Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waomba Serikali kudhibiti mikopo ‘umiza’

Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Shinyanga Salome Makamba (kushoto) akimkabidhi zawadi mshindi wa chemsha bongo  Petronila Raphael mkazi wa Majengo Shinyanga ili kuwainuwa wanawake kiuchumi.

Muktasari:

Mikopo ‘umiza’ inayotolewa na watu binafsi mitaani imetajwa kuwa chanzo cha ndoa nyingi kuwa hatarini kuvunjika kutokana na baadhi ya wanawake kuweka dhamana ya thamani za ndani na hati za nyumba nakusababisha migogoro kwenye familia.

Shinyanga. Mikopo ‘umiza’ inayotolewa na watu binafsi mitaani imetajwa kuwa chanzo cha ndoa nyingi kuwa hatarini kuvunjika kutokana na baadhi ya wanawake kuweka dhamana ya thamani za ndani na hati za nyumba nakusababisha migogoro kwenye familia.

Hayo yameelezwa na baadhi ya wanawake wakati wakikabidhiwa zawadi ya Sh300,000 kupitia chemsha bongo ya Salome Makamba kwa kushirikiana na Radio Faraja kwa lengo la kuongeza ubunifu.

Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga, Mariam Senkondo amesema mikopo umiza imekuwa ni janga kubwa kwa wanawake kutokana na wengi kuikimbilia kwa kuwa mashariti yake ni nafuu na matokeo yake  wengine wanakimbia familia.

“Jamani wakina mama tunawakati mgumu sana, tunapenda mikopo ili tufanye biashara itusaidie lakini tunaumizwa na mikopo umiza wengine wanaita kausha damu ukisema uende benki mashariti ni magumu ndiyo maana wengi wanaishia mikopo umiza,’amesema Mariam

Mkazi wa Kambarage,  Vumilia Mtambalike ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwadhibiti watu wanaofanya biashara ya kukopesha fedha na kutoza riba kubwa ambayo imekuwa kama njia ya kuwakandamiza wenye kipato cha chini.

Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya shule za Sekondari kisha kuzungumza na makundi mbalimbali, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba amesema mikopo umiza imekuwa janga kubwa kwa jamii.

Makamba amesema kutokana na changamoto hiyo waliamuwa kuanzisha kampeni ya chemsha bongo kwa kushirikiana na Radio ya jamii Faraja ili kuwafikia wananchi wengi na kutumia fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na kupata elimu itakayowawezesha kujikwamuwa.

Amesema baadhi ya vikundi vya wanawake katika jamii kikiwemo cha Papo kwa papo kimeshinda zawadi ya Sh300,000  kupitia kampeni ya chemsha bongo, fedha ambazo zitasaidia kukuza mtaji wao badala ya kwenda kukopa mikopo umiza.

Akizungumzia suala la elimu, amewataka wanafunzi kuzingatia malengo waliyojiwekea ili wafikie ndoto zao na kuacha kujiunga na makundi ambayo hayana maadili pamoja na kutumia kampeni ya chemsha bongo kuongeza uelewa wao kwa kujifunza historia ya mambo mbalimbali.

Mkuu wa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Monica Sahele  amesema wamekuwa wakiona wanawake wanafanyiwa ukatili wa kiuchumi kupitia mikopo wanayochukuwa mitaani kwa watu binafsi jambo ambalo linawaumiza wakina mama.

Amesema njia pekee ya kuwasaidia wanawake ni kuwawezesha kiuchumi ili wafanye shughuli za kiuchumi ili kuwasomesha watoto wao ambao baadaye watakuwa na msingi mzuri na kutojihusisha na mikopo umiza.

Mratibu wa kampeni ya chemsha bongo, Simeo Makoba amesema lengo la kuuliza maswali kupitia chemsha bongo ni kuwafanya watu wajue mambo yanayoendelea nchini kupitia sekta mbalimbali pamoja na kujua historia ya mambo mbalimbali.