Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wapendekeza ujumuishaji jinsia, afya ya uzazi kukabiliana mabadiliko ya tabianchi

Muktasari:

  • Athari za mabadiliko ya tabianchi zinagusa sekta ya afya ikiwemo kusababisha maradhi kama malaria, kuhara, utapiamlo pamoja na kukwamisha juhudi za huduma za afya baada ya majanga kama mafuriko.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiandaa mpango mkakati wa tatu wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC 3.0), wadau wamependekeza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na afya ya uzazi katika mpango huo.

Mapendekezo hayo yanakuja wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikigusa sekta ya afya ikiwemo kusababisha maradhi kama malaria, kuhara, utapiamlo pamoja na kukwamisha juhudi za huduma za afya baada ya majanga kama mafuriko.

Hayo yamebainishwa kwenye warsha ya siku mbili kuanza Juni 11, 2025 ya shirika lisilokuwa la kiserikali la CAN Tanzania iliyowakutanisha wadau hao pamoja na wawakilishi wa Serikali jijini Dar es Salaam.

Imeelezwa athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na ukame zinazowagusa moja kwa moja na kuwaletea changamoto makundi ya wanawake na wasichana.

Akizungumza na Mwananchi nje ya warsha hiyo, Msimamizi wa Miradi wa CAN Tanzania, Dk Mkama Manyama amesema athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo magonjwa zinapaswa kuandikwa kwenye utaratibu utakaokuwa rahisi kuwa na mkakati wa kuzitatua.

“Tumejadili namna mabadiliko haya yanavyoibua changamoto mpya za kiafya na mapendekezo tunawasilisha serikalini ili kama Taifa tunakuwa na mustakabali wa sasa na kizazi kijacho,” amesema Dk Manyama.

Katika warsha hiyo, Reebok Mnyigumba, Mratibu wa Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Afya kutoka CAN Tanzania, amewasilisha utafiti unaoonesha jinsi ongezeko la joto, vimbunga, mafuriko na ukame vinavyoathiri sekta ya afya ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya msingi katika maeneo yanayoathirika na janga la mabadiliko ya tabianchi.

“Kutokana na tafiti za kisayansi zilizofanyika nchini, mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ongezeko la magonjwa mbalimbali ikiwemo kuhara, malaria, dengue, na tatizo la lishe kutokana na athari zinazotokea kwenye sekta ya kilimo na mifumo ya vyakula.

“Pia majanga kama vile mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea katika baadhi ya maeneo kama vile Wilaya ya Kilwa yanaathiri mfumo wa utoaji wa huduma za afya msingi ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto kutokana na uharibifu wa miundombinu muhimu ikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya na  barabara,” ameeleza.

Akifafanua zaidi Budodi Walwa Ofisa afya kutoka Wizara ya Afya amesema walifanya tathimini kwa mwaka 2024 kwakuwa sekta hiyo ndiyo waathirika wakubwa pindi yanapotokea mabadiliko ya tabianchi ikiwemo upepo, mafuriko na ongezeko la magonjwa yanayoibuka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mwaka 2021 Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilisema uchafuzi wa hali ya hewa unasababisha vifo vya mapema (Premature death) karibu milioni saba kwa mwaka.

Amesema walifanya tathimini ya sekta ya afya kwa mwaka 2024 na kugundua mikoa kama Kigoma, Tabora na Katavi iliathirika na utapiamlo, kipindupindu na kuharisha baada ya mafuriko na athari kama ukame.

“Tunaendelea kumalizia kuhuisha mpango wa sasa ambao utakuwa na mwongozo wote wa athari za mabadiliko ya tabianchi kiafya,” amesema.

Akifafanua zaidi amesema majanga kama mafuriko yakitokea basi kuwe na njia ya ufikiaji na uhimilivu wa huduma ya afya, aidha matibabu kwa njia ya mtandao na ubunifu mwingine. 

“Wakati mwingine wanawake, watoto na masuala ya uzazi yanabakia nyuma sasa tumejadili namna ya kuingiza katika mpango wetu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Naye Ramadhan Hangwa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya Watu Duniani (UNFPA), amesema anaamini maoni na mapendekezo hayo yatachukuliwa na kufanyiwa kazi.