Hivi ndivyo dunia inavyomlilia Papa Francis

Muktasari:
- Papa Francis amekuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, amefariki dunia leo Jumatatu akiwa na umri wa miaka 88.
Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali pamoja na watu mashuhuri duniani wameendelea kuomboleza msiba wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis aliyefariki dunia leo Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88.
Kwa mujibu wa mtandao wa kijamii wa Vatican News, Papa Francis amefariki dunia akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta. Kiongozi huyo wa Vatican alizaliwa Desemba 17, 1936 jijini Buenos Aires, Argentina.
Viongozi hao wametumia akaunti zao za mtandao wa X kumzungumzia Papa Francis pamoja na kuweka picha ambazo walipiga naye kwenye matukio tofauti walipokutana naye.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema ni msiba kwa Wakatoliki wote pamoja na ulimwengu kwa ujumla.
“Kutoka Buenos Aires hadi Roma, Papa Francis alitaka Kanisa lilete furaha na matumaini kwa maskini na liwaunganishe wanadamu wenyewe kwa wenyewe pamoja na mazingira. Tumaini kama hilo na lihuishwe daima zaidi yake,” ameandika Rais huyo.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole huku akisema dunia imempoteza kiongozi wa kiroho aliyeacha alama ya amani, upendo na maendeleo ya watu.
“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa waumini wote wa Kanisa Katoliki hapa nchini na duniani kote,” amesema Rais Samia.
Amesema mchango wa Papa Francisko katika kudumisha amani na kuhimiza maendeleo ya binadamu utabaki kuwa kumbukumbu ya kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema Wakatoliki na watu wa imani zote wameguswa na kifo cha kiongozi huyo wa kiroho ambaye katika uhai wake alijitahidi kuunganisha ubinadamu na kutamani kuona dunia inayotawaliwa na maadili yenye misingi ya utu.
Amesema Papa akiwa kiongozi wa Kanisa Katoliki, alisimamia mtazamo wa dunia unaojumuisha usawa, mshikamano, huruma kwa watu na makundi yaliyosahaulika, sambamba na uwajibikaji na utunzaji endelevu wa mazingira ya asili.
“Maisha yake ya kipekee na safari yake ya kuwa mkuu wa Kanisa Katoliki yalijaa unyenyekevu mkubwa na dhamira ya dhati ya kulifanya Kanisa na dunia kuwa sehemu bora kwa ajili ya wanadamu wote.
“Kifo chake kimekuja muda mfupi baada ya Pasaka, kipindi cha sala na tafakari na hivyo kuendelea kuongeza uzito wa kipindi hiki kwa kuwakutanisha waumini na jumuiya ya kimataifa kwa pamoja, ili kutafakari juu ya maisha na urithi aliouacha Baba Mtakatifu.”

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema kufuatia kifo hicho, Kanisa Katoliki na ulimwengu umepoteza mtetezi wa wanyonge, mpatanishi na mtu mwenye moyo mkunjufu.
“Nilithamini sana maoni yake wazi kuhusu changamoto zinazotukabili. Huruma zangu ziende kwa jumuiya ya kidini duniani kote,” ameandika Scholz kwenye mitandao yake ya kijamii.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amesema, mamilioni ya watu kote ulimwenguni wanaomboleza kifo cha Papa Francis ambaye maisha yake yalikuwa yametolewa na Mungu kwa watu na kwa Kanisa.
“Alijua jinsi ya kutoa tumaini, kupunguza mateso kupitia maombi, na kukuza umoja. Alisali kwa ajili ya amani katika Ukrainia na kwa ajili ya Waukraine. Tunahuzunika pamoja na Wakatoliki na Wakristo wote waliomtegemea Papa kwa msaada wa kiroho,” ameandika.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema amesikitika kusikia kifo hicho kwa kuwa juhudi zake kubwa zilikuwa ni kuwa na ulimwengu wa haki kwa wote.
“Juhudi zake zisizochoka zitaacha urithi wa kudumu. Kwa niaba ya watu wa Uingereza, ninatoa rambirambi zangu za dhati kwa Kanisa Katoliki.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance amesema salamu zake za rambirambi ziwaendee mamilioni ya Wakristo duniani kote waliompenda.
“Nilifurahi kumuona jana, ingawa ni wazi alikuwa mgonjwa sana. Lakini nitamkumbuka kila wakati kwa hotuba iliyo hapa chini aliyotoa katika siku za mapema sana za Uviko19,” amesema Vance.
Aliyekuwa Rais wa Marekani, Joe Biden amesema kifo cha Papa ni huzuni kwani alikuwa wa kipekee tofauti na hata waliomtangulia. Amesema Papa atakumbukwa kama mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa zaidi wa kizazi chetu, “nilipata bahati ya kumfahamu.”
“Kwa miongo kadhaa, alihudumia wanyonge nchini Argentina, na dhamira yake ya kuwahudumia maskini haikuwahi kuyumba. Akiwa Papa, alikuwa mchungaji mwenye upendo na alifungua milango kwa imani mbalimbali duniani.
“Alituhimiza kupigania amani na kulinda dunia yetu dhidi ya janga la mabadiliko ya tabianchi. Alisimama kwa ajili ya wale wasio na sauti wala mamlaka. Alihakikisha kila mmoja anakaribishwa na kuonekana na Kanisa. Alipigania usawa na kutokomeza umaskini na mateso duniani kote alikuwa Papa wa watu wote” amesema Biden.
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amesema Papa alikuwa mtu mnyenyekevu na mwenye huruma, aliyeongoza Kanisa Katoliki kwa kielelezo.

“Tunaungana na Wakatoliki na Wakristo wenzetu duniani kote katika maombolezo. Roho yake ipumzike kwa amani ya milele.”
Rais wa Kenya, William Ruto amesema Kenya inaungana na Kanisa Katoliki na jumuiya ya Wakristo duniani kote katika kuomboleza kifo cha Papa Francis.
“Hii ni pigo kubwa kwa waumini wa Kikatoliki na ulimwengu wa Kikristo. Baba Mtakatifu atakumbukwa kwa maisha ya kujitolea kumtumikia Bwana, Kanisa na binadamu. Alionyesha mfano wa uongozi wa mtumishi kupitia unyenyekevu wake, kujitolea kwake bila kuyumbayumba kwa ushirikishwaji na haki, na huruma yake ya kina kwa maskini na walio hatarini.”

Naye, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema Papa Francis atakumbukwa daima kama taa ya huruma, unyenyekevu, na ujasiri wa kiroho kwa mamilioni ya watu duniani kote.
“Tangu akiwa kijana, alijitolea kwa dhati kutimiza maadili ya Bwana Yesu Kristo. Aliwahudumia maskini na wanyonge kwa moyo wa kujitoa. Kwa wale waliokuwa wakiteseka, alichochea tumaini jipya,” amesema Modi.