Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utekelezaji sheria PPRA kupunguza ukosefu wa ajira

Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa umma, Dennis Simba akizungumza katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari   hawapo pichani, jijini Dar es Salam.

Muktasari:

  • Sheria ya PPRA inazitaka taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi wa umma (tenda za Serikali) kwa ajili ya makundi maalumu ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, imeelezwa utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma (PPRA) ya mwaka 2023 unaweza kuwa msaada katika kuitatua.

Sheria hiyo inazitaka taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi wa umma (tenda za Serikali) kwa ajili ya makundi maalumu.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba amesema hayo leo, Mei 12, 2025 jijini Dar es Salaam, katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari akizungumzia maendeleo ya ujenzi na matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Umma Tanzania (NeST). Mfumo huo wa kidijitali ni ishara ya maendeleo, uwazi, uwajibikaji na ufanisi.

Simba amesema makundi hayo maalumu ni wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu, ambao Serikali inalenga kuwawezesha kujiinua kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kupata sehemu ya fursa za tenda za Serikali.

Mfumo huo ulianza kutumika rasmi Julai mosi, 2023 na ulizinduliwa Septemba 9, 2024 wakati wa kongamano la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki lililofanyika mkoani Arusha.

Tangu kuanza kwa mfumo wa NeST, vikundi 85 vya vijana vimepata zabuni zenye thamani ya Sh3.1 bilioni, vikundi 95 vya wanawake vimepata zabuni zenye thamani ya Sh5.6 bilioni, vikundi vitatu vya watu wenye ulemavu vilipata zabuni 12 zenye thamani ya Sh138.5 milioni na vikundi vitano vya wazee vilipata zabuni 17 zenye thamani ya Sh800.6 milioni.

Katika hatua nyingine, Simba amesema mfumo unawezesha zabuni katika ngazi za chini za Serikali za Mitaa, zinazohusisha shule za sekondari na msingi, vituo vya afya, zahanati, kata, vijiji na mitaa.

Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa umma, Dennis Simba akizungumza katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari  jijini Dar es Salam.

“Ngazi hizi, tangu kuanza kutumika kwa moduli ya lower level (ngazi ya chini), zimeweka katika mfumo mipango ya ununuzi yenye thamani ya Sh1.5 trilioni yenye jumla ya zabuni 139,080. Jumla ya zabuni 122,937 zilitangazwa zenye thamani ya Sh947.1 bilioni. Zabuni 50,102 ziliweza kutolewa tuzo ya zabuni zenye thamani ya Sh476.8 bilioni,” amesema.

Katika kuziwezesha ngazi za chini, amesema mamlaka imejenga aplikesheni ya simu inayotumiwa na taasisi nunuzi katika ngazi za shule na vituo vya afya, vijiji/mitaa na kata.

“Vilevile, aplikesheni hii inatumiwa na wazabuni katika kupata taarifa na kuomba zabuni. Lengo ni kurahisisha zoezi la ununuzi wa umma mahali popote ambapo mtumiaji alipo,” amesema.

Simba amesema hadi Machi, 2025 wazabuni 34,678 waliidhinishwa na kusajiliwa. Kati ya hao, 33,114 ni wazabuni wa ndani na 1,564 ni kutoka nje ya nchi.

Amesema taasisi nunuzi 57,993 zimesajiliwa NeST zikiwa na jumla ya watumiaji 117,900 waliopo kwenye mfumo. Kati ya hizo, amesema kuna taasisi kuu na kasimiwa 1,215 na taasisi za ngazi za chini za Serikali za Mitaa 56,778. Pia, watumiaji 53,584 wamesajiliwa kama wasimamizi wa wazabuni.

Amesema shule, vituo vya afya, zahanati, kata, vijiji, mitaa 56,778 vimesajiliwa kwenye mfumo na kuanza matumizi.

NeST umeunganishwa na mifumo zaidi ya 20 ya Serikali ili kufanikisha uhakiki na uhalisi wa taarifa na kubadilishana taarifa na mifumo mingine pale inapobidi.

“Pamoja na hayo, ni kupunguza kwa kiasi kikubwa upakiaji wa nyaraka zinazohitajika kwenye usajili na michakato ya ununuzi wa umma,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan mara kadhaa amekuwa akiagiza mifumo yote ndani ya Serikali isomane, akiagiza makatibu wakuu wa wizara kuhakikisha wanasimamia utekelezwaji wake.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bakari Machumu amepongeza hatua iliyofikiwa kwa mifumo kusomana, akisema ni hatua kubwa ya kupunguza usumbufu na kuleta ufanisi.

“Kelele za kusomana kwa mifumo hii leo imeonekana kwenye ununuzi na ni wazi kuna hitaji la waandishi wa habari kujifunza na kuelewa sheria, kanuni na taratibu ili kuelimisha jamii na kuona fursa ili waweze kuzitumia,” amesema.