Wataka Kiswahili kuwaunganisha Waafrika

Muktasari:
- Julai 7, mwaka huu, dunia itaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani, huku viongozi mbalimbali duniani wakitaka lugha hiyo iwe kiungo cha Waafrika na dunia.
Japan. Viongozi wa mataifa mbalimbali wameeleza umuhimu wa kukua na kuenea kwa Kiswahili, wakisema ndiyo lugha itakayowaunganisha Waafrika na mataifa mengine duniani.
Kwa mujibu wa viongozi hao, ukuaji wa kasi wa Kiswahili unaonyesha matumaini kuwa lugha hiyo itakuwa kiungo cha kibiashara na uchumi kati ya Waafrika na mataifa mengine.
Viongozi hao wamesema hayo kwa nyakati tofauti jana, Julai 4, 2025 walipotembelea Banda la Tanzania katika Maonyesho ya Biashara ya Dunia (Expo 2025), Osaka nchini Japan.
Akiwa katika banda hilo, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Prudence Sebahizi, ameeleza kufurahishwa na namna Kiswahili kilivyopewa nafasi katika maonesho hayo ya dunia.
Hatua hiyo, amesema, inafanya lugha hiyo kuwa nyenzo muhimu ya kuwaunganisha Waafrika katika juhudi za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

"Lugha ya Kiswahili inakidhi kwa matumizi ya Waafrika," amesema, huku akisisitiza umuhimu wa lugha hiyo kuendelea kupewa nafasi zaidi duniani.
Sambamba na Sebahizi, viongozi wengine waliotembelea banda hilo ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Japani, Koichiro Gemba, na Mfalme wa Lesotho, Letsie III, kila mmoja akieleza umuhimu wa Kiswahili na utamaduni wa Mtanzania.
"Hakika nimevutiwa kwa kiasi kikubwa na lugha ya Kiswahili na utamaduni kupata nafasi katika maonyesho haya ya dunia yenye hadhi kubwa," amesema Koichiro.
Viongozi hao pia walishuhudia vivutio vya kitamaduni kama mavazi ya jadi, sanaa za mikono, bidhaa zikiwemo kahawa ya Kilimanjaro, madini ya Tanzanite, viungo vya asili vya Zanzibar na machapisho mbalimbali ya Kiswahili, ikiwemo Kamusi Kuu ya Kiswahili kutoka Bakita.
Ushiriki huu wa Tanzania katika maonyesho hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za kuitangaza lugha ya Kiswahili kama urithi wa Afrika na dunia, sambamba na utamaduni wake tajiri, ili kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kuvutia wawekezaji, watalii na washirika wa maendeleo kupitia nguvu ya lugha na utambulisho wa kitaifa.

Kilele cha Wiki ya Utamaduni na Kiswahili katika maonyesho hayo kitafanyika Julai 7, mwaka huu, tarehe ambayo ni Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, kikihusisha utoaji wa vyeti na tuzo mbalimbali kwa wadau walioshiriki kukikuza, kukieneza na kukiendeleza Kiswahili nchini Japan.