Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kuajiri watoa huduma za afya wawili kila kijiji

Muktasari:

  • Serikali inakwenda kushughulikia mambo manne yaliyoibuliwa katika mkutano wa 10 wa Afya Tanzania uliomalizika jana, ikiwemo uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuajiri watoa huduma za afya ngazi ya jamii ili kufikia afya kwa wote sambamba na kuanzisha taasisi ya afya ya jamii.

Dar es Salaam. Serikali imetaja mambo manne yanayokwenda kufanyiwa kazi ambayo yameibuliwa katika Mkutano wa 10 wa Afya Tanzania (THS) ikiwemo uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuajiri wafanyakazi wa afya ngazi ya jamii 153,308 ili kufikia lengo la afya kwa wote.

Katika kutekeleza hayo, Serikali imesema inakusudia kuajiri watoa huduma hao wawili katika kila kijiji na msimamizi mmoja ili kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii.

Hayo yamesemwa jana Oktoba 5, 2023 na Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia afya, Dk Charles Mahera wakati akifunga mkutano huo wa siku tatu uliowakutanisha wataalamu, madaktari, watafiti na wadau mbalimbali wanaoshughulikia afya nchini.

“Haya ni maandalizi kuelekea afya kwa wote Serikali tumejipanga kuajiri kila mwaka 51,192 hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu tutafikia lengo la kuhakikisha tunavifikia vitongoji 64,384 katika vijiji 12,300, hatuwezi kufanya peke yetu tunatoa wito kwa wadau kuongeza nguvu kushughulikia hili,” amesema.

Mahera amesema kuna umuhimu wa kuongeza nguvu na kuwekeza katika afya ya msingi kwani asilimia 85 ya Watanzania wanapata huduma katika ngazi za chini.

“Wataalam wakuu na watendaji wametoa mada anuwai, ikijumuisha umuhimu haya maeneo manne, kama tunavyojua afya ya msingi ni  mfumo thabiti wa afya na ni hatua ya kwanza ya mawasiliano kwa watu wengi wanaotafuta huduma ya afya na muhimu kwa kuzuia na kutibu pia kutoa huduma ya kina kwa wajawazito na watoto,” amesema Mahera.

Wakati huohuo, Serikali ya Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinakusudia kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya ya Jamii ili ziweze kuimarisha uwezo wa nchi katika kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya milipuko pamoja na majanga.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyasema hayo Octoba 3 mwaka huu wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi.

“Rais Mwinyi, kwako kupitia Waziri wa Afya Zanzibar Nassoro Ahmed Mazrui tumesema ni wakati sasa umefika tuanzishe Taasisi za Taifa za Afya ya Jamii ili nchi zetu ziweze kuratibu hili na tutaendelea kushirikiana na wadau, mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuimarisha huduma za afya nchini.”

Pia amesema Serikali imeamua kuja na mpango mmoja na jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuimarisha huduma za afya ngazi ya msingi ambapo Wizara imeshatengeneza mtaala ambao watapatiwa mafunzo ya miezi sita ili waweze kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

Amesema wahudumu hao wamekuwa wakisaidia kuibua wagonjwa wa kifua kikuu pamoja na kushughulikia masuala mbalimbali ya mama na mtoto.

Sambamba na hilo, amesema ili kufikia lengo la huduma za afya kwa wote ni lazima kuzingatia ubora wa huduma, ugharamiaji wa huduma za afya kupitia bima ya afya kwa wote pamoja na kuimarisha huduma za kinga.

“Bado Serikali tunayo dhamira ya dhati ya kuendelea na mchakato wa muswada wa Bima ya Afya kwa wote ili kuwarahisishia Watanzania kupata huduma kwa haraka na bila kikwazo cha fedha,” amesema Waziri Ummy.