Serikali kupunguza gharama za gesi

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato
Muktasari:
- Katika kukabiliana na changamoto ya matumizi ya kuni na mkaka, Serikali imesema inaboresha na kuona namna ya kuendelea kupunguza gharama za mitungi ya gesi.
Dodoma. Serikali imesema inaangalia namna nyingine ya kupunguza gharama za gesi ya viwandani ili kila mwananchi aweze kutumia nishati hiyo.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 21, 2023 na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema) Aida Khenan.
Mbunge huyo alisema wananchi wa vijijini wanatumia nishati ya kuni kwasababu ndiyo nishati inayopatikana kwa urahisi kwenye maeneo yao.
“Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala ambayo ni gesi asilia ili iendane na nguvu tunayotumia ya kupika marufuku matumizi ya kuni na mkaa?” amehoji.
Akijibu swali hilo, Byabato amesema anakubaliana kuwa watu wengi wanatumia kuni na mkaa na kwamba Serikali imeanza jitihada za kukabiliana suala hilo na kwa kuanzia njia ambayo imeonekana ni rahisi zaidi ni matumizi ya nishati ya gesi ya viwandani.
Amesema jitihada nyingine ni kuwezesha kupata mitungi ya gesi ya viwandani katika mwaka huu wametenga mitungi 70,000 na mwaka 2023/24 watatoa mitungi 200,000 ili kutoa mtaji wa mwananchi kuanza kutumia nishati mbadala.
“Tunaboresha na kuona namna ya kuendelea kupunguza mitungi ya gesi ili wananchi waweze kuimudu katika maeneo yao. Serikali inaweka ruzuku lakini tutaangalia namna nyingine ya kupunguza gharama hizi ili kila mwananchi aweze kutumia gesi hii,” amesema.