Madaktari 3,000, wauguzi 25,000 nchini hawana ajira

Muktasari:
- Ada ya masomo ya udaktari imetajwa kuanzia Sh5 milioni kulingana na kozi husika kwa mwaka, na ili daktari ahitimu masomo gharama si chini ya Sh60 milioni.
Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya afya wametoa maoni wakitaka muundo rasmi uwepo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupambana na changamoto ya wahitimu kada ya afya wasio na ajira, hususani madaktari na wauguzi.
Profesa Abel Makubi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), iliyopo jijini Dodoma amesema lazima kuwe na mikakati ili rasilimali fedha inayowekezwa kusomesha wataalamu hao isipotee.
Ametoa maoni kwenye kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, linalofanyika leo Jumamosi, Julai 6, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).
"Ajira ni changamoto kubwa sekta ya afya, tunao zaidi ya madaktari 3,000 na manesi 25,000 hawana ajira, hili suala linaniogopesha sana. Lazima tuweke mikakati katika dira ijayo, hawa watu wasiendelee kuzagaa katika jamii yetu hii ionekane kwenye dira yetu," amesema.
Kwa mujibu wa Rais Mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko ili daktari aweze kuhitimu chuo, hutumika si chini ya Sh60 milioni.
"Chuo cha umma gharama zinaanzia Sh5 milioni sasa kwa miaka mitano ni Sh25 milioni, ukija kwenye vyuo binafsi gharama yake ni Sh8 milioni kwa miaka mitano Sh40 milioni, ukihesabu uliishije na mambo mengine si chini ya Sh60 milioni," amesema Dk Nkoronko.
Akilizungumzia hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuna changamoto kubwa ya wahitimu wasio na ajira madaktari, walimu, mainjinia ambao pia wanahitajika sana.
"Tuna changamoto kwa wasomi na wafanyabiashara, kazi zipo duniani pia huko Magharibi, Japan wana shida ya watu wa kuwaajiri, ni vema wasomi wetu kuanza kufikiria nafasi nje ya Tanzania na fursa zipo nyingi, pia Serikali itajitahidi kuongeza ajira inapobidi," amesema Profesa Kitila.
Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Alexander Bahulya amesema uwekezaji wa watumishi wa afya bado ni changamoto.
Amesema mafanikio mengi yamepatikana katika sekta ya afya lakini uwekezaji kwa wafanyakazi imekuwa changamoto.
"Lazima tujiwekee mikakati miaka 25 ijayo tuna mpango gani katika rasilimali watu, tumewezesha kiasi gani kutekeleza majukumu yetu ya kuhudumiwa Watanzania.”
"Sera ya afya inatoa tamko gani uwezeshaji wa wahudumu wa afya, mabaraza ya vyama vya kitaaluma yanatumika kiasi gani, miongozo mbalimbali ambayo wataishauri Serikali kuna mwingiliano mkubwa wa utendaji kazi kwa viongozi kuingilia mihimili hii," amesema.
Mambo tisa
Ajira ni miongoni mwa mambo tisa yaliyoibuliwa na wadau wa sekta ya afya ikiwemo ugharimiaji wa huduma za afya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mengine ni uwekezaji katika kinga, ubora wa huduma, tafiti, teknolojia, watoa huduma za afya ngazi ya jamii, uwajibikaji na kupimwa utendaji wa watumishi.
Profesa Makubi ametaja pia uwekezaji eneo la upatikanaji wa dawa, kwa kuwekeza katika viwanda vya dawa, na ugharimiaji wa afya kupitia bima ya afya.
"Bima ya afya peke yake haiwezi kukidhi ugharimiaji wa huduma za afya, lazima tuwe na mfuko wa afya zaidi ya bima ya afya, bila kuwa nao hatuwezi kuhudumia wasio na uwezo.”
"Kama tunaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa nini tusiweke bajeti ya bima ya afya ni suala la maamuzi tu," amesema Profesa Makubi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Akizungumzia hali halisi ya uchangiaji wa sekta binafsi nchini, kwa niaba ya Aphtha, Profesa Kaushik Ramaiya amesema ina nafasi kubwa ya kukuza teknolojia ya afya.
"Sekta binafsi itumike pia kuboresha teknolojia kwa sekta ya umma kutokana na changamoto ya mabadiliko ya maradhi, lazima tushirikishane kwa pamoja kwa sababu sisi tunaongoza katika upande wa teknolojia," amesema.
Mkurugenzi wa Mpaka Foundation, Dk Ellen Senkoro amesema kuelekea mwaka 2050 lazima nchi iwekeze kwenye kinga na si katika tiba pekee, kuwe na sera na miongozo ya misingi katika afya ya msingi.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejikita katika maeneo sita ikiwemo maboresho ya kiuchumi, kijamii, utawala bora, haki na amani, sayansi ya mabadiliko ya kidijitali, utunzaji mazingira na mabadiliko ya tabianchi.