Watalii wakubali masharti waone alipofia mama yake Chifu Mkwawa

Muktasari:
- Wadau wa Utalii kutoka katika mikoa 10 ya kusini wa Tanzania wamelazimika kila mmoja kuchuma jani la mti na kwenda kurundika karibu na eneo alilofia mama yake Chifu Mkwawa, ili waone.
Iringa. Tangazo la kumtaka kila mmoja achume jani la mti ili kutupa karibu na eneo alilofia mama yake Chifu Mkwawa, katika eneo la Kikongoma wilayani Iringa lilimfanya kila mdau wa utalii aliyeenda eneo hilo kutii.
Historia inaonyesha kuwa mama yake Mkwawa alijiua baada ya kujitumbukiza kwenye daraja la Mungu eneo la Kikongoma akikwepa kutoa dawa inayoitwa 'Luhoma' ambayo ilikuwa ikimsaidia mwanaye Mkwawa vitani.
Eneo hilo linaitwa daraja la Mungu kutokana na mawe kujipanga juu kwa zaidi ya mita 150 huku chini Mto Ruaha Mdogo ukipitisha maji yake.
Ofisa Utalii wa Iringa Vijijini, Abineli Msovela ndiye aliyetangaza kila mdau wa Utalii aliyetembelea eneo hilo kuchuma jani ili aone mama Mkwawa alipofia.
"Jamani, eneo hili linamatumizi mengi, wapo ambao huwa wanakuja hapa kutambika, kusali na vitu vingine. Sherti hapa ni kuchuma jani na kuja kurundika," amesema Msovela.
Jimson Sanga, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa na Mkurugenzi wa Makumbusho ya Boma Iringa amesema eneo hilo limekuwa likitumika kama sehemu ya Utalii.
"Huyu mwanamke aliyejiua hapa akitetea mwanae asidhulike ni shujaa, kama Ile dawa angewapa adui wa Mkwawa maana yake angekuwa anamsaliti mwanaye. Hii ni historia yetu," amesema Sanga.
Kwa upande wake Mercy Ishengoma, Afisa Raslimali watu wa Kampuni ya Qwihaya amesema ni muhimu kuendelea kutangaza vivutio hivyo ili vijulikane.
"Waliposema tuchume majani niliogopa na kwa kweli sijafika alipofia mama yake Mkwawa, hiki ni kivutio kizuri nawashauri waendelee kutangaza," amesema Ishengoma.