Watanzania waibuka washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi 2024

Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza lugha ya Kiswahli kwa kuwa, kinatumika katika nchi nyingi za Kiafrika na baadhi ya nchi za ulaya
Dar es Salaam. Watanzania wameibuka washindi katika mashindano ya tisa ya Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kupitia miswada yao ya mashindano hayo ya mwaka 2024.
Tuzo hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015 na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma Wa Ngugi mwaka 2014 ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na kuhimiza tafsiri kutoka lugha hizo, inafadhiliwa na Kampuni ya Safal Group kupitia Alaf-Tanzania na Mabati Rolling Mills-Kenya.
Mshindi wa kwanza katika kipengele cha Riwaya ni Mayasa Abdalla (Mtanzania) alijinyakulia Dola 5000 za Marekani kwa kuwasilisha muswada ujulikanao kama ‘Kitanzi cha Mauti.’
Mshindi wa pili katika kipengele hicho ni Ali Othman Masoud (Mtanzania) aliyewasilisha muswada wa ‘Nyaraka za Wafu’ huku akipata Dola 2,500 za Marekani.
Katika kipengele cha Ushairi, mshindi ni Bashiru Abdalla (Mtanzania) mwenye muswada ujulikanao kama ‘Bure Ghali’aliyepata zawadi ya Dola 5000 za Marekani huku Mohamed Idrisa (Mtanzania) akishika nafasi ya pili kupitia mswada wake wa ‘Laana ya Uovu’ na kujipatia Dola2,500 za Marekani.
Mshiriki kutoka Kenya, Edwin Omindu alitangazwa mshindi wa kipengele cha Hadithi Fupi kupitia muswada wake wa ‘Mungu Hadanganywi’ huku aki-zawadiwa kitita cha Dola2,500 za Marekani.
Akizungumza katika hafla hiyo ya tuzo iliyofanyika katika Chuo Kikuu Dar es Salaam leo Alhamisi Julai 3, 2025, Waziri wa Utamaduni, Habari, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ametoa pongezi kwa washindi wote kwa kazi nzuri na kuipa kongole Safal Group kwa kuwa mstari wa mbele katika kukienzi Kiswahili mwaka hadi mwaka.
“Mashindano haya yamekuwa maarufu na kuzidi kuvutia washiriki wengi wakiwemo baadhi kutoka katika mabara mengine kutokana na umuhimu wa lugha hii ya Kiswahili ambayo ni tunu yetu kwa hivyo lazi-ma tujivunie na tukienzi ipasavyo,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza lugha ya Kiswahli kwa kuwa, kinatumika katika nchi nyingi za Kiafrika na baadhi ya nchi za ulaya wanakifundisha vyuoni ambayo ni fursa nzuri ya ajira kwa Watanzania.
Pia, amepongeza Mkuki na Nyota Publishers na Africa Poetry Book Fund ambao ni wachapishaji wa miswada iliyoshinda, huku akitoa wito kwa mashirika mengine yajitokeze kuunga mkono jitihada hizi za kukienzi Kiswahili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Alaf Tanzania, Ashish Mistry amesema Kampuni ya Safal Group ambayo ni kampuni mama ya Alaf Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya, imeendelea kudhamini tuzo hizo kutokana na ukuajia wake mwaka hadi mwaka na umuhimu wa Kiswahili katika kuunganisha Bara la Afrika.
Mwenyekiti wa majaji wa mashindano ya mwaka 2024, Dk Salma Hamad wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) amesema, “miswada ilikuwa mingi, hata hivyo, tumeburudika vya kutosha kwa sababu tumesoma kazi zilizoandikwa na kusukwa kiubunifu na tumejifunza kwamba kuna hazina kubwa ya vipaji vya uandishi wa fasihi ya kiswahili. Vikiendelezwa fasihi ya Kiswahili haitafilisika.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya tuzo hizo, Abdilatif Abdalla, amesema: “Ni jambo la kufurahisha mno kuona tangu mashindano yalipoan-zishwa mwaka 2015, bado tuzo hizo zinaendelea kuwavutia washiriki kutoka nchi mbalimbali na kwa idadi kubwa. Pia, kiwango cha ubora wa miswada inayoshindanishwa kinaongezeka kila mwaka na kuitajirisha Fasihi ya Kiswahili.”