Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira amjibu Maalim Seif

Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira 

Muktasari:

Wasira alikuwa anazungumzia kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kibandamaiti, Zanzibar na kusema kuna mpango wa siri wa kubadilisha Sheria ya Kura ya Maoni ili Rasimu itakayopitishwa na Bunge la Katiba ipitishwe na wananchi “kwa mteremko” kwa kuruhusu wakazi wa Tanzania bara kupiga kura Zanzibar.

Dodoma/Zanzibar. Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira amesema kauli zinazotoka kinywani mwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, haziendani na hadhi yake.

Wasira alikuwa anazungumzia kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kibandamaiti, Zanzibar na kusema kuna mpango wa siri wa kubadilisha Sheria ya Kura ya Maoni ili Rasimu itakayopitishwa na Bunge la Katiba ipitishwe na wananchi “kwa mteremko” kwa kuruhusu wakazi wa Tanzania bara kupiga kura Zanzibar.

Maalim Seif alisema kitendo hicho kinakwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imeeleza wazi kuwa lazima kupatikane theluthi mbili ya Wazanzibari na Watanzania Bara katika kupitisha Katiba na lazima Rasimu hiyo iungwe mkono na zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wa upande mbili za Muungano.

“Kitendo cha kukarabati sheria ili kuruhusu Watanzania Bara kupiga kura ya maoni wakiwa Zanzibar ni kinyume na sheria, hiyo ni sawa na kuamua kujitekenya na kucheka mwenyewe,” alisema Maalim Seif.

Kutokana na kauli hiyo, Wasira alisema kumjibu kiongozi huyo ambaye alisema: ‘amewekwa ndani ya Serikali inayoaminika’ ni kupoteza muda kwa kuwa kauli zake siku zote hazina mashiko na zimejengwa katika misingi ya kubomoa.

“Yule ni Makamu wa Rais katika Serikali yetu, asingepaswa kutoa kauli kama hiyo lakini anapozungumza wakati mwingine hata huwezi kumwelewa anachokisema maana huamua kukurupuka,” alisema Wasira.

Bila kuingia kwenye hoja ya Maalim Seif, Wasira alisema kiwango alichofikia Makamu huyo wa Rais, alipaswa kuwa na busara zaidi kwa kuwa ni kiongozi anayeaminiwa.

Akizungumzia suala la Wabara kupiga kura kama Wazanzibari alisema: “hilo halipo na halitakuwapo, ukitaka njoo mle ndani ya kamati yangu namba sita na kamati zingine halafu nianze kuwaita mmoja na uwapige picha,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema katika kamati zote idadi ya Wazanzibari ni kubwa na kuwa haina shaka yoyote katika upigaji wa kura, theluthi mbili itapatikana tofauti na wengine wanavyosema.

Wasira alisema kauli zote ambazo zinatolewa na wanasiasa kwamba hakuna akidi ya kutosha kupitisha, hazina nafasi kwa wakati huu.

Katika mkutano huo, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF alisema Wazanzibari wenyewe ndiyo wenye mamlaka ya kuamua aina ipi ya muungano wanaoutaka na Katiba ya aina gani na kusisitiza kwamba kazi ya kudai mamlaka kamili ya Zanzibar ndiyo kwanza imeanza visiwani humo.

“Kuna watu wanasema kuwa suluhisho la Ukawa na Bunge la Katiba ufunguo wake anao Maalim Seif, si kweli kabisa. Suluhisho la jambo hilo wanalo Wazanzibari wenyewe ikiwamo kuamua hatima ya muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.

Kuhusu Ukawa kurejee bungeni kwa jitihada zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, alisema wajumbe kutoka CCM katika vikao hivyo hawakuwa na nia njema ya kuheshimu Rasimu ya Katiba na hivyo mazungumzo hayo kushindwa kupata mwafaka.