Wanne wajeruhiwa ajali iliyohusisha basi, Coaster na Lori Mbeya

Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea leo Jumapili ,Julai 16, 2023 saa 12.30 za asubuhi katika eneo la mpakani mwa Makambako na Mbeya Kata ya Igurusi, Kijiji cha Mapungu, Tarafa ya Ilongo Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.
Mbeya. Watu wanne wamejeruhiwa katika ajali iliyotokea wilayani Mbarali, mkoani Mbeya leo Jumapili Julai 16, 2023 baada ya Coaster kugongana na basi la kampuni ya Fikosh linalofanya safari ya Mwanza kuja Mbeya.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Mstaafu, Denis Mwila amesema ajali hiyo imetokea saa 12.30 alfajiri katika kona iliyopo Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea leo ambapo basi la Kampuni ya Fikosh lililokuwa linatokea Mwanza kuja Mbeya limeigonga costa inayofanya safari kutoka Ubaruku kuja Mbeya na kusababisha kugongana na uso kwa uso na gari linguine (Lori) kisha kuanguka pembezoni mwa barabara,”amesema.
Ameongeza kuwa Coaster iliyogongwa kwa nyuma ni mali ya Umoja wa Madereva Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva Hemedy Bamboya (46).
Aidha Kanali Mstaafu Mwila amewataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Mathias Mashala (59) Mkazi wa Wilaya ya Mbozi, Justina Stephano (Mkazi wa Mbozi), Ngimba Mashala (43) na Ombeni Given (23) wote walikuwa wakisafiri kwenye basi la Kampuni ya Fikosh lililokuwa likitokea Mwanza kuja Mbeya.
Mwila amesema hadi sasa (saa 5. 46 asubuhi) kutokana na taarifa za daktari, majeruhi watatu wameruhusiwa na mmoja bado anaendelea na matibabu.
Diwani Kata ya Igurusi, Hawa Kihwele amesema ajali hiyo imetokea eneo la mpakani mwa Mbeya na Makambako kijiji Mapungu Kata ya Igurusi tarafa ya Ilongo.
“Hilo eneo ni baya sana mara kwa mara zinatokea ajali na watu kupoteza maisha tunaiomba Serikali kuangalia namna ya kufanya upanuzi wa miundombinu ya barabara ili kunusuru maisha ya Wananchi,”amesema.