Tembeleeni Boma kujua historia ya Iringa na Chifu Mkwawa - Sanga

Baadhi ya wadau wa Utalii wakiwa nje ya Makumbusho ya Boma yaliyokusanya historia ya Chifu Mkwawa na Mkoa wa Iringa.
Muktasari:
- Mratibu wa Makumbusho ya Iringa Boma, Jimson Sanga amewashauri Watanzania kutembelea maeneo yanayo hifadhi historia ili kujua simulizi za mababu zinazoweza kuwasaidia katika maisha ya sasa.
Iringa. Watanzania wametakiwa kutembelea kwenye makumbusho ili kujua historia za mababu zinazoweza kuwa tiba kwenye maisha ya sasa yaliyojaa changamoto.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Boma na kiongozi wa wadau wa Utalii wanaoshiriki maonyesho ya Karibu Kusini, Jimson Sanga amesema yapo maswali mengi yanayoweza kujibiwa kwa kutembelea maeneo hayo.
Akitoa mfano, Sanga amesema kwenye Makumbusho ya Boma wamehifadhi simulizi za mababu kuhusu uwepo wa nyoka wa vichwa kwenye vyanzo vya maji lengo likiwa kutunza mazingira.
"Kwa hiyo ukija Boma utajua historia ya Mkwawa na Mazingira yaliyokuwa yanamzunguka na utajua historia ya mababu na namna walivyoishi kwenye jamii yao, tutembelee vivutio vya Utalii," amesema Sanga.
Amesema vipo vivutio vingi ndani ya Mkoa wa Iringa vinavyoweza kusaidia katika kukuza uchumi.
Awali, baadhi ya wadau wa Utalii walisema ipo haja kwa Serikali na taasisi zinazo jihusisha na masuala ya utalii kuwa na mkakati wa kutangaza vivutio vilivyo kwenye maeneo yao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU), Dk Isdory Minani amesema wanaweza kuandaa vipeperushi na kuvisambaza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Taasisi za elimu ya juu.
"Ukiingia hoteli unakutana na matangazo mengine tu, kule watu wakutane na vipeperushi vya Utalii, leteni hata vyuoni ni taasisi zinapokea watu wengi," amesema Minami
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema wataendelea kuhamasisha na kuona Watanzania wanajua vivutio vinavyo wazunguka.