Serikali yatangaza ajira mpya 137,29 ngazi ya jamii

Muktasari:
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kuna upungufu wa asilimia 64 ya watoa huduma za afya, hivyo ni muhimu kuwatumia wa ngazi ya jamii kuimarisha huduma za afya
Dar es Salaam. Serikali imetangaza kutoa ajira 137,294 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa kwa Watoa Huduma wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW.
Tayari Serikali imetenga Sh899.473 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango huo kwa kuwapa ajira wahudumu hao katika maeneo yao vijiji, vitongoji, mitaa pamoja na kujengewa uwezo.
Baada ya kupata ajira, watoa huduma hao watajikita kutoa elimu ya afya kwa jamii, kutoa huduma za kinga, huduma tembezi na mkoba na huduma za awali za tiba kabla ya kumpa mgonjwa rufaa kwenda hospitali kupatiwa matibabu.
Hatua hiyo ya Serikali imetangazwa leo Jumatano Januari 31, 2024 na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa Uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Huduma ya Afya Ngazi ya Jamii jijini Dar es Salaam.
Dk Mpango amesema upo upungufu wa asilimia 64 ya watoa huduma za afya, hivyo ni muhimu kuwatumia watoa huduma wa afya ngazi ya jamii kuimarisha huduma za afya.
“Watoa huduma ya afya ngazi ya jamii watafanya uchunguzi wa awali wa magonjwa na kuyabaini katika hatua za awali, kutoa kinga na kuipunguzia Serikali gharama za ununuzi wa dawa ambayo kwa mwezi imefikia Sh200 bilioni,” amesema Dk Mpango.
Amesema CHW watachaguliwa kuanzia ngazi ya mitaa,vitongoji na vijiji hivyo wananchi waitumie fursa hiyo kupata ajira huku akisisitiza viongozi watakaosimamia upatikanaji wa watoa huduma hao wazingatie uadilifu na kuepuka rushwa ili wapatikane watoa huduma watakaofanikisha mpango huo wa Serikali.
Watumishi hao watakaoajiriwa, Dk Mpango amesema watajikita kutoa elimu ya uzazi wa mpango, kubaini magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza katika hatua ya awali ndani ya jamii hasa kifua kikuu, malaria, matatizo yatokanayo na lishe, afya ya uzazi wa mama na mtoto pamoja na kuhamasisha usafi wa mazingira.
“Tunafanya kazi kubwa kugundua matatizo kwa haraka na kuripoti kwa wataalamu kilichofanywa na Serikali ni hatua kubwa ambayo inakwenda kuimarisha afya ya wananchi kwenye jamii,” amesema Dk Mpango.
Mmojwa wawato huduma hizo, Anastazia Hassan amesema kutambulika kwao kunawapa moyo wa kufanya kazi kwa bidii ndani ya jamii kukabili maradhi mbalimbali.
Maagizo ya Dk Mpango
Katika maagizo yake, Dk Mpango amezielekeza Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tamisemi kuhakikisha usimamizi madhubuti wa mpango huo kwa kuweka mfumo mzuri wa uratibu na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinapatikana.
“Jambo linguine, Wizara ya Afya ihakikishe inatoa elimu na hamasa kwa jamii kuhusu mpango huu ili kurahisisha utekelezaji wake, jamii nayo ipokee mpango huu na kuudhamini ili kulinda na kuboresha afya,"amesema Dk Mpango.
Pia, amesisitiza watoa huduma kuzingatia weledi na wadau wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mpango huo.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema watoa huduma za afya ngazi ya jamii wataongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini na kupunguza mzigo kwenye vituo vya afya kwa kuimarisha kinga ya maradhi kwenye jamii.
Ummy ametolea mfano namna watoa huduma za afya ngazi ya jamii walivyosaidia kuibua magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu mkoani Mwanza na ugonjwa wa Maburg Mkoa wa Kagera.
“Ukiangalia Ugonjwa wa Kifua Kikuu katika kila wagonjwa 100, wagonjwa 50 wameibuliwa na watoa huduma wa afya ngazi ya jamii, kwa hiyo watakwenda kupunguza gharama za kuwatibu watu, Taasisi ya Satani Ocean Road wagonjwa wanafikia tatizo likiwa hatua za mwisho, kisukari na matatizo ya figo wagonjwa wanachelewa kubaini matatizo haya,” amesema Ummy.
Ummy amedokeza kuwa watoa huduma hao hawatakwenda kuchukua nafasi ya wataalamu wa afya, bali watakuwa daraja la kati ya wananchi na watoa huduma za afya.
Ummy amesema CHW wamewekewa malengo ya kufikia kaya 25 kwa wiki na 100 kwa mwezi na wote watawajibika chini ya kituo cha afya kilichopo karibu naye chini ya mtendaji wa kata.
“Watoa huduma hao watawezeshwa vitendea kazi, mafunzo kwa miezi sita darasani na nje ya darasa pamoja na malipo yao kwa asilimia 100, Shirika la Globalfund litagharamia mafunzo kwa watoa huduma 500 kwa miaka mitano,” amesema Ummy.
Akihitikisha hotuba yake, Ummy ametaja changamoto zilizopo katika sekta ya afya kwa sasa ni ugharamiaji wa huduma na ubora wa huduma za afya.
“Hizo ndio changamoto zinazoikabili sekta ya afya, lakini watoa huduma zetu wanafanya kazi kubwa sana,kwa wachache wanaokwenda kinyume na miiko ya afya tutawafutia leseni zao kufanya kazi ndani na nje ya nchi,” amesema Ummy.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dk Faustine Ndugulile amesema mpango huo jumuishi ni hatua nzuri ya kutokomeza Kifua Kikuu na Malaria kufikia mwaka 2030.
“Sisi kama Bunge tunataka kuona mpango huu ni endelevu kufikia malengo yaliyokudiwa,” amesema Dk Ndugulile.
Mwakilishi wa Asasi za Kiraia, Dk David Sando amesema watoa huduma wa afya ngazi ya jamii wakitumika ipasavyo mpango wa kujenga jamii imara utafanikiwa. Amewataka wadau kuunganisha nguvu na Serikali kutoa fedha ili kuifanya mpango huo kuwa endelevu.