Serikali yatangaza ajira za wahudumu wa afya 8,900

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
Muktasari:
- Katika kuhakikisha mpango jumuishi wa wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii nchini unafanikiwa kwenye mikoa 10 ya awali, Serikali imetangaza nafasi za kazi 8,900 kwa wahudumu watakaokwenda kutekeleza afua jumuishi za afya maeneo ya vijiji na vitongoji.
Dar es Salaam. Serikali imetangaza nafasi za kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 8,900 watakaokwenda kutekeleza afua jumuishi za afya, lishe na ustawi wa jamii katika ngazi ya vitongoji na vijiji.
Tangazo lililotolewa leo Jumamosi Aprili 6, 2024 na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais Tamisemi limeeleza kuwa hivi sasa Serikali inatekeleza mpango jumuishi wa wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii nchini.
Kupitia mpango huo, Serikali imeweka utaratibu wa kuwapata wahudumu wenye sifa zilizowekwa kutoa mafunzo na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika utekelezaji wa afua hizo. Mpango huo unahitaji wahudumu wawili mwanamke na mwanaume.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, awamu ya kwanza ya mpango huo utaanza kwenye mikoa 10 na halmashauri mbili kwa kila mkoa na itakayonufaika ni Geita wahudumu 920, Kagera (878), Kigoma (1094), Lindi (1724), Mbeya (836), Njombe (746), Pwani (480), Songwe (774), Tabora (966) na Tanga (482).
“Utekelezaji wa mpango huu utaendelea kwa awamu katika mikoa na halmashauri zote za Tanzania Bara, wananchi wenye sifa stahiki ndani ya mikoa 10 wanahimizwa kuomba nafasi za wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika mitaa na vitongoji vyote ndani ya halmashauri zao.
“Maombi yote yawasilishwe kwa wakurugenzi wa halmashauri, watakaosimamia mchakato huu wa kuwachagua wahudumu wenye sifa miongoni mwa waliotuma maombi kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa,” imeeleza sehemu ya tangazo hilo.
Tangazo hilo limeanisha miongoni mwa sifa za waombaji ni pamoja na utambulisho rasmi wa Kitambulisho cha Taifa (Nida), hati ya kusafiria leseni ya udereva au kitambulisho cha mpiga kura. Pia awe amemaliza elimu ya sekondari (angalau kidato cha nne) na awe na cheti cha kuhitimu.
Sifa zingine mwombaji awe mkazi anayeishi katika kitongoji, kijiji na mtaa husika, afahamu lugha, utamaduni, mila na desturi za jamii husika, akubalike kimaadili na kiutamaduni na jamii husika.
Maombi hayo yatatakiwa kuwasilishwa ofisi ya mtendaji wa kata yakiambatanishwa na barua ya maombi ya kazi iliyoandikwa kwa mkono na kuwekwa saini ya mwombaji, maelezo binafsi (cv), cheti cha kidato cha nne, namba za kiganjani za wadhamini wasiopungua wawili.
“Mwisho wa kuwasilisha maombi haya ni wiki mbili tangu tarehe ya kutolewa kwa tangazo hili.”
Januari 31 mwaka huu, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema Serikali imetenga Sh899.4 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kuajiri na kuwajengea uwezo jumla ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 137,294 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Dk Mpango alieleza hayo kwenye uzinduzi wa mpango jumuishi wa huduma za afya ngazi ya jamii, akisema kuna upungufu wa asilimia 64 ya watoa huduma za afya, hivyo ni muhimu kuwatumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii ili kuimarisha huduma.
Katika mkutano huo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema watoa huduma za afya ngazi ya jamii wataongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya, kupunguza mzigo kwenye vituo vya afya kwa kuimarisha kinga ya maradhi katika jamii.