Wanawake wanolewa elimu ya matumizi nishati safi ya kupikia

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), Janeth Mbene akizungumza na wanawake wajasiliamali wa Wilaya ya Kinondoni katika semina ya nishati safi ya kupikia, iliyoandaliwa na shirika lisilo la kisetikali la TAWEN jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Wanawake wa Wilaya ya Kinondoni wameendelea kupewa elimu ya matumizi safi ya nishati safi ili kulinda afya zao na kukuza uchumi wao.
Dar es Salaam. Katika jitihada za kuhakikisha wanawake wanaondokana na matumizi ya kuni na mkaa, Mtandao wa Kuwezesha Wanawake Tanzania (Tawen) umeendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kundi hilo.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya serikali yaliyotolewa Juni 8 mwaka huu na Waziri wa Nishati, January Makamba kwenye kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi lilofanyika Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza katika kongamano lilofanyika, Kinondoni, Dar es Salaam leo, Agosti 02, 2023, likiwa na Kaulimbiu ya 'Mkaa na Kuni Sasa Basi', Mkurugenzi wa Taasisi ya Tawen, Frolence Masunga amesema kampeni hiyo inayolenga kuunga mkono juhudi za serikali wanatarajia kutembelea mikoa mbali mbali nchini.
"Serikali imeweka mpango hadi kufikia Mwaka 2025 asilimia 80 ya Watanzania wote wawe wanatumia nishati safi katika sekta ya chakula ili kulinda afya na mazingira kwa ujumla," amesema
Amesema katika kuona namna ya kuwafikia wanawake wote, Masunga aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake mkoa wa Dar es Salaam, (UWT) amesema elimu hiyo itawafikia hadi vijana wanaosoma elimu ya ngazi ya vyuo.
Kwa upande wake, akizungumza kwenye kongamano hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kinondoni kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Shedrack Maximilian amesema elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa jamii kuwa na uelewa mpanga juu ya nishati safi.
"Tunaomba elimu hii iendelee kuja hasa kwenye ngazi mbalimbali kata hadi mitaa watu wajue hasa sekta ya chakula waweze kutumia fursa hiyo na Kinondoni tunamatumizi makubwa ya nishati isiyo safi," amesema.
Amesema kuna watu wengi wanapata madhara kutokana na matumizi ya nishati isiyo sahihi na kuna maeneo mengi nchini yanabaki jangwa kutokana na ukataji miti.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Manispaa ya Kinondoni, Magreth Jackson amesema shughuli wanazozifanya mamantilie na wachoma chipsi wanatumia zaidi kuni na mkaa tumeona tuwatoe huko watumie fursa ya nishati ya gesi.
"Serikali inamifuko mbalimbali kuwasaidia wanawake na tunawasihi waliochukua mikopo kurejesha kwa wakati ili wenzetu waweze kukopeshwa na wapate nishati ya mitungi ya gesi," amesema Magreth.