Viongozi wa dini waonya mambo manne kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa akizungumza wakati wa kongamano la kuelimisha tunu za taifa kwa viongozi wa dini mkoani Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Muktasari:
- Tunu saba za taifa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa, ambazo viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza wanaamini zikifuatwa na kuheshimiwa, hakutakuwa na uvunjifu wa amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mwanza. Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke, amesema matumizi ya lugha za matusi na kudhalilisha utu miongoni mwa wanasiasa, pamoja na uzembe wa baadhi ya vyombo vya dola katika kushughulikia masuala ya rushwa na ukosefu wa uwazi katika utoaji wa matokeo ya uchaguzi, ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuchochea machafuko na kuhatarisha tunu za taifa katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Sheikh Kabeke, ambaye pia ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Aprili 19, 2025, wakati wa kongamano la kuhamasisha tunu za taifa kwa viongozi wa dini mkoani humo kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke akizungumza wakati wa kongamano la kuelimisha tunu za taifa kwa viongozi wa dini mkoani Mwanza. Picha na Damian Masyenene
Kongamano hilo lilihusisha makundi mbalimbali, ikiwemo bodaboda, machinga, vyombo vya dola na wanasiasa, likibeba kaulimbiu isemayo: "Kulinda amani na kuenzi tunu za Taifa kwa mustakabali wa nchi."
Amesema baadhi ya vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi, vinashindwa kutimiza wajibu wao kwa kutenda haki, na kujikuta vikishiriki kusindikiza wagombea watoa rushwa wakati wa uchaguzi, ama kuwakamata baadhi ya wagombea na kuwabeba wengine.
“Kuna maeneo mengine wakati wa uchaguzi unaambiwa ‘Sheikh, mimi nimepigwa asubuhi kwa sababu mwenzangu alikuwa anatoa rushwa na alisindikizwa na vyombo vya dola. Hii ni aibu. Tunataka Takukuru wasimamie uadilifu na kudhibiti rushwa kwenye vyama.
“Uchaguzi utakapofika tupate mtu sahihi, haijalishi ni nani. Sisi tunataka Mtanzania kama ana sifa hizo, umaskini wake haumuondolei sifa ya kuwa kiongozi,” amesema Kabeke.
Kabeke amewaonya baadhi ya wanasiasa wanaochochea machafuko kwa kisingizio cha kudai haki, kwani taifa likiingia kwenye machafuko, haki wanazozitaka hazitapatikana. Badala yake, wanatengeneza taifa lenye wananchi wasio na adabu na wasiokuwa na heshima kwa viongozi wao.
“Kuna watu wanasema, ‘masheikh na viongozi wa dini wameshanunuliwa, wanasema tu amani, mbona hamsemi haki?’ Jamani, hauwezi kuleta haki kama hamna amani. Sasa viongozi wa dini hawa si wajinga, wanahimiza lile ambalo linaweza kufanya hiyo haki ipatikane,” amesema Kabeke.
Ameongeza kuwa,“chama cha siasa, lengo lenu ni kushika nchi, halafu mnahamasisha vijana kuwa wavunja sheria. Siku mkitawala, nyie hao vijana mtawabadilishaje? Tujaalie CCM imeondoka madarakani, mmekaa pale nyie chama B au C, lakini mlishawatengeneza vijana na wafuasi wenu kuwa kasoro-adabu, mtawabadilishaje?”
Akiunga mkono hoja hizo, Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa, amesema kuelekea uchaguzi mkuu, mambo yanapaswa kufanyika kwa uwazi na ushirikishwaji ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima. Amesema utawala bora ukitekelezwa ipasavyo utaepusha manung’uniko, machafuko na mapigano.
Sekelwa, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, amesema kinachotakiwa katika kuzitunza tunu za taifa ni nidhamu, huku akiwataka viongozi wa kisiasa, dini na watendaji wa Serikali kuwa wazalendo, na kuuishi uzalendo kwa kusimamia wanachokizungumza na si kubadilikabadilika kutegemeana na wanayekutana naye.
“Tunatazamia viongozi wa Serikali kuilinda, kuiheshimu na kuifuata Katiba inavyosema badala ya kuivunja. Sisi tunahangaika na amani, lakini wakati mwingine inavunjwa na viongozi wanaotuongoza kwa kukiuka maadili, sheria na Katiba.
“Watendaji wa Serikali watii Katiba, wanasiasa watii sera na miongozo ya vyama vyao, na viongozi wa dini watii maandiko ya Mungu. Kinyume chake, watakuwa wamekosa maadili,” amesema Sekelwa.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Chagu Ng’oma, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wananchi kutofuata mkumbo wakati wa upigaji kura kwa kutowapigia kura wanasiasa wenye ahadi za kusadikika.
Amekiri kuwa, endapo viongozi wa Serikali wakiwajibika ipasavyo, vurugu zote zitakwisha.
“Wapigakura, twende tukapige kura inavyotakiwa. Tuachane na kwenda na upepo wa kisiasa. Usimpigie kura mwanasiasa ambaye unaona kabisa ana ahadi ambazo kiuhalisia hazitekelezeki. Unakubali kuchukua utu wako na kuuza kwa sababu ya Sh200.
“Wanasiasa wafike sehemu waridhike na wanachokipata, wazungumze kwa uwazi bila kudanganya, na wakati wa kusimamia, wasimamie kwa haki,” amesema Ng’oma.
Mchunguzi Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Protasi Andrew, amewaomba viongozi wa dini kushirikiana na taasisi hiyo kuhubiri na kukemea vitendo vya rushwa kuanzia kwenye chaguzi za ndani za vyama vya siasa hadi kwenye uchaguzi mkuu, ili kuhakikisha taifa linapata viongozi watakaotetea maslahi ya umma kuliko ya kwao binafsi.
“Tunapokwenda kuweka dola madarakani, si jambo ambalo ni la mchezo. Tunakwenda kuweka mustakabali wa nchi yetu na maisha yetu. Watoto na wajukuu ni jambo ambalo hatutakiwi kufanya makosa. Hizi tunu ambazo zimeongelewa, kimsingi, inabidi tuzihubiri kila mmoja ili tutembee na lugha moja. Maana tukikosea tunu mojawapo, tutakuwa tunaiweka nchi yetu katika hali ya hatari na kuvunja amani. Msije mkakosea,” amesema Andrew.

Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo, akiwemo Mchungaji wa Kanisa la Qavah Pentecostal, Upendo Isaya, ameshauri elimu ya tunu za taifa itolewe kuanzia ngazi ya familia ili kudumisha amani, upendo na kutoa haki kuanzia ngazi ya chini.
Naye Leonidas Thomas, Katibu wa Kamati ya Amani Wilaya ya Misungwi, amesema, “Takukuru wasipendelee katika ukamataji wa wala rushwa wakati wa uchaguzi, jambo hili siyo jema. Tunasikia kwamba wamekuwa wakikamata wagombea wa vyama fulani, lakini vingine vinafanya vitendo kama hivyo tena hadharani na haviguswi. Hiyo siyo sawa.”