Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wawili wateketea magari mawili yakigonga na kuwaka moto Mufindi

Gari kubwa  ambalo limeteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso na gari ndogo  aina Toyota Double cabin kisha kuwaka moto. Picha na Mary Sanyiwa

Muktasari:

  • Gari hilo liligongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Toyota Double Cabin namba zake bado hazijulikani   likitokea Makambako kuelekea Iringa likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika na kusababisha magari yote mawili kuwaka moto na kuteketea.

Iringa. Watu wawili wameteketea kwa moto na kubaki majivu baada ya ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha magari mawili kugongana uso kwa uso na baadaye kushika moto katika eneo la Sao Hill, msitu wa Mnara wa Voda, barabara kuu ya Iringa-Njombe.

Ajali hiyo imetokea saa 1:05 usiku wa kuamkia Mei 28, 2025, na kuthibitishwa na Kamanda  wa Polisi Wilaya ya Mufindi, Anthony Gwandu, ambaye amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva.

Akizungumza katika eneo la tukio leo Alhamisi Mei 29,2025 Gwandu amesema  ajali hiyo ilihusisha gari kubwa aina ya Iveco Tanker, lililokuwa likiendeshwa na Gimson Lungu (32), raia wa Zambia na mkazi wa Lusaka, ambalo lilikuwa limebeba mafuta ya dizeli likitokea Dar es Salaam kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na gari dogo aina ya Toyota Double Cabin ambalo namba zake bado hazijafahamika.

Gari kubwa  ambalo limeteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso na gari ndogo  aina Toyota Double cabin kisha kuwaka moto. Picha na Mary Sanyiwa

“Gari hilo dogo lilikuwa likitokea Makambako kuelekea Iringa na liligongana uso kwa uso na tanker, magari yote mawili yalishika moto na kuteketea kabisa,” amesema Gwandu.

Amesema kuwa watu wawili waliokuwa kwenye gari dogo wameungua hadi kubaki majivu, na hadi sasa utambuzi wao haujafanyika kutokana na hali ya miili yao.

Mkuu huyo wa Polisi amebainisha kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ni watu wangapi walikuwemo kwenye gari dogo zaidi ya dereva, huku dereva wa gari la mafuta akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.

“Chanzo cha ajali hii bado kinachunguzwa kwa kina, lakini kwa sasa tunaendelea na hatua za awali za uchunguzi ili kubaini idadi kamili ya waliokuwemo kwenye gari dogo pamoja na sababu halisi ya tukio,” amesema.

Jeshi la Polisi limewataka madereva kuwa waangalifu na kuzingatia sheria za usalama wa barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.