Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NeST yatajwa kuleta matunda, Serikali yatoa maagizo

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akizungumza kwa niaba ya Dk Mwigulu Nchemba, kwenye kongamano la tisa la ununuzi wa umma lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA)

Muktasari:

Amesema mfumo huo wa kielektroniki wa manunuzi ya umma (NeST), umesaidia mapambano dhidi ya rushwa na udanganyifu katika ununuzi wa umma pamoja na kutoa fursa kubwa kwa watoa huduma mbalimbali kuweza kufanya kazi na Serikali kwa ufanisi, uwazi, uwajibikaji na weledi

Arusha. Matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), yametajwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuleta thamani ya fedha katika manunuzi pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.

Mafanikio mengine yaliyochangiwa na mfumo huo yanatajwa kuwa ni pamoja na uboreshaji wa mazingira na kupungua kwa gharama za kufanya manunuzi kwa wazabuni na Serikali.

Kauli hiyo imetolewa Juni 14, 2025 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima kwa niaba ya Dk Mwigulu Nchemba, katika kongamano la tisa la ununuzi wa umma lililoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA).


Amesema kuwa Tanzania kama nchi nyingi duniani imetambua umuhimu wa matumizi ya mifumo ya Tehama katika ununuzi wa umma, kwani mifumo hiyo inaondoa changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwenye sekta hiyo.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliamua kujenga mfumo huo ambapo baada ya kuanza kutumika umesaidia kupunguza matumizi ya karatasi, kuongezeka kwa kasi ya manunuzi na kupungua kwa makosa katika ununuzi na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.


“Mfumo wa NeST umeongeza uwazi, uwajibikaji na kuleta thamani ya fedha katika manunuzi ni wazi mfumo huo umeleta faida nyingine nyingi kama vile kuimarisha utawala bora na kuongeza wigo wa ununuzi,”amesema.

Ameongeza, “mafanikio ya PPRA na NeST yamechangiwa na juhudi za Serikali katika kusimamia misingi imara na thabiti ya utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa na udanganyifu katika ununuzi wa umma, mfumo unatoa fursa kubwa kwa watoa huduma mbalimbali kuweza kufanya kazi na Serikali kwa ufanisi, uwazi, uwajibikaji na weledi.

Kutokana na faida hizo Waziri huyo aliagiza taasisi za ununuzi  nchini kutenga asilimia ya ununuzi wao wa mwaka kwa ajili ya kampuni za wazawa na makundi maalumu kama zilivyokusudiwa na kusimamia matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali ununuzi wa umma nchini.

Pia ameagiza halmashauri zote nchini  kusaidia kuibua makundi maalumu ya kijamii katika maeneo yao ambayo yatajipatia fursa zilizotengwa na Serikali kwa ajili yao.

Amesema ni muhimu taasisi za ununuzi wa umma kujitahidi kukuza ununuzi endelevu ambavyo vitaimarisha usawa wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi na uendelevu wa kimazingira, kwa kutambua kuwa wanapotumia fedha za umma kununua bidhaa, huduma au miradi mbalimbali wanapaswa kufahamu hitaji la maendeleo endelevu kwa manufaa ya muda mrefu wa wananchi.

Mmoja wa maofisa ununuzi hao, Julius Solomon amesema mfumo huo umewezesha kupunguza mianya ya rushwa kwa baadhi ya maofisa waliokuwa hawazingatii mfumo umewarahisishia utendaji kazi kutokana na kila kitu kufanyika kwa njia ya mtandao.




Naye Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba amesema lengo la kongamano hilo lenye washiriki zaidi ya 1,000 ni kutoa fursa na kujadiliana masuala mbalimbali yenye nia ya kuleta tija, kuboresha sekta ya ununuzi wa umma nchini ambapo mada 16 zitajadiliwa.

Amesema hadi kufikia Juni 11, 2025, wazabuni 38,163 waliidhinishwa na kusajiliwa, kati ya hao 36,377 wa ndani na 1,786 wa kutoka nje ya nchi huku taasisi za nunuzi 61,415 zikiwemo kuu na ngazi za chini za serikali za mitaa zimesajiliwa NeST zikiwa na jumla ya watumiaji 131,202.



Mkurugenzi huyo amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 hadi kufika Juni 11,2025 taasisi za ununuzi 20,954 zilitangaza mipango ya ununuzi ya mwaka yenye thamani ya zaidi ya Sh30 trilioni na zabuni 258,787 zimetangazwa huku zabuni 61,174 zikifunguliwa.

"Jumla ya tuzo za zabuni 140,494 zilitolewa zenye thamani ya Sh8.6 trilioni na taasisi nunuzi 1,701 pamoja na shule na vituo vya afya 59,714 zinatumia mfumo na kuchakata zabuni mbalimbali ndani ya mfumo,"amesema.