‘Sitasahau tukio la moto wa Mbeya’

Hili ni kabauri walimozikiwa watu zaidi ya 42 waliyoungua kwa ajaili ya moto maeneo ya isongole kijiji cha idweli mwaka 2000
Muktasari:
Wanalinganisha moto huo na wa Sodoma na Gomola unaotajwa kwenye Biblia Takatifu ingawa tofauti iliyopo ni kwamba ule wa kale uliangamiza watu waliokithiri kwa kutenda maovu.
Oktoba ya kila mwaka ni mwezi ambao Wakazi wa Idweli wilayani Rungwe wanaukumbuka tukio la kutisha lililowahi kutokea mwanzoni mwa miaka 2000 na kuweka historia mbaya katika maisha yao.
Wanalinganisha moto huo na wa Sodoma na Gomola unaotajwa kwenye Biblia Takatifu ingawa tofauti iliyopo ni kwamba ule wa kale uliangamiza watu waliokithiri kwa kutenda maovu.
Watu karibu 40 waliteketea kwa moto na wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa vibaya na kulazwa katika hospitali za Makandana na Igogwe wilayani Rungwe na wengine Kituo cha Afya cha Igawilo na Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Hata hivyo, ofisi ya Kijiji cha Idwele haina takwimu kamili za waliofariki kwa kuwa viongozi na wakazi wake wanatoa takwimu tofauti wakisema waliofariki walikuwa 30, 50, 80 na hata 100.
Moto huo ulitokea Oktoba 2002 baada ya lori la mafuta lililotoka Dar es Salaam likielekea Malawi kuanguka kutokana na utelezi katika mteremko unaoishia kwenye kijiji hicho.
Kwa mujibu wa ofisa mtendaji wa kijiji hicho,
Julius Mwangola mara baada ya ajali hiyo, watu mbalimbali kutoka kijiji hicho na wengine wa Vijiji vya Mchangani, Ndaga na Isyonje ambao waliokuwa wakishuhudia mchezo wa mpira kijijini hapo, waliamua kutimkia kwenye ajali hiyo kwa malengo ya kuchota mafuta.
Umati wa watu ulifika eneo la tukio ukiwa na madebe, ndoo, madumu chupa kwa malengo ya kuchota mafuta, lakini wengine walienda mbali kwa kutaka kuiba betri ya gari.
Kama waswahili wasemavyo “cha mtu mavi’’, ghafla moto ulilipuka na kuwaua watu na kusababisha wengine wengi kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mathew Kazimoto anasema watu walifariki katika hali ambayo inatisha.
“Wapo walioteketea kwenye tukio, wapo waliofariki baada ya kukimbia nusu kilometa na wengine waliokotwa baada ya siku mbili kwenye mashamba wakiwa wamefariki,’’ anasema.
Anasema tukio lile lilikifanya kijiji kizike watu bila ya kuweka matanga, kwani karibu mwezi mzima kijiji kilikuwa kikifanya shughuli za maziko kutokana na ukweli kwamba wengi walikuwa wakifa kwa siku tofauti kulingana na majeraha waliyoyapa.
“Matokeo yake kijiji kilibaki na yatima wengi pamoja na wajane kwa kuwa walioshiriki katika shughuli hiyo wengi walikuwa wanaume wenye familia zinazowategemea,’’ anasema.
Mwenyekiti huyo anasema moto wa ajali ya lori uliua wengi na kuwaacha wengine wakiwa hawana uwezo kama zamani baada ya kupata majeraha makubwa.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni Exavery Pascal (45) ambaye aliuguza majeraha kwa muda wa miezi mitatu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Kwa sasa, Pascal anaishi Kijiji cha Idweli akiwa mwathirika ambaye uwezo wa kuchapa kazi kwa sasa umepungua kutokana na kuwa na makovu makubwa mwilini. Kutokana na makovu hayo, Pascal hawezi tena kulima kama zamani.
Paschal anasema kila akikumbuka tukio hilo, machozi humtoka kwa vile alishuhudia wengi wakikata roho, kuanzia kwenye tukio hadi hospitalini.
“Mpaka sasa naamini moto ule wa Petroli ulikuwa wa kiama kwa kijiji chetu,’’ anasema.
“Nakumbuka Oktoba 2000, saa 10.00 jioni niliamua kuelekea kwenye klabu ya pombe za kienyeji. Nikiwa njiani niliwaona watu wakikimbia kufuata barabara kuu ya Tukuyu- Mbeya kuelekea mlimani ambako walisema lori limeanguka na linamwaga mafuta,’’ anasema.
Pascal anasema alifika eneo hilo na kushuhudia watu wakichota mafuta, lakini ghafla alisikia kishindo cha moto uliowaunguza wengi.
“Niliamua kujitosa kuwaokoa waliokuwa wakitapatapa na ndipo moto ule uliponirukia na kuniunguza usoni, mikono na karibu mwili wangu wote,’’ anasema.
Anasema yeye aliokolewa na mwanakijiji mwenzake anayeitwa Japhet Sanga na baadaye kuchukuliwa na dada yake, Lucy Pascal aliyempeleka Hospitali ya Makandana wilayani Rungwe na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Asimulia ya hospitalini
‘’Pale Hospitali ya Rufaa tulikaa siku nne bila kupewa dawa wala chakula. Tuliambiwa tupewe maji pekee ili kutoa sumu mwilini. Baadaye tulianza kupata dawa ambazo wauguzi walitueleza kwamba zilitolewa na Rais Benjamin Mkapa kwa kipindi hicho, lakini nakumbuka wenzangu wengi walikuwa wakifariki kila siku, hivyo hata mimi nilishakata tamaa,’’ anasema.
Pascal anasema Rais Mkapa ndiye aliyokoa maisha yake na ya wengine kwani ndiye aliyetoa msaada wa dawa za bure.
‘’Mimi nilikaa hospitalini pale miezi mitatu nikiuguzwa na kusaidiwa na mama yangu mzazi, Maria Pascal (76) ambaye ni mjane kwani mke wangu wakati huo alikuwa amejifungua mtoto hivyo asingeweza kukaa hospitalini kunihudumia,’’ anafafanua.
Anasema baada ya kutolewa hospitali ya Rufaa aliendelea kupata dawa kwenye zahanati ya kijiji chake hadi alipopona ingawa watalaamu walimshauri asifanye kazi ngumu kutokana na makovu kuwa makubwa.
Wosia kwa watoto wake
Pascal anasema kwa sasa kila akikumbuka ajali hiyo, anaweweseka. Kwa hiyo anachofanya sasa ni kuwaelimisha watoto wake kwamba si vizuri kwenda kwenye matukio ya ajali za magari.
‘’Usia huu nautoa kwa watoto wangu na wale ndugu zangu wote, nawasihi na wengine waache kukimbilia kwenye maeneo ya ajali, ni hatari.’’ anasisitiza.
Idweli ilipo
Kijiji cha Idweli kipo wilayani Rungwe na ni moja ya vijiji vinavyopitiwa na barabara kuu ya kuanzia Uyole jijini Mbeya kuelekea Malawi kupitia Kyela. Kijiji hiki kipo umbali wa kilometa 27 kutoka jijini hapa na pia kipo kilometa 26 kutoka Tukuyu ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Rungwe.
Kijiji cha Idweli kipo kwenye bonde dogo baada ya kuteremka umbali wa karibu kilometa sita mteremko unaoanzia Kijiji cha Isyonje hadi kijijini hapo.
Matukio mengine ya moto
Wiki iliyopita jijini Dar es Salaam watu zaidi ya watano walipoteza maisha na wengine 16 walijeruhiwa baada ya lori la mafuta kulipuka wakati baadhi yao wakiwa katika zoezi la kuchota mafuta na mmoja wao kuwasha mshumaa.
Mwaka 2011, watu watano walikufa papo hapo wakibaki majivu na mafuvu na wengine 46 kujeruhiwa vibaya baada ya kuungua na moto petroli uliolipuka wakati wakijaribu kuiba mafuta kwenye gari aina ya fuso lililogonga injini ya treni katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.