Altezza Travel yashinda tuzo ya kampuni bora ya utalii Tanzania

Dar es Salaam. Kampuni ya Altezza Travel yenye makao yake mkoani Kilimanjaro imeibuka kidedea kwa mara ya pili mfululizo baada ya kutangazwa kuwa Kampuni Bora ya Utalii Tanzania katika hafla ya Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards 2025) kwa ukanda wa Afrika na Bahari ya Hindi, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Sherehe hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Jahari Rotana, ilikusanya wadau zaidi ya 500 kutoka mataifa 39 ya Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa hafla hiyo kubwa tangu mwaka 2016.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Msimamizi wa Mradi wa Altezza Travel, Dickson Muganda amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za pamoja za timu yao na dhamira ya dhati ya kulinda mazingira, kuendeleza jamii na kutoa huduma bora kwa watalii.
“Tunaendelea kuandaa safari salama na kusaidia miradi ya uendelevu. Mwaka jana tulipata Cheti cha Travelife, mojawapo ya vyeti vya juu kabisa vya kimazingira duniani. Hadi sasa, ni kampuni tano tu Tanzania zenye cheti hicho, na Altezza ni kubwa zaidi kati yao,” amesema Dickson.
Kwa mujibu wa Muganda, Altezza imepanga kupanua vifaa vyake, kuongeza magari ya safari, na kujenga nafasi zaidi za ajira ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mishahara bora kwa wafanyakazi. Pia kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi ya uhifadhi kama kuondoa mitego ya wanyama katika Hifadhi ya Serengeti, upandaji wa miti, na kusaidia TANAPA kwa vifaa vya kuzima moto.
Katika hatua nyingine, mwanachama wa timu ya Altezza anayehusika na kuhifadhi nafasi, Irene, ameeleza kuwa mafanikio ya kampuni hiyo ni mfano halisi wa jinsi utalii unavyoweza kuchochea maendeleo ya watu na jamii kwa ujumla.
“Kila mwaka maswali kutoka kwa watalii wanaotaka kuja Tanzania yanaongezeka. Watu wengi wanafaidika, lakini ni wajibu wetu kuhakikisha tunalinda urithi wetu wa asili,” amesema Irene.
Mbali na Altezza, hifadhi kadhaa za Taifa ziliibuka na tuzo mbalimbali zikiwemo Serengeti, Kilimanjaro, Ruaha na Nyerere, jambo linaloonesha mafanikio ya mkakati wa utalii na uhifadhi nchini.
Kadiri jioni ilivyokolea jijini Dar es Salaam, taswira ya Tanzania kama kinara wa utalii barani Afrika iliendelea kung'aa, huku wengi wakiamini kuwa ushindi wa Altezza ni ishara ya kilele cha mafanikio makubwa yanayoweza kufikiwa kupitia weledi, maono na uzalendo katika sekta ya utalii.