Watu 66, 400 wana VVU Mara, asilimia 96 wanajua hali zao

Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Bunda wakiwa kwenye foleni kwaajili ya kupima virusi vya Ukimwi wakati wa maadhimisho ha siku ya Ukimwi duniani. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Zaidi ya watu 66,400 wanakadiriwa kuwa na Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi mkoani Mara huku maambukizi ya mkoa yakiwa  ni asilimia 3.6 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini ikiongoza kwa kuwa na maambukizi kwa asilimia.3.8

Bunda. Mkoa wa Mara unakadiriwa kuwa na watu 66,436 wanaoishi na virusi vya Ukimwi huku kati yao 64,315 wanajua hali yao ya maambuki sawa na asilimia 96.8.

Kati ya hao wanaokadiriwa wanaume ni 20,109, wanawake 44,206 na watoto ni 2, 137.

Takwimu hizo zimetolewa leo Ijumaa Desemba Mosi na Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Mara, Dk Omari Gamuya kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi ambayo ki mkoa yamefanyika katika kijiji cha Kisorya wilayani Bunda.

"Wateja 61,099 tayari wameanza dawa na kati yao 60,489 wamefubaza virusi sawa na asilimia 99 ya wateja wote wanaotumia dawa mkoani hapa," amefafanua Dk Gamuya 

Amesema maambukizi ya Ukimwi kwa Mkoa wa Mara ni asilimia 3.6 ambapo kwa ngazi ya halmashauri,  halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini inaongoza kwa kuwa na asilimia 3.8.

Ameongeza kuwa Halamshauri ya Wilaya ya Rorya ni ya pili kwa kuwa na asilimia 3.6 huku Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ikiwa na kiwango  kidogo cha maambukizi kwa asilimia 1.2.

Akizungumzia katika maadhimisho  hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda; Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amesema  mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi ni jukumu la jamii nzima.

"Siku hii itumike hasa katika kukumbushana juu ha umuhimu wa kupambana na Ukimwi, jamii ijue Ukimwi bado upo na itambue kuwa ina wajibu wa kushiriki moja kwa moja kwenye mapato," amesema 

Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwaajili ya huduma za Ukimwi ikiwepo ongezeko la vituo vya kutolea huduma mkoani Mara  kutoka vituo 134 mwaka 2022 hadi vituo 174 mwaka huu.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Bunda wamesema ipo haja ya Serikali na wadau kuongeza jitihada zaidi katika kupambana na ugonjwa huo, hatua  ambayo itasaidia kupunguza au kumaliza kabisa maambukizi mapya.

"Siku hizi masuala ya Ukiwmi hayapewi kipaumbele kama zamani sijui kimetokea nini hapa katikati ni vema ile nguvu iliyotumika kipindi cha mwanzo ikarejea,”amesema Abdul Athumani 

Mwijarubi Mashauri amesema kipindi cha nyuma jamii ilipata elimu ya kutosha hali ambayo  ilisaidia katika kupunguza maambukizi na kwamba endapo kasi ya elimu na hamasa iliyokuwepo awali ingeendelea hivi sasa maambukizi yasingekuwepo.

"Kipindi kile kila kona kulikuwa na elimu ya ukimwi kwa njia mbalimbali lakini sasa hivi pametulia kama vile ugonjwa haupo yaani habari za Ukimwi tunazisikia siku ya maadhimisho tu hii sio nzuri kabisa," amesema Mashauri