Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia aomboleza kifo cha Papa Francis

Muktasari:

  • Leo Jumatatu, Aprili 21, 2025, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Dunia, Papa Francisko amefariki dunia akiwa na miaka 88.

Dar/Mbeya. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameomboleza kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Dunia, Papa Francisko aliyefariki saa 1:35 asubuhi ya Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025.

Taarifa za kifo chake zimetangazwa na Kardinali Kevin Joseph Farrell, ambaye ni Camerlengo ambapo amesema: "Kaka na dada wapendwa ni kwa huzuni kubwa kwamba sina budi kutangaza kifo cha baba yetu Mtakatifu Francisko. Saa 1.35 asubuhi ya leo, Askofu wa Roma, Francisko, alirejea nyumbani kwa baba.”

Papa Francisko amefariki akiwa na miaka 88 kwenye  nyumba ya mtakatifu Marta, ambako ni makazi yake, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Vatican na viongozi mbalimbali duniani wameanza kutuma salamu za rambirambi.

Rais Samia ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kutoa salamu hizo akisema: “Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisko. Katika kipindi chote cha miaka 12 akiwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francisko ameishi maisha yake kama mwalimu na kiongozi aliyefundisha na kuhimiza ustawi na maendeleo ya watu pamoja na kudumisha amani.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa waumini wote wa Kanisa Katoliki hapa nchini na duniani kote. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.”

Naye Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ametuma salamu za pole kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), waumini wa kanisa hilo kutokana na kifo hicho.

"Muda huu nimepokea taarifa ya kusikitisha ya kifo cha Papa Francis naomba tusimame kwa dakika chache tumuombee, lakini pia nitoe pole kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa msiba huu mkubwa," amesema.

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson.

Dk Tulia amewataka viongozi wa Kanisa Katoliki na waumini wawe watulivu na  kuendelea kumuombea wakati tukisubiri taratibu nyingine.

"Huu ni msiba mkubwa niombe utulivu, lakini pia tuendelee kumuombea Papa Francis Mungu amlaze mahala pema," amesema Dk Tulia muda mfupi baada ya kupata taarifa ya msiba akiwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mradi wa kisima cha maji uliofanyika kwenye Kata ya Mwansekwa jijini Mbeya.