Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Warioba ashindilia msumari Katiba Mpya

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wakiwa katika vikao vya Bunge hilo , mjini Dodoma. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi wa Serikali kutegua kitendawili cha lini mchakato wa mabadiliko ya Katiba utahitimishwa ili Taifa liwe na utulivu.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amewataka viongozi wa Serikali kutegua kitendawili cha lini mchakato wa mabadiliko ya Katiba utahitimishwa ili Taifa liwe na utulivu.

Wito huo umekuja wakati kukiwa na shinikizo la kupatikana kwa Katiba mpya, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiweka msimamo wa kudai katiba hiyo na kusema hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa Katiba hiyo haitapatikana.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa msimamo wake Juni 28 mwaka huu, alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari na kusema kuwa suala la Katiba mpya lisubiri, ili apewe muda wa kujenga uchumi ambao alisema umeathiriwa na mlipuko wa ugonjwa wa corona (Covid-19).

Licha ya msimamo huo wa Serikali, vyama vya siasa na asasi za kiraia vimeendelea kushinikiza kufanyika kwa mchakato wa Katiba mpya kwa njia mbalimbali hasa mitandao ya kijamii na makongamano.

Akizungumza juzi katika hafla ya uzinduzi wa juzuu ya tatu ya Rai ya Jenerali, kitabu ambacho kimejumuisha makala za mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu alizoandika tangu mwaka 1996, Warioba ambaye pia ni Jaji mstaafu, alisema anashangaa kuona malumbano kuhusu Katiba kwa sababu nchi iliamua kuwa na mchakato wa mabadiliko ya Katiba na sheria ikatungwa.

Akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Jaji Warioba alisema mchakato huo ulianzishwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikaundwa, ikaenda kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya Katiba ambayo ilijadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba mpaka Katiba Pendekezwa ikapatikana.

“Kufuatana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kilichokuwa kimebaki ni kura ya maoni kwa Katiba Pendekezwa, hapo ndipo tulipoishia. Tulishindwa wakati ule kwa sababu Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisema isingeweza kuandaa kura ya maoni kwa sababu walikuwa wanaandaa uchaguzi mkuu,” alisema.

Jaji Warioba alisema pengine wakati huu kura ya maoni haiwezi kufanyika, kwa sababu kuna changamoto kadhaa likiwamo janga la maambukizi ya virusi vya corona na uchumi wa nchi kushuka kutokana na athari za ugonjwa huo.

Hata hivyo, alisema kilichobaki ni kukubaliana lini kura ya maoni ifanyike ili wananchi wajue wakati ambao kura hiyo itapigwa, jambo litakalochochea utulivu hapa nchini tofauti na hali iliyopo sasa.

“Rais ameomba muda, ni kweli, lakini muda gani? Nadhani ni juu ya viongozi kukubaliana ni lini hasa mchakato wa Katiba mpya utaendelezwa,” alisema Warioba huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria hafla hiyo.

Waziri mkuu huyo mstaafu alipendekeza kura ya maoni kufanyika sambamba na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Tunaweza kufanya kwamba tuvumilie mpaka mwaka 2024 wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tuunganishe. Wakati wananchi wanapiga kura, wapige na kura ya maoni.

“Haya yakifanyika, Taifa litatulia. Mimi sioni hili kama ni tatizo, naona ni rahisi kabisa. Ifike mahali tufanye uamuzi, tukifanya uamuzi nchi itatulia,” alisema Jaji Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema ni kweli Katiba Pendekezwa inatakiwa kufanyiwa marekebisho kadhaa, kwa sababu sheria inaitambua kama Katiba ya mwaka 2014 lakini haikupatikana mwaka ule, kwa hiyo itabidi ibadilishwe na kupitia nafasi hiyo mabadiliko mengine yanaweza kufanyika bila kuitisha Bunge Maalumu la Katiba.


Rais kukutana na wapinzani

Warioba alizungumzia umuhimu wa Rais Samia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili wajadiliane mambo mbalimbali kwa mustakabali wa Taifa, na kwamba bahati nzuri pande zote mbili zimeonyesha utayari katika hilo.

“Ushauri wangu, viongozi hawa wakutane, sio kwenda kupambana, waende kuzungumzia matatizo ya nchi; tunakabiliana vipi na janga la corona, wazungumzie suala la Katiba mpya, nini kifanyike? Tunainuaje uchumi wetu,” alisema.

Wakati huohuo, Warioba alisema anategemea kipindi hiki Taifa litaangalia utaratibu wa uchaguzi kwa sababu chaguzi zilizopita zilitawaliwa na mambo ambayo hayakuwahi kuwepo huko nyuma ikiwamo kuenguliwa kwa wagombea na mawakala kuzuiliwa vituoni.

Alisema rushwa ilitawala katika mchakato wa uteuzi wa wagombea, jambo ambalo halikukemewa na viongozi.

“Mimi nategemea kwenye uchaguzi ujao, suala la kuenguliwa kwa wagombea lisiwepo, suala la kuzuiliwa kwa mawakala lisiwepo na vitendo vya rushwa wakati wa uteuzi wa wagombea visiwepo,” alisisitiza Warioba.


Udini, ukanda na ukabila

Warioba alisema amekuwa akifuatilia mijadala mitandaoni na kuona masuala ya udini, ukabila na ukanda yamekuwa yakitawala mijadala hiyo, jambo linalohatarisha amani ya nchi hii.

Alisikitishwa kuona viongozi wakishindwa kukemea hali hiyo hadharani, kama alivyokuwa akifanya Mwalimu Julius Nyerere katika hotuba zake.

“Haya yanatokea sasa hayakemewi, sisi viongozi hatukemei. Ni mambo ambayo yatatugawa na yakitugawa hatutakuwa na amani,” alisema.

Aliongeza kuwa sasa umeongezeka ubaguzi wa kisiasa ambao umefikia hatua kwamba, mtu akiongea kitu, badala ya kuangalia hoja yake inaangaliwa kwamba ametoka chama gani. Alisema jambo hilo linaleta mgawanyiko kwa wananchi.

“Mimi nilifikiri, likitokea tatizo vyama vinaitana wanazungumza, lakini ikitokea tofauti kati yao yanakuwa ni malumbano, kisha inakuwa kazi ya polisi halafu tunaambiwa polisi walikuwa wanaleta amani.

“Polisi hawaleti amani, wanalinda amani lakini tunataka polisi walete amani. Amani inaletwa na jamii kama haitaki udini, ukabila na ukanda,” alisisitiza Jaji Warioba katika hotuba yake iliyodumu kwa takribani dakika 45.

Alisema ni vizuri kila mmoja akajua majukumu yake na polisi waachwe walinde amani badala ya kutakiwa kuleta amani.


Jenerali na Katiba

Jenerali Ulimwengu alisema kitabu chake kina makala ambazo zinajadili mahitaji ya Katiba mpya kwa muktadha wa wakati ule hasa baada ya Tume ya Jaji Francis Nyalali kupendekeza mabadiliko.

Alisema wakati huo CCM haikupenda uamuzi wa kuwa na vyama vingi ulioanzishwa mwaka 1992 na kwamba, wakati Mwalimu Nyerere anazungumza kwenye mkutano wa chama kutetea jambo hilo, ilisikika minong’ono ya chini huku wengine wakiguna japo hawakupaza sauti.

“Katiba peke yake haitoshi bali kuna uhitaji wa kuwa na watu wenye ukatiba ndani yao. Wapo walioandika katiba nzuri, lakini unakuta rais ndiyo anaongoza kwa kuvunja katiba,” alisema Jenerali.

Alisema mjadala wa Katiba uendelezwe kwa sababu ni haki na unatoa nafasi kwa wananchi kuifahamu Katiba yao na maudhui yaliyomo ndani yake.