Mwanafunzi ajinyonga bwenini, Polisi yaanza uchunguzi

Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi wa eneo la Kigezi, Elly Maate mwili wa Kiconco umepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kabale kwa ajili ya uchunguzi
Uganda. Mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Solberg, iliyopo Manispaa ya Kabale nchini Uganda, Nikita Kiconco (21) amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ndani ya bweni la shule hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi wa eneo la Kigezi, Elly Maate mwili wa Kiconco tayari umepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kabale kwa ajili ya uchunguzi.
"Yadaiwa kuwa Siku ya Ijumaa Kuu, baadhi ya wanafunzi wa Solberg waliondoka kwenda likizo ya Pasaka, huku wanafunzi wapatao 60, akiwamo Kiconco, wakibaki shuleni.”
“Leo (Jumapili), wanafunzi waliondoka shule kwenda kusali katika Kanisa la Uganda, Nyabikoni, majira ya saa 4:30 asubuhi, lakini Kiconco na mwenzake mmoja walibaki shuleni kwenye mabweni yao. Inasemekana Kiconco hakuwa anaendelea vizuri kiafya na alikuwa akitumia dawa kwa ajili ya hali isiyojulikana," amesema Maate.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Daily Monitor, mkuu wa shule hiyo, Denis Tusiime, aliieleza polisi kuwa wanafunzi waliporudi kutoka kanisani saa 7 mchana, walimkuta Kiconco amefariki, akiwa amejinyonga kwa kamba iliyofungwa kwenye mbao moja ya paa la bweni.
"Wanafunzi walipiga kelele za kuomba msaada, jambo lililomtia hofu mlezi wa mabweni ambaye alinijulisha, na mimi mara moja niliripoti tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kabale," amesema Tusiime.
"Baada ya kupokea taarifa hizo, polisi walifika katika eneo hilo lilipotokea tukio kwa ajili ya uchunguzi kisha mwili uliondolewa eneo la tukio na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kabale kwa uchunguzi zaidi," amesema Maate.
Kifo cha Kiconco kinatokea ikiwa ni miezi miwili imepita baada ya mwanafunzi mwingine kukutwa amefariki kwa kujinyonga katika bweni la Shule ya Sekondari ya Seeta.
Imeandaliwa na Mariam Mbwana