RC Manyara awataka walimu waachane na ‘kausha damu’

Muktasari:
- Walimu wamewatakiwa kuachana na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama mikopo umiza na kausha damu ila wakope fedha kwenye taasisi rasmi za fedha ikiwemo benki.
Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga walimu amewataka walimu kuachana na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama mikopo umiza au kausha damu na badala yake wakope fedha kwenye taasisi rasmi za fedha ikiwemo benki.
Sendiga ameyasema hayo leo Jumamosi Agosti 19 mjini Babati kwenye warsha ya Mwalimu Spesho iliyohusisha walimu 200 wa shule za msingi na sekondari iliyolenga kuwainua na kuwawezesha kiuchumi walimu na kuwapa fursa za mikopo.
Amesema mikopo rasmi inapatikana kwenye taasisi za fedha ikiwemo benki hivyo watumie fursa hiyo kuliko kuchukua mikopo umiza na kausha damu.
"Eneo kubwa lililoathirika na mikopo hii ni kada ya elimu na afya, Kwa kuweka bondi kadi zao za benki, tunapaswa kuachana na hayo kwani yanadhalilisha na kufedhehesha taaluma," amesema Sendiga.
Mmoja kati ya walimu hao, Abdalah Hussein amesema walimu wengi wanakimbilia mikopo ya kausha damu kutokana na masharti nafuu wanayopata.
"Mkopo benki ni hadi uwe na dhamana ya nyumba ila mikopo umiza ukiwa na mtungi wa gesi tuu unajitwalia zako kausha damu bila wasiwasi wowote ule," amesema Hussein.
Meneja wa benki ya NMB kitengo cha wateja maalum, Queen Kinyamagoha amewaahidi walimu hao kuwapatia elimu ya fedha ili waweze kutumia mikopo ipasavyo na kutimiza malengo yao.