.
“Udaktari ni taaluma na ukiacha kuwa anahitajika kuwa na ujuzi, lakini kama kuna kitu hakifanyi mara kwa mara uwezekano wa kukisahau huongezeka, ikilinganishwa na anayekifanya mara kwa mara, ataanza kusahau na atajikuta anafanya vitu vingine vinamtoa kwenye udaktari.
“Hawezi kusahau moja kwa moja, lakini kadri anavyokaa nje, atavisahau ataanza kufanya vitu vingine tofauti na udaktari,” amesema.
Majibu ya Waziri Ummy
Akizungumzia hilo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema nchi haina uhaba wa madaktari bali Serikali haina uwezo wa kuwaajiri wote.
"Changamoto kubwa kwenye sekta ya afya kwa sasa ni rasilimali watu, kwanza tunazalisha wa kutosha, nashukuru leo hatuna tatizo la madaktari na ndiyo maana wengine tunawapeleka Saudia, sababu hatuna uwezo wa kuwaajiri wote. Tunao wengi sokoni, tuna wauguzi wengi sokoni.
“Changamoto ipo kwenye baadhi ya fani, kwa mfano wataalamu wa radiolojia sio wa kutosha, lakini kuna wataalamu wa macho, kwa hiyo kuna baadhi ya maeneo wataalamu ni wachache, upungufu upo kwa asilimia 60,” amesema.
Waziri Ummy amesema pengo hilo limetokea kwa sababu wameongeza vituo kuanzia ngazi ya msingi kwa kuongeza zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, za mikoa, kujengwa kwa hospitali za rufaa za kanda na ongezeko la vifaa vya kisasa, hivyo kufanya uhitaji mkubwa.
Hata hivyo, mwandishi wa habari za sayansi ya tiba, Dk Syriacus Buguzi amesema idadi kubwa ya madaktari walio nje ya mfumo wa ajira ni kengele ya kuviamsha vyombo vya habari kukumbuka wajibu wake na kuacha habari za kusifia ajira mpya zinazotangazwa, bali la kuonyesha pengo lililopo.
“Wasio katika ajira na wana vigezo ni 5,000, ajira zimetangazwa 900 na kuna upungufu wa watumishi kwa asilimia 60 nchi nzima, lazima tuionyeshe jamii huu mchanganuo. Bila kufanya hivyo unaiacha jamii iamini Serikali inaajiri vizuri, ilhali hakuna huo uhalisia,” amesema Dk Buguzi na kusisitiza uandishi wa takwimu ni muhimu kwa vyombo vya habari.
Gharama kumpata daktari
Wakati madaktari wengi wakiwa nje ya mfumo, imeelezwa gharama za kumpata daktari mmoja zinaanzia Sh5 milioni kwa mwaka kulingana na kozi husika, na kuwa ili awe tayari kufanya kazi anaweza kugharimu hadi Sh90 milioni.
“Gharama huwa kubwa zaidi inategemea na daktari husika anasoma chuo gani cha umma au binafsi na ndani au nje ya nchi…,” amesema Dk Ndilanha.
Akifafanua zaidi gharama hizo, Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema mwaka wa kwanza daktari huanza masomo yake kwa kuingia darasani na kuanza kutumia vifaa mbalimbali zikiwemo mashine katika kujifunza.
Amesema daktari huyo hutumia zaidi maabara, darubini na mashine mbalimbali kwa vitendo zaidi na anapomaliza mwaka wa kwanza hutumia mwili wa binadamu halisi (miili ya watu waliofariki ambayo hutunzwa kwa gharama kubwa kwa ajili ya mafunzo, hapa anafundishwa mwili ulivyo na seli zake zote zinavyofanya kazi na aina zake.
Alichobaini CAG
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha unaoishia 2023, Tanzania ilikuwa na upungufu wa wataalamu wa afya 217 katika Hospitali za Rufaa, huku upungufu wa vifaatiba ukiwa ni 179.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ilikuwa na upungufu wa wataalamu 10 wa afya, kadhalika vifaa tiba 10.
Hospitali ya rufaa ya Ligula ilikuwa na upungufu wa wataalamu wawili na vifaatiba viwili, huku Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ikipungukiwa wataalamu 10 na vifaatiba 10.
Kwa upande wa hospitali ya rufaa ya Chato, upungufu wa wataalamu ulikuwa ni 13, huku vifaatiba 13 pia, wakati hospitali kama hiyo mkoani Iringa ilipungukiwa wataalamu saba.
Ripoti hiyo ilieleza hospitali kama hiyo mkoani Geita, ilipungukiwa wataalamu saba na vifaatiba saba, huku hospitali ya Songea ikipungukiwa wataalamu 18 wa afya.
Kwa upande wa Shinyanga, ilipungukiwa wataalamu wa afya 10 na vifaatiba 10, Simiyu wataalamu wa afya 13, Bukoba wataalamu wa afya sita Mtwara wataalamu 13 na Njombe wataalamu 12.
Hospitali za rufaa za Tumbi ilipungukiwa wataalamu wa afya 24, Songwe 19, Tabora 21, Singida 14 na Maweni ni 18.