Wanawake vijijini wanolewa haki ya kumiliki ardhi

Muktasari:
- Katika kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wanawake wa vijijini wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa kupambana na mila kandamizi zinazosuia wanawake kumiliki ardhi
Morogoro. Wanawake kutoka katika vijiji mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi na kupewa mbinu za kupambana na mifumo kandamizi inayosababisha wawekwe pembeni kwenye suala hilo.
Baadhi ya wanawake hao wamekiri kuwa bado mila na desturi kandamizi zinawazuia kumiliki ardhi kwa kuonekana kama wao ni watu wakuolewa na hivyo hawana haki hiyo.
Mafunzo hayo yametolewa mjini Morogoro na Shirika la kimataifa linalojihusisha na masuala ya ardhi la Landesa, Pelum Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Meda yakiwa na lengo likiwa kuendeleza kampeni ya kidunia ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi.
Akizungumza jana Machi 4 mkoani hapa, Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la Landesa, Godfrey Massay amesema utafiti unaonyesha licha ya kuwa wanawake wengi ni wakulima lakini idadi ya wanaomiliki ardhi ni ndogo kutokana na mfumo dume.
“Bado wanawke wamewekwa pembeni kwenye masuala ya ardhi, ukiangalia kwenye kilimo ni wengi wanalima sasa njoo kwenye umiliki wa ardhi, wachache wanamiliki ardhi. Hakuna uchumi wa mwanamke kijijini kama ardhi anayolima haimiliki,” amesema Massay.
Kwa upande wake, Ofisa Jinsia kutoka Meda Tanzania, Lilian Mosha amesema kama mwanamke hana maamuzi kwenye ardhi anayofanyia kazi hawezi kufanikiwa kiuchumi.
“Ndio maana nasema ni haki ya mwanamke kama ilivyo kwa mwanaume kumiliki ardhi. Hii itasaidia kuinua uchumi,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa miradi, Jinsia na Wanawake kutoka Pelum Tanzania Anna Marwa alisema kinachosababisha wanawake wengi hasa vijijini kushindwa kumiliki ardhi ni mila na desturi kandamizi pamoja na hali ya uchumi.
“Kwa hiyo elimu ndiyo pekee itakayosaidia katika mapambano haya na kwa kuanza tumekuja na mafunzo haya kwa wanawake zaizi ya 40 kutoka katika vijiji mbalimbali. Wanawake hao wakirudi vijijini watakuwa sauti kwenye masuala ya ardhi,” amesema.
Baadhi ya wanawake waliopewa mafunzo hayo wamesema pamoja na kupewa elimu hiyo, waume zao pia wanapaswa kupewa elimu ili kuwe na mabadiliko.
“Nikienda nitatoa elimu lakini baba akisema nyamaza nitakosa nguvu, tunaomba mje mpaka vijijini kule wanasema ukiolewa wewe unatakiwa kutumia ardhi ya hukohuko hata kurithi, wanawake hatupewi kipaumbele,” amesema Amina Hamis, Mwenyekiti wa Kijiji cha Jenjeluse, Chemba Mkoani Dodoma.