Prime
Ndani ya Habari: Misitu yateketea, gesi bado haijawavutia wananchi wengi

Pwani. Wimbo wa mazingira ni mtamu unaposikika kwenye masikio ya watu, lakini kwa macho na masikio ya kawaida, wimbo huo ni mchungu kama shubiri.
Kila kona ya Tanzania wanaimba mazingira, watoto wa shule wanaimba mazingira, nyumba za ibada nako pia mazingira.
Ni nani ameachwa katika hili, kwa nini vita hii inawashinda Watanzania zaidi ya 60 milioni?
Serikali ilishatangaza kuwa, mazingira ni ajenda mtambuka ambayo kila mahali inapaswa kuzungumzwa, licha ya kuwa wengi hawana meno ya kung’ata hata wanapoona mazingira yanaharibika.
Kwa kiasi kikubwa suala la mazingira linaanzia na ukataji wa miti. Kupotea kwa miti ndiko kunasababisha jangwa, hali mbaya ya hewa, ukosefu wa maeneo ya kupumulia kwa miji mikubwa, lakini ni chanzo cha mafuriko.
Miti inakatwa kwa ajili ya matumizi ya mambo kadhaa ikiwemo ujenzi, samani lakini kwa kiasi kikubwa ukataji wa miti unaochukua nafasi kubwa ni kwa ajili ya kuchoma mkaa na uandaaji wa mashamba.
Ofisa Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki kitengo cha matumizi masoko na mipango Mkama Kusaga, anakiri kuwa hali ni mbaya kwenye baadhi ya misitu na kwamba chanzo chake ni shughuli za kibinadamu.
Kusaga anataja matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya nishati ya kupikia, ndiyo yanamaliza misitu hata wakati mwingine watu wanaingia usiku kwenye misitu minene kwa ajili ya kutafuta upenyo wa kukata miti ya mkaa jambo ambalo ni la hatari kwao.
Kwa mujibu wa Kusaga, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 pekee jumla ya magunia yaliyovunwa kwa kufuata utaratibu ndani ya Mkoa wa Pwani ni 33,8519 licha ya ukweli kuwa wengi wanavuna kwa njia za panya na hawapo kwenye hesabu.
"Idadi hiyo tunaipata kutokana na jumla ya wasafirishaji na wavunaji tuliowasajili kwa kipindi hicho ambao idadi yao ni 375 na kwamba hao walifuata sheria za uvunaji endelevu na walitambuliwa hata kwa kulipa kodi," anasema Kusaga.
Anafafanua kuwa, takwimu hizo hazijumlishi kiasi chote cha magunia ya mkaa yaliyozasilishwa kwa kipindi hicho kwani baadhi ya wananchi wamekuwa wakikata miti na kutengeneza nishati hiyo kwa njia zisizo rasmi na hawajasajiliwa katika utaratibu.
Akizungumza kuhusu suluhisho la changamoto hiyo, anasema hakuna namna kama jamii itaendelea kung’ang’ania katika matumizi ya nishati ya kuni bila kuingia kwenye matumizi ya gesi, kwani idadi ya watu kila uchwao inazidi kuongezeka hivyo lazima kuwe na tatizo.
“Vita ni kubwa na sisi tunaendelea kupambana kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii ili itambue kuwa lengo siyo kuzuia kabisa ukataji wa miti bali kinachotakiwa ni kuvuna misitu kwa kufuata utaratibu ili iwe endelevu,” amesema.
Anashauri kuwa kuna umuhimu wa jamii kubadilika kwa kutojikita kwenye matumizi ya mkaa pekee kwa kupikia, bali iangalie hata namna ya kuhamia kwenye matumizi ya gesi kwa ajili ya nishati ya kupikia
Agizo la Waziri Mkuu
Kauli ya mtaalamu huyo wa misitu inakwenda sambamba na agizo alilotoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akihitimisha mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma hivi karibuni ambapo alisema sasa ni lazima watu wakubali kuhamia kwenye gesi.
Majaliwa alisema kuwa Rais alishaagiza kuwa, kila mwananchi aanze kutumia gesi ili ifikapo 2030 lengo la asilimia 80 ya Watanzania kuwa wanatumia nishati ya gesi liweze kutimia.
“Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa, kila Mtanzania ahamie kwenye matumizi ya gesi, taasisi zote zinazohudumia watu kuanzia 100 lazima muanze kutumia gesi kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi misitu yetu,” alisema Majaliwa.
Hata hivyo, kiongozi huyo anakiri kuwa inatakiwa elimu ya kutosha ili kuwahamasisha wananchi kutambua kuwa nishati ya gesi ina gharama ndogo na haina madhara ukilinganisha na matumizi ya kuni na mkaa.
Wasemavyo wananchi
Akizungumzia suala la matumizi ya kuni ukilinganisha na mkaa, mkazi wa Mailimoja Kibaha Mwajuma Mvungi yeye anasema katika majaribio yake, amebaini kuwa mkaa una gharama nafuu kuliko gesi ambayo kwake anaona ni kwa matajiri na wenye uwezo.
Mwajuma anataja kipimo kimoja cha mkaa katika maeneo yao kinauzwa kati ya Sh1,500 hadi Sh2,000 na kwamba anapikia siku nne hadi tano hivyo anaona ni rahisi kwake na angetamani kuendelea kutumia mkaa.
“Hapo naweza kupikia makande na vyakula vingine na mkaa ukabaki lakini gharama ambazo nitakuwa nimetumia haziniumizi, kwani zinaendana na kipato changu cha chini hivyo mimi naona mkaa unarahisisha gharama kuliko huko kwenye gesi,” amesema.
Alipoulizwa kama amewahi kutumia gesi na kujaribu kufanya mlinganisho, alisema hajawahi na kwamba, amekuwa akiogopa hasa anapoona watu wanachukua muda mfupi kuwa wamekamilisha kupika chakula na akasema gharama ya Sh50,000 kununua mtungi wa gesi kwake anaona ni anasa.
Kwa upande wake, Alfa Gama wa Kibaha Vigaeni anasema matumizi ya gesi kwa kupikia yanarahisisha mapishi pia gharama yake ni nafuu ikilinganishwa na mkaa lakini gesi ni salama hata kwa afya.
Gama anasema kuwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kg 6 hujaza kwa Sh23,000 lakini matumizi yake ni zaidi ya miezi miwili hivyo kwake anaona kabisa kwamba inaokoa gharama.
“Kama ningekuwa nanunua mkaa, kwa siku ningetumia Sh1,000 ambayo kwa mwezi ingekuwa ni Sh30,000 na hapo ujumlishe usumbufu wakati mwingine mkaa hauwaki halafu na wewe unakuwa na haraka zako hivyo inakuwa ni vurugu,” anasema Gama.
Hata hivyo anakiri kuwa, wananchi wengi hawajapata elimu kuhusu matumizi ya gesi lakini kama wataelimishwa kwake anaona hakutakuwa na mtu ambaye anaweza kuendelea kutumia kuni au mkaa.
Akizungumzia juu ya umuhimu na tofauti ya matumizi ya gesi na mkaa, mtaalamu kutoka Taifa Gesi (LPG), Angel Bhoke anasema iko tofauti kubwa hata kiuchumi ambayo inawezesha kuokoa fedha na muda kwa wanaotumia gesi.
Bhoke amesema moja wapo ya faida hizo ni kulinda mazingira jambo ambalo linajionyesha hadharani kuwa nishati ya kupikia ndicho chanzo cha uharibifu wa mazingira.
“Zipo faida nyingi za kutumia gesi kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine, kwanza usalama wa kiafya kwa mpishi kuepukana na moshi lakini inaokoa muda na haina harufu kama kuni au mkaa,” amesema.
Anasema katika kuunga mkono mapambano ya uharibifu wa mazingira, kampuni yao imeweka mitungi ya bei ya chini.