Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wa nchi 25 Afrika wakutana Tanzania

Muktasari:

Warsha hiyo imezinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, ambaye amesema mkutano huo ni hatua muhimu kuelekea kutokomeza kabisa ugonjwa wa PPR ifikapo mwaka 2030.

Dar es Salaam. Zaidi ya wataalamu 100 wa afya ya wanyama na wadau kutoka nchi 25 za Afrika wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya warsha ya siku tano yenye lengo la kuandaa miongozo ya pamoja ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi, kondoo - Peste des Petits Ruminants (PPR).

Warsha hiyo imezinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, ambaye amesema mkutano huo ni hatua muhimu kuelekea kutokomeza kabisa ugonjwa wa PPR ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), ugonjwa wa Peste des Petits Ruminants (PPR) huathiri zaidi ya kondoo na mbuzi milioni 330 barani Afrika, na husababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 2.1 kila mwaka.

Ugonjwa huu una uwezo wa kuua hadi asilimia 90 ya wanyama walioambukizwa kwa mara ya kwanza. Nchini Tanzania, mlipuko wa mwaka 2016 uliua zaidi ya wanyama 12,000.

Hayo yakijiri jijini Dar es Salaam, jana Juni 16,2025 akiwa ziarani mkoani Simiyu, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua  kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo, itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu hadi 2029.

Akitoa taarifa ya kampeni hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashantu Kijaji alisema Serikali imetenga Sh216 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Alisema Serikali imetoa Sh19.2 bilioni kwa  mwaka huu wa kwanza wa utekelezaji awamu ya kwanza ya chanjo na utambuzi.

Profesa Shemdoe amesema kuwepo kwa miongozo ya pamoja ya chanjo kutaziwezesha nchi za Afrika kufanya kampeni za chanjo kwa wakati mmoja, kuboresha ubora wa chanjo, na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa.

“Kuandaa viwango vya chanjo ya PPR kwa Afrika nzima ni hatua ya msingi. Kwa kuoanisha sera na taratibu za kitaifa, tunaweza kuongeza ufanisi wa kampeni za chanjo, kudumisha ubora wa chanjo, na kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa,” amesema Prof Shemdoe.

Ameongeza kuwa vita dhidi ya PPR inahitaji mbinu shirikishi inayojumuisha chanjo, ufuatiliaji madhubuti na huduma bora za mifugo. Pia ameeleza kuwa miongozo hiyo itaendana na viwango vya kimataifa vya afya na biashara.

“Kwa kutumia mfumo mmoja, tunaweza kuhakikisha chanjo na bidhaa za mifugo zinafuatilia ubora na zinatambulika kimataifa. Hili litafungua fursa kwa Tanzania kuuza nyama katika soko la dunia na kushindana ndani ya eneo la biashara huru la Afrika (AfCFTA) na kwingineko,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Umoja wa Afrika cha Chanjo za Mifugo (AU-PANVAC), Dk Charles Bodjo, amesema viwango vya pamoja vitahakikisha ubora wa chanjo unadhibitiwa kote Afrika, jambo litakalosaidia kuimarisha afya ya mifugo.

“Miongozo hii ya pamoja itahakikisha chanjo zinakidhi viwango thabiti vya ubora katika bara zima. Hii itaongeza uwezo wetu wa kugundua na kudhibiti magonjwa ya mifugo, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa mamlaka za udhibiti,” amesema Dk Bodjo.

Ameongeza mbinu hiyo ya ushirikiano itawezesha watengenezaji wa chanjo na taasisi za mifugo kubadilishana taarifa kwa urahisi na kutambua haraka chanjo zisizo na ubora unaohitajika.

“PPR ni tishio kubwa kwa usalama wa chakula na maisha ya vijijini barani Afrika, ambapo mamilioni ya watu hutegemea kondoo na mbuzi kwa kipato na lishe. Mpango wa Afrika wa Kutokomeza PPR ni sehemu ya juhudi za kimataifa kuondoa kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030,” ameongeza.

Warsha hiyo inalenga kutoa mfumo wa pamoja wa mwongozo ambao utasaidia nchi zote za Afrika katika mapambano dhidi ya PPR, huku pia ukichangia katika kuboresha huduma za mifugo na uchumi wa mifugo barani kote.

Meneja wa Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), Dk Charles Mayenga amesema Tanzania tayari imetengeneza aina saba za chanjo za mifugo na inaendelea kufanya tafiti zaidi kwa lengo la kudhibiti magonjwa ya mifugo ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuna juhudi zinazoendelea kuandaa mwongozo wa pamoja wa usajili wa chanjo ya PPR, utakaorahisisha taratibu za kupata kibali cha chanjo hiyo katika nchi mbalimbali barani Afrika.

“Lengo la kuwa na mwongozo mmoja wa usajili ni kuhakikisha matumizi ya chanjo yanakuwa sawia katika bara zima, jambo linalosaidia Afrika kutimiza malengo ya kimataifa ya kutokomeza PPR ifikapo mwaka 2030,” amesema.

Dk Mayenga pia ametaja changamoto zinazokwamisha Tanzania kuuza chanjo na bidhaa za mifugo nje ya nchi, zikiwemo milipuko ya magonjwa na kampeni hafifu za chanjo ambazo hazitoshi kuwahakikishia wanunuzi wa kimataifa kuwa bidhaa hizo ni salama.

“Kwa mwongozo huu wa pamoja, tunalenga kuzalisha chanjo bora na salama zitakazofungua milango ya soko la kimataifa,” amesema.

Miongoni mwa magonjwa 13 ya mifugo yanayozuia biashara barani Afrika, PPR imepewa kipaumbele katika warsha hii kwa lengo la kuhakikisha inaondolewa kabisa.